HEADER AD

HEADER AD

AWESOME EXPEDITION KUTINGA MARA KUHAMASISHA UTALII

>>> Mkutano wa Kimataifa, maonesho ya biashara kufanyika Musoma

>>>Waandishi wa Habari nchi mbalimbali kushiriki

Na Dinna Maningo, Mara 

KAMPUNI Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition yenye makao yake makuu mkoani Arusha nchini Tanzania inaandaa Kongamano la kuhamasisha Utalii lijulikanalo Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, litakalofanyika mjini Musoma mkoani Mara.

Mpango huo wa uhamasishaji wa Utalii utakwenda sambamba na mkutano wa Kimataifa, maonesho ya biashara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utakaofanyika Mei, 22-28,2023.

Lengo ni kuhamasisha utalii katika mkoa wa Mara ambapo Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali watapata fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao katika viwanja vya Mukendo mjini Musoma.

Akizungumza na DIMA Online mjini Tarime, Mratibu wa mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy amesema mpango huo umelenga kuhamasisha utalii na kwamba ni wa kwanza kuanzishwa Afrika ya Mashariki utakaoanzia mkoa wa Mara.

   Mratibu wa Mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy

"Kutakuwa na mkutano wa Kimataifa     (International Conference)  utakaofanyika ukumbi wa NHC Mukendo Plaz, tunategemea kuwa na wageni 350 utakafanyika kwa siku tatu, tarehe 23/05/2023 hadi 25/05/2023.

"Zitajadiliwa mada sita ambazo zitahusu Safari, Michezo na Burudani (Travelling for businesses, Sports and Leisure),Utalii (Ecotourism), Mitumbwi ya makasia (Canoeing), Kutembea kwa miguu (Trekking), Matamasha ya asili (Cultural Festivals) na Mchezo wa kuvua samaki (Sport Fishing).

"Baada ya nadharia kutafanyika vitendo kutokana na mada zilizotajwa ambavyo vitahamasisha utalii zaidi baada ya kumalizika kwa kongamano. Pia Mei, 26-28/2023 kutafanyika Bush Party Serengeti National Park kisha kutoka hifadhini na kurudi kufunga maonesho"amesema Buchebuche.

Buchebuche ameongeza kusema kuwa maonesho ya biashara (Business Expo) yatafanyika kwa siku nane ambapo Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao.

Ameongeza kuwa Waandishi wa habari wa mkoa wa Mara nchini Tanzania kwa kushirikiana na Waandishi wa Habari kutoka nchi 24 ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Ghana, Uturuki, USA, Canada, India na Israel kupitia vyombo vyao vya habari wataripoti habari kuhamasisha utalii yakiwemo maonesho ya bidhaa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Waandishi hao wa Habari wataripoti habari na kuandaa vipindi na makala na kuvirusha katika vyombo vyao vya habari katika nchi zao kwa lengo la kutangaza vivutio vya mkoa wa Mara ili kuwavutia watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii mkoani Mara sambamba na kuitembelea hifadhi ya Serengeti.

Buchebuche amewaomba wananchi wa Mara kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mukendo kuona maendeleo ya utalii na sanaa mbalimbali kwani kutakuwepo na bidhaa nyingi za kuuza na kuuza.

Ratiba



No comments