KIFICHO GHARAMA UJENZI WA JOSHO LILILOJENGWA CHINI YA KIWANGO NA IRASANILO GOLD MINE
Na Dinna Maningo, Butiama
KUMEKUWEPO na sintofahamu juu ya gharama halisi zilizotumika katika ujenzi wa Josho lililopo Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa wilaya ya Butiama mkoani Mara lililojengwa na Kikundi cha Wachimbaji wadogo wa Dhahabu Irasanilo Gold Mine.
Kwa mujibu wa wananchi wa Kijiji hicho wameiambia DIMA Online kuwa ujenzi wa Josho na choo vimegharimu jumla ya Tsh. Milioni 27 huku wengine wakisema ni Tsh.Milioni 28.
Viongozi wa mgodi huo nao wakitupiana mpira kueleza gharama halisi za ujenzi wa Josho hilo ambalo halijakamilika na limejengwa chini ya kiwango.
Mjumbe wa Halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Magunga Matias Maremi Washima amesema mifugo imekosa huduma kutokana na josho kushindwa kukamilika.
Josho lililojengwa na mgodi wa Irasanilo linalodaiwa kugharimu Tsh Milioni 27 ambalo ujenzi wake haujakamilika na limejengwa chini ya kiwango
"Tulikuwa na Josho letu la Kijiji walipokuja watu wa Stamico walizungusha uzio, josho likawa ndani ya uzio ambako ndio kuna huo mgodi, mgodi ukatakiwa kujenga Josho lingine tukawaonesha eneo lingine ndani ya Kijiji. Fedha zilichangwa na wachimbaji wa mgodi zaidi ya Tsh. Milioni 28 kama tulivyosikia.
Jumanne Francis ambaye ni Barozi Kitongoji cha Rwamakore amesema " Josho limejengwa na mgodi hatujawahi kuambiwa gharama halisi za ujenzi tunasikia tu wakisema kuwa limegharimu Tsh. Milioni 27 wengine wanasema Milioni 28.
"Hatujui gharama maana Kijiji bado hakijakabidhiwa josho ndiyo tungejua pesa halisi, halijapokelewa kwasababu mkaguzi alikuja akakuta siyo la kiwango kinachotakiwa akatoa maelekezo, yakafanyika marekebisho kama unavyoona lakini bado lilionekana lipo chini ya kiwango.
"Limejengwa tangu 2021 lipo tu kama pambo hatujui kinachoendelea limetelekezwa, tunaomba serikali na mgodi watukamilishie josho mifugo inaathiriwa na magonjwa" amesema Jumanne.
"Fedha za ujenzi wa josho alipewa Daniel Yuda ambaye alichaguliwa na mgodi kusimamia ujenzi wa Josho, Josho lilijengwa likamalizika cha hajabu muda mfupi maji yakawa yanavuja yanapita chini na choo kikabomoka ikaonekana vimejengwa chini ya kiwango na fedha zimeliwa mifugo inatembea km 3 kwenda kupata huduma Kijiji cha Mirwa "amesema Matias.
Daniel Mahemba Mwita amesema" Ofisi ya mgodi wakabomoa Josho letu wakaja kujenga hapa Kitongoji cha Rwamakore limejengwa kwa Tsh. Milioni 27, uongozi wa mgodi ulisema kwenye mkutano wa wananchi.
"Wamejenga josho lenyewe bovu, choo kimebomoka hata kabla ya kuanza kutumika, hatuambiwi shida ni nini na litakamilishwa lini mgodi umekaa kimya na serikali imekaa kimya" amesema Daniel.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rwamakore Maroba Warioba amesema" Mgodi ulituonesha nia kujenga lakini josho halijakamilika ukipiga simu hupati majibu, ukifuatilia hupati majibu.
"Mimi kama Mwenyekiti nimeshindwa cha kuwajibu wananchi wangu hii ni namna ya kurudisha nyuma maendeleo,tunaomba mgodi ujenge josho, huo sio msaada ni wajibu maana Kijiji kilikuwa na josho kikawapatia eneo lingine na kuahidi kujenga josho jipya wakajenga lakini halifanyi kazi limejengwa chini ya kiwango kwa hiyo sio msaada ni lazima wajenge na wakamilishe"Amesema Mwenyekiti huyo.
Diwani wa Kata ya Mirwa Willy Broun amesema Josho hilo limejengwa na mgodi wa Irasanilo na hawajawahi kukabidhi ili wawaambie mapato na matumizi ya ujenzi huo.
Afisa mifugo Kata ya Mirwa Washington Benasius alipoulizwa kuhusu ujenzi wa josho ambalo limejegwa chini ya kiwango na halitumiki licha ya gharama nyingi kutumika katika ujenzi amesema;
"Awali josho lilikuwa eneo kuliko na mgodi wa Irasanilo mgodi ulichukua eneo hilo ukakubaliana na Kijiji kuwajengea josho lingine. Kijiji kiliingia makubaliano na mgodi kikatoa eneo mgodi ukajenga Josho.
"Wakati maongezi hayo yanafanyika mimi nilikuwa afisa mifugo Kata ya Buhemba, nilichokisikia mgodi haukushirikisha wataalam wa idara husika kwa maana ya idara ya mifugo,walitafuta mkandarasi wao wakaanza ujenzi.
Ameongeza " Afisa mifugo aliyekuwepo Dornad Lamtei alinieleza kuwa alipofuatilia ujenzi wa Josho hilo hawakumpa ushirikiano wakasema wana mtaalam wao.
"Nilipohamishiwa hapa Mirwa nilienda kwenye hilo josho nilibaini mapungufu, kina kwenda chini ni kifupi hakiwezi kuruhusu mifugo mikubwa kutumbukia akiruka atafika kwenye sakafu chini ni rahisi kuvunjika.
Washington amesema upana wa Josho hilo ni mdogo hauruhusu wanyama wakubwa kuogeshwa hawawezi kuingia maana ni jembamba.
"Pia josho linatakiwa lijengwe kwa upana ambao mnyama akigeuka panakuwepo na sehemu ambayo mtu anaweza kusimama na kumgeuza myama pindi anapokuwa amegeuka kurudi alipotokea" Amesema.
Ameongeza kuwa eneo ambalo wanyama wanasimama baada ya kutoka kwenye josho sakafu yake sio imara hivyo kwa hali hiyo Josho hilo limejengwa chini ya kiwango.
"Kuhusu gharama zilizotumika mimi sijui ila nachofahamu baada ya hapo uongozi wa wilaya ulikutana na uongozi wa mgodi wakakubaliana lijegwe josho lingine jipya ambapo mgodi utatoa fedha halmashauri na halmashauri itasimamia ujezi, kikao hicho mimi sikuwepo" amesema Washington.
Aliyekuwa Meneja wa mgodi wa Irasanilo Gold Mine wakati wa ujenzi wa josho hilo Isaya Daudi alipotakiwa kueleza gharama za ujenzi wa josho aliomba aulizwe msimamizi wa mradi Daniel Yuda kwamba ndiye anayefahamu gharama za ujenzi.
DIMA Online imemtafuta msimamizi wa mradi wa josho ambaye pia ni mchimbaji katika mgodi wa Irasanilo Daniel Yuda Magogo kufahamu ni kiasi gani kilichogharimu josho lakini hakuwa tayari kutaja kiasi kilichogharimu ujenzi na hivyo kuomba aulizwe mhasibu wa Irasanilo.
"DC alimleta mtu wa mifugo akaja kusimamia ujenzi wa josho akachukua na fedha mgodini akaleta fundi akabomoa hilo jengo, halikuwa hivyo akachukua na fedha, akaleta fundi wakaja saiti matokeo yake ujenzi haukufanyika hadi matirio yakaharibika.
"Ofisi ya Mkurugenzi inafahamu muulize vizuri afisa mifugo wa Halmashauri aitwaye Mturi, jengo halikuwa hivyo walibomoa kuwa wanataka kurekebisha kwamba limejengwa kizamani,kuna vikao vilikaa na wakamteua Mturi kuja kusimamia, tukatoa vifaa na matirio vikaharibika fundi akaishia mitini"amesema Daniel.
Kuhusu kiasi alichodai chukua afisa mifugo wa halmashauri kutoka mgodini kwa ajili ya kurekebisha kasoro za ujenzi wa josho msimamizi huyo wa mradi hakutaja kiasi na badala yake akaomba aulizwe afisa mifugo na sababu za kutokamilika jengo.
"Kuhusu gharama zilizojenga josho ni kitu ambacho kinaandaliwa kwenye maandishi sina kumbukumbu, alafu hao waliokuambia ni Milioni 27 ni akina nani ?nenda kwa mhasibu wa mgodi ndiyo anajua ni shilingi ngapi na pesa aliyopewa Mturi atakwambia ni sh. ngapi"amesema.
Aliyekuwa mhasibu katika mgodi huo Edward Mohere amesema aliyekuwa msimamizi wa mradi Daniel Yuda ndiye anayefahamu gharama za ujenzi kuanzia hatua ya msingi hadi ukamilishaji hivyo aulizwe yeye.
"Mimi nakumbuka zilikuwa Tsh. Milioni 20 na kitu hazifiki Milioni 22 ,mara ya kwanza tulihidhinisha Milioni 19 na kitu mpaka Milioni 20, baadae wakasema limepasuka, halmashauri ilikuja kukagua wakati huo sikuwepo nilikuwa nimesafiri.
"Sijajua ni kiasi gani injinia wa Halmashauri alikuja akapendekeza na kuongezeka ila Daniel ndiyo alikuwa anachukua hela anasaini hizo hela, yeye ndiye amesimamia ujenzi wa josho kuanzia mwanzo hadi mwisho na alikuwa anasaini hizo fedha.
"Sasa akisema uniulize mimi anakwepa majukumu yake yeye ndiye anajua fedha alizotumia na yeye ndiye alikuwa analeta maombi kila kitu kipo kwenye faili la josho ofisini"amesema Edward.
Afisa Mifugo Halmashauri ya wilaya ya Butiama Edward Mturi alipoulizwa kiasi alichopewa kwa ajili ya ujenzi licha ya habari kudai kuwa mgodi ulimpatia Tsh. Milioni 3 kwa ajili ya kufanya marekebisho ya josho alikanusha kupewa kiasi hicho na kusema alipewa Tsh.300,000 kama fedha za mafuta kwa ajili ya usafiri katika shughuli hiyo ya ujenzi wa josho.
"Hawakutoa pesa walichokitoa ni pesa ya mafuta kwa ajili ya sisi kutoka halmashauri kwenda saiti kiasi cha Tsh. 300,000, kweli pesa hiyo inajenga josho! nilipewa kiasi hicho nafikiri na fundi alipewa 300,000, na mafundi hawakuwa na vifaa pesa hiyohiyo tuliwanunulia nyundo na sururu za kubomolea pale kwenye zizi ili waanze kazi." amesema Mturi.
"Yule fundi aliyekuwa saiti ni wa Bisumwa na hakuna fundi anayedai, wataalamu walipofika walikuta josho limejengwa chini ya kiwango tulijaribu kutaka kurekebisha lakini ilishindikana.
Afisa huyo ameongeza kusema "Afisa mifugo anaanzaje kwenda kuwaambia mgodi wajenge josho? Josho ni la kijiji wao ndio wawaulize.Kuhusu gharama za ujenzi hata mimi sijui nasikia tu kuwa limegharimu Tsh. Milioni 27.
"Ukiangalia jengo na gharama zilizotumika haziendani sisi tunaangalia matirio, kwa mfano ukiangalia yale mazizi ng'ombe akiingia anabomoa hata kwa kwato,tulipochimbua chini hata mawe hayapo.
"Pale ni kujenga jipya siyo kuripea inabidi wajenge sehemu nyingine, tuliwambia kwa mdomo kama tulivyoagizwa kwa mdomo kwenda kukagua josho.
Anazidi kueleza " Sisi tulitumwa na Dc kama wataalam tukafika pale na mafundi kwa ajili ya kwenda kupima kuona kama linaweza kurekebishika kwasababu lipo nje ya mchoro.
"Baada ya kuona halirekebishiki tuliwaambia wajenge jipya tukaishia hapo sisi tuliwaambia kwa jinsi michoro ilivyo ilitakiwa kuchimbwa kina kirefu, sasa huwezi bomoa hapo walipoweka zege uchimbe liingie ndani lakini pia tulijaribu kubomoa yale mazizi tukawaambia haliwezi kurekebishika "Amesema.
Amesema hawakurekebisha bali walijaribu kurekebisha lakini haikuwezekana hivyo mpaka wajenge josho jipya na kwamba tayari mgodi umepewa mchoro.
"Wajenge upya kwakuwa awali walijenga bila kushirikisha wataalam, hivyo wao wanachotakiwa kufanya wajenge josho jipya na walisema watagharamia vifaa vyote.
Ameongeza kuwa Serikali ya Kijiji ndiyo inapaswa kuhimiza mgodi kujenga josho na siyo halmashauri na kwamba afisa mifugo hawezi kwenda mgodini kuhimiza kujengwa kwa josho.
"Serikali ya Kijiji isikwepe majukumu yake Mtendaji wa Kijiji ndiye anatakiwa kuandika barua kuwa mradi uliojengwa ulikuwa chini ya kiwango na wanatakiwa kujenga josho jingine jipya nakala atume kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri.
"Wakishapeleka barua mgodini wao wanatakiwa wajibu, sasa yale majibu yao ndio tunaanzia hapo, Mkurugenzi hana la kusema yeye anasubiri Kijiji, pale Serikali ya Kijiji ni shida hawajui majukumu yao" Amesema Mturi.
Amesema wao kama halmashauri hawajakabidhiwa mradi huo na kwamba mgodi ulitakiwa kukabidhi Kijiji mradi na sio kukabidhiwa halmashauri na kwamba mgodi ndiyo unajua kiasi cha fedha kilichotumika kwenye ujenzi kwakuwa yeye hana uhakika na gharama zilizotumika katika ujenzi huo.
Post a Comment