HEADER AD

HEADER AD

WAZAZI WASHINDWA KUCHANGA 15,000 YA MADAWATI SHULE YA REGORYO

>>>Wanafunzi wakaa chini huku viatu wakiacha nje

>>>Shule haina choo cha walimu

>>>Vitabu vyatunzwa chini ya sakafu

Na Dinna Maningo, Tarime

BAADHI ya Wanafunzi katika shule ya msingi Regoryo iliyopo Mtaa wa Regoryo Kata ya Nkende, katika Halmashauri ya Mji Tarime Mkoa wa Mara, wanalazimika kukaa chini ya sakafu kutokana na upungufu wa madawati huku wakivua viatu na kuviacha nje ya darasa.

Shule hiyo ilisajiliwa mwaka jana 2022 na kuanza rasmi kupokea wanafunzi Januari, 9, 2023, ina jumla ya madawati 107 kati ya hayo 100 ni ya Serikali na saba yamenunuliwa na wazazi huku ikiwa na idadi ya wanafunzi 546 wa darasa la awali hadi darasa la nne na walimu saba .

            Shule ya msingi Regoryo

Kuwepo kwa changamoto ya madawati kamati ya shule kwa kushirikiana na Wananchi na Serikali ya Mtaa wa Regoryo na Kwibanga walikubaliana wazazi kuchanga fedha kununua madawati ambapo walikubaliana muda wa mwezi mmoja madawati yawe yametengenezwa na kupelekwa shuleni.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Regoryo Yamed Mekere Nyeitange amesema kuwa Januari, 2023 kilifanyika kikao cha wazazi na kukubaliana kutengeneza madawati ndani ya mwezi mmoja lakini muda umeisha wazazi hawajapeleka madawati.

         Mwenyekiti wa Mtaa wa Regoryo Yamed Mekere Nyeitange 

"Kamati ya shule walisema kuna changamoto ya madawati tukakaa mitaa miwili ambayo ndio imejenga hiyo shule tukakubaliana na wazazi kwamba wazazi wanne waungane watengeneze dawati moja ambalo thamani yake ni Tsh. 60,000, ambapo kila mzazi atachangia Tsh. 15,000.

"Madawati hayo wanatengeneza wenyewe kwa fundi kisha wanapeleka shuleni wanamwambia mwalimu kuwa ni dawati kwa ajili ya wanafunzi fulani na fulani, wanafunzi wanapewa wanakaa dawati moja wanne lakini wazazi wachache ndio wametengeneza.

"Wengine wanasema hali ni ngumu tuwaongezee muda wa mwezi mmoja watengeneze kwakuwa njaa ilipiga sana pesa iliyokuwa ikipatikana ununua chakula ili kulisha familia, kwahiyo wanafunzi wengine wanaketi chini"Amesema Yaredi.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa baadhi ya madarasa yenye madawati pungufu wanafunzi wanapotaka kuingia darasani huvua viatu na kuviacha nje.

     Darasa ambalo viatu vimeonekana nje ya mlango

"Hufanya hivyo ili darasa lisichafuke kwakuwa wengine wanakaa chini, wakiingia na viatu darasa litachafuka sio vizuri wakae kwenye uchafu wakati wanakaa chini, na sasa hivi tumeingia msimu wa mvua, mwanafunzi anafika matope yamejaa kwenye viatu"amesema Yaredi.

Shule hiyo ina choo kimoja cha wanafunzi chenye matundu 8 ikiwa na upungufu wa matundu 13. Haina choo cha walimu wanalazimika kutumia vyoo vya wanafunzi, haina ofisi ya mkuu wa shule hivyo kuchangia ofisi moja na Walimu.

Pia shule haina mkataba, kabati ya kutunza vitabu, walimu wanalazimika kutunza vitabu vya shule chini ya sakafu, haina viti na meza kwa ajili ya walimu, haina bendera ya Taifa, hakuna kibao cha shule, picha ya Rais na kitabu cha kusaini wageni.

Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Regoryo amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi ambapo ujenzi ulianza tangu mwaka 2013, ina madarasa matano, matatu yaliyojengwa na wananchi wa mtaa huo na madarasa mawili, ofisi moja  na choo yaliyojengwa na wananchi wa mtaa wa Kwibanga.


"Wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu km.4 kwenda shule ya msingi Nkende, Rebu, na Nyamwino, wakati wa mvua walipata shida kuvuka mto walilazimika kuzunguka mahali ambako kuna vivuko salama.

"Kutokana na changamoto ya umbali tukaona shule ianze mahitaji mengine yataendelea kufanyika wakati watoto wakiwa wanaendelea kusoma. 

"Wanafunzi waliokuwa wanasoma kwenye hizo shule wa darasa la kwanza hadi la nne ambao wanatoka kweye mitaa hii ilibidi wahamishwe waje kusoma kwenye hii shule ili kuwapunguzia mwendo".amesema Yaredi.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa katika kuunga juhudi za wanachi, Serikali imejenga madarasa mawili pamoja na ukamilishaji wa madarasa yaliyojengwa na wananchi.

              Madarasa yaliyojengwa na serikali

"Wananchi walijenga madarasa matano, Mbunge Kembaki alituezekea mabati madarasa yote, Diwani nae akatuwekea milango 5 ya magrili, akatuletea madawati 60 , Serikali ikaleta madawati 40 na kutujengea madarasa mawili kutoka chini hadi ukamilishaji ikiwemo upigaji lipu na upakaji rangi.

"Pia ikaweka madirisha, wananchi wa mtaa wangu walichimba shimo la choo lakini nguvu imekwisha wanaiomba Serikali iwasaidie kuwajengea choo maana vilivyopo havitoshelezi mahitaji" Amesema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwibanga Daud Magabe amesema mtaa wake umejenga vyumba 2 vya madarasa, ofisi moja ya walimu na choo cha wanafunzi chenye matundu 8.

                                       Choo

"Wanamtaa wamejenga madarasa mawili , wamejenga choo kwa nguvu zao kuanzia uchimbaji shimo hadi kuezeka na kupiga lipu. Rangi tuliomba iliyokuwa imebaki wakati wa upakaji rangi vyumba vya maasundi akatupakia.

"Tunamshukuru mbunge, diwani na Serikali kwa kuunga mkono juhudi za wananchi. Kuanzishwa kwa shule hii kumewanusuru wanafunzi kutotembea umbali mrefu kwenda kusoma shule zilizo mbali  km.3-4.

Mwenyekiti huyo amesema kwamba shule hiyo ni mpya bado haijaanza kupokea fedha za uendeshaji wa shule hivyo anawaomba wadau mbalimbali kuunga juhudi za wananchi ili kuondoa changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema kuwa mbali na changamoto ya fedha baadhi wameshindwa kutoa mchango kwakuwa wamekuwa wakisikia kupitia Vyombo vya Habari marufuku ya wananchi kuchangishwa michango shuleni.


"Tulisikia kwenye vyombo vya habari Rais na viongozi wengine wa Kitaifa wakisema hakuna wananchi kuchangishwa michango, Wenyeviti wa Mitaa nao wanasema watu wachangie madawati, wengine wamekataa wakihisi huwenda Serikali imetoa fedha za madawati ila viongozi wamekula.

"Ni kweli madawati ni machache wanafunzi wengine wanakaa chini, kwanini Serikali isinunue madawati wakati wananchi wamejenga madarasa? hii inakuwa ni mzigo kwa wananchi, shule imeshasajiliwa changamoto zilizobaki Serikali imalizie"Amesema Ghati Chacha.

Wenyeviti hao wamewapongeza wananchi kwa michango iliyofanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa huku wakiwahimiza kutengeneza madawati ili kuondoa changamoto hiyo kwa wanafunzi.








No comments