AWESOME EXPEDITION : BURUDANI ZA ASILI ZITUMIKE KUKUZA UTALII MARA
Na Dinna Maningo, Mara
IMEELEZWA kuwa Matamasha ya asili yakitumiwa vyema yatasaidia kukuza Utalii katika mkoa wa Mara lakini pia ni chanzo cha uchumi kwakuwa yanatoa fursa ya watu kujitangaza kupitia maonesho na burudani.
Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition yenye makao yake makuu mkoani Arusha, kupitia mpango wake ujulikanao Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, imesema kuwa mkoa wa Mara kuna makabila mbalimbali yanayodumisha michezo na burudani za asili kama njia ya kutunza na kudumisha utamaduni.
Afisa Masoko katika Kampuni ya Awesome Expedition, Daines Yahya Hemed amesema mkoa wa Mara ukitumia vyema matamasha ya asili yatasaidia kukuza Utalii wa mkoa huo ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
"Matamasha ya asili yana mchango mkubwa katika kukuza sekta ya Utalii, mkoa wa Mara tuyatumie katika kukuza Utalii wa Mara kupitia maonesho ya ngoma za asili" amesema Daines.
Amesema mkoa Mara kuna makabila mbalimbali yana ngoma au burudani za asili hivyo zikutumiwa vizuri zitasaidia kuwavutia watalii kuendelea kuvitembelea vivutio vya mkoa huo.
Burudani hizo za asili ni pamoja na Ritungu, Rilandi kutoka kabila la Wakurya, kabila la Wajita wenye burudani ya asili maarufu ngoma ya Kadogoli, ngoma ya Waluo kwa kabila la Wajaluo na makabila mengineo yaliyopo katika mkoa huo.
"Pamoja na kuwa na hizo burudani za asili je mkoa wa Mara tunazitumia vipi katika kukuza utalii pindi watalii wanaotembelea vivutio vyetu vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara?.
"Ni vyema watalii wanapoingia mkoa wa Mara tuzitumie burudani za ngoma zetu za asili kama kivutio cha watalii wajue utamaduni wetu.
"Tufanye hivyo kama wafanyavyo Wamasai pindi watalii wanapoenda kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na Arusha huonesha matamasha ya asili na hivyo kujipatia fedha na kuutangaza utamaduni wao Kimataifa.
" Tuwe na matamasha ya asili, istoshe matamasha ya asili ni chanzo cha uchumi kwani yanatoa fursa ya kujitangaza kibiashara, yanasaidia kuutangaza mkoa au Nchi, yanasaidia kufufua mila zinazopotea.
"Yanasaidia kuibua au kubaini vyanzo vipya vya utalii na yanasaidia kukuza utalii kwa wale wanaopenda kujifunza toka kwa wengine"amesema Afisa huyo wa masoko.
Daines amesema wananchi wa mkoa wa Mara wanaweza kutumia fursa ya matamasha ya asili kujiinua kiuchumi na kwamba yakifanyika yatasaidia kuhamasisha utalii wa mkoa wa Mara
Amesema matamasha hayo ni pamoja na matamasha ya ngoma au burudani za asili, vitu au vifaa mbalimbali vya asili,mavazi ya asili, mapishi ya vyakula vya asili, vinywaji vya asili, matambiko, michezo ya asili na matamasha ya ulinzi wa asili.
Je Kampuni ya Awesome Expedition inashiriki vipi katika kuhamasisha matamasha ya asili katika kukuza Utalii nchini?
Afisa Masoko wa Kampuni hiyo amesema" Tunatumia matamasha ya asili kutangaza utalii kwa kufanya matukio au kazi mbalimbali za sanaa, biashara, na burudani za jadi.
"Tunafanya matangazo mbalimbali kabla ya kuanza matamasha au matukio, mpango mkubwa au kabambe wa kuleta watalii nchini na kuongeza spidi ya ubunifu mkubwa katika matukio ya kiasili" amesema Daines.
Daines amewaomba wananchi wa mkoa wa Mara kutumia matamasha ya asili kuutangaza Utalii wa mkoa huo lakini pia Kutumia mbinu za asili kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Post a Comment