JAMII YATAKIWA KUTOA TAARIFA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA
Na Samwel Mwanga, Bariadi
JAMII imetakiwa kutoa taarifa za vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vinavyofanywa na watu katika maeneo mbalimbali badala ya kuona kama ni mila na desturi.
Afisa Ustawi wa jamii,Halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu,Wamdenge Kalingoji amesema hayo kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Sapiwi na Dutwa wilayani hapa wakati akitoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa jamii .
Afisa Ustawi wa jamii wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu, Wamdenge Kalingonji akizungumzia katika Mkutano wa hadhara wa kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika katika Kijiji Cha Dutwa.
Mikutano hiuo iliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Bariadi Mass Media chini ya ufadhili wa Fondation For Civil Society(FCS).
Amesema kuwa wapo watu wengi wanafanyiwa ukatili wa Kijinsia na jamii inafahamu lakini wanakaa kimya hawatoi taarifa kutokana na tamaduni mbalimbali.
Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Sapiwi wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu ulioandaliwa na Bariadi Mass Media kupinga ukatili wa kijinsia.
"Matukio ya ukatili wa Kijinsia ni mengi katika jamii ila wakati umefika sasa wa kusema matukio hayo sasa basi tutumie Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Mashirika kama hili la Bariadi Mass Media linalopingana na Ukatili huo Ili kutoa taarifa za ukatili ili na muathirika aweze kusaidiwa,"amesema.
Amesema pia yapo madawati ya jinsia katika vituo vya polisi, hivyo jamii ihakikishe inavitumia ipasavyo na kuripoti matukio yote ya ukatili.
Aidha, amesema jukumu la kuwatunza watoto ni la wote ili wasiishi mitaani, hivyo ukatili unatakiwa kukomeshwa.
Naye Mratibu wa Bariadi Mass Media,Frank Kasamwa amesema kuwa ni jambo lisilopingika kuwa ukatili wa kijinsia umekuwa na athari kubwa sana kwa waathirika na taifa kwa ujumla.
Mratibu wa Bariadi Mass Media,Frank Kasamwa akizungumza na wananchi wa Kijiji Cha Sapiwi wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu(hawapo pichani)juu ya athari za ukatili wa kijinsia
Amesema kuwa vitendo hivyo vya ukatili vinapoendelea kwa muda mrefu ndivyo athari zake zinavyokuwa nyingi na kusababisha athari nyingine kuwa za kudumu.
"Ni jambo la muhimu sana kwa mwathirika kujiondoa katika hali hii mapema Ili kujinusuru na madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia.
"Japo kuwa ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa umekuwa ukielekezwa kwa wanawake athari zake zimekuwa zikiligusa taifa kwa ujumla hivyo toeni taarifa hizo pindi mnapoona vitendo hivyo katika jamii,"amesema.
Pia ameongeza kuwa madhara ya ukatili huo ambao ni wa kimwili,kingono,kisaikolojia,kiimani na kiuchumi yanakumba makundi yote yaani mtu binafsi, familia,jamii na taifa kwa ujumla.
Shirika la Bariadi Mass Media limekuwa likijishughulisha na kokomesha ukatili wa kijinsia kwa jamii katika wilaya ya Bariadi.
Post a Comment