TET YAFAFANUA TAARIFA ZA UPOTOSHWAJI KITABU KIPYA CHA HISABATI
Na Andrew Chale, Dar es salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba imetoa ufafanuzi wa taarifa iliyochapishwa katika Gazeti la Mwananchi la Jumamosi tarehe 4, Machi, 2023 lenye namba ISSN 0856-7573 NA. 8239 yenye kichwa cha habari Madudu tena Kitabu Kipya cha Hisabati.
Amesema kuwa taarifa hiyo ni ya upotoshaji kwa kile alichodai kuwa maeneo yaliyotajwa hayaathiri ujifunzaji na ufundishaji na hayapotoshi wanafunzi kama taarifa inavyoeleza.
Ameongeza kuwaTaasisi imepokea maoni mbalimbali kutoka kwa watumiaji wa mwisho juu ya ubora wa kitabu tajwa.
"Sura ya kitabu inayolalamikiwa imeandaliwa kukidhi mahitaji ya muhtasari na ina lengo la kumuwezesha mwanafunzi kupata msingi wa kiuhasibu ili aweze kutumia maarifa haya katika maisha ya kila siku.
Kanuni nyingine zote za kiuhasibu zimeelezewa bayana katika vitabu vya masomo ya uhasibu Kidato cha 1-6.
"Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu ilitoa Waraka Na. 4 wa Mwaka 2014, kuhusu utayarishaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Amesisitiza kuwa katika waraka huo, kazi ya kuandaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia inasimamiwa na TET ili kufanikisha kazi hiyo na kwamba TET iliandaa miongozo ya uandishi, tathimini na uidhinishwaji wa vitabu vya kiada na ziada.
"Kwa kutumia miongozo hiyo, uandishi, uhariri na tathimini ya vitabu vya kiada hufanywa kwa kushirikiana na wataalamu bobezi kutoka sekta za umma na binafsi zikiwemo taasisi za elimu za juu, vyuo vya ualimu, na shule.
Amesema mpaka sasa TET imeweza kuandika jumla ya vitabu 361 vya kiada na kusimamia uidhinishaji wa vitabu 433 vya ziada, ambapo vitabu vya kiada vinapatikana bure katika maktaba mtandao ya TET kupitia kiunganishi http://ol.tie.go.tz "
"Mwisho, TET inaujulisha umma kuwa imeweka mfumo wa kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu machapisho na masuala mengine yote yanayohusu mitaala, vitabu na mafunzo kwa walimu.
Maoni hayo ni fursa ya kuendelea kuboresha machapisho hayo na kuhakikisha kuwa yanakidhi mahitaji ya jamii na yanaiwezesha Serikali kufikia azma yake ya kutoa elimu bora kwa kila Mtanzania.
Hivyo, amewaomba wadau wote kutumia fursa hiyo kutuma maoni kupitia barua pepe ya Mkurugenzi Mkuu kwa anuani ya director.general@tie.go.tz. ".
Mkurugenzi huyo ametoa taarifa ya ufafanuzi yenye saini yake.
Post a Comment