HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI ILIVYOUA SACCOS YA UMAWANYA KWA KUSHINDWA KULIPA MADENI

Na Dinna Maningo, Butiama 

CHAMA cha Ushirika cha kuweka na kukopa cha Walimu (UMAWANYA) kimekufa kutokana na kushindwa kujiendesha baada ya Halmashauri ya wilaya ya Butiama na Halmashauri ya wilaya ya Musoma kushindwa kulipa madeni zaidi ya Tsh. Milioni 20, fedha ambazo ni makato ya mishahara ya walimu 61 wakiwemo wastaafu 29.

Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kila mwezi ilikuwa ikiwakata mishahara wanachama walimu 57 kwa ajili ya kuwawekea fedha zao kwenye SACCOS hiyo kama Akiba yao lakini mwaka 2018-2020 ilishindwa kuweka licha ya kuendelea kuwakata mishahara jumla ya Tsh. 16,971,000.

    Halmashauri ya Wilaya ya Butiama

Katika Halmashauri ya wilaya ya Musoma Walimu wanne wanadai fedha jumla ya Tsh. 3,195,768 fedha ambazo ni madeni ya mwezi Agosti, 2011- Desemba, 2019, deni lote katika halmashauri hizo likiwa na jumla ya Tsh. 20,116,768 ambazo hadi sasa walimu hao hawajalipwa.

Madeni hayo ya walimu ni makato ya akiba na marejesho ya mikopo yaliyokuwa yakikatwa kupitia Hazina ya Watumishi na fedha kuwekwa katika akaunti za Halmashauri hizo kwa lengo la kuwawekea akiba kwenye SACCOS lakini halmashauri hazikufanya hivyo. 

Walimu hao ambao wengine kwa sasa ni wastafu wamekuwa wakichapa mwendo hadi ofisi mbalimbali za Serikali kufuatilia hatma ya malipo yao lakini imekuwa ndoto kwao kitendo wanachodai huwenda Halmshauri hizo zimekula fedha zao na kuwadhulumu haki yao halali itokanayo na makato ya mishahara yao.

Mwandishi wa DIMA Online amefika katika Kijiji cha Kyonkoma Kata ya Nyamimange Tarafa ya Kiagata wilaya ya Butiama kulikokuwa Makao makuu ya SACCOS ya UMAWANYA.

Lengo likiwa kuzungumza na viogozi wa Chama hicho kufahamu sababu ya SACCOS hiyo kushindwa kujiendesha na kuhusu madai yao yaliyodumu kwa miaka kadhaa bila kutatuliwa.

Wanachama hao ambao baadhi yao wamestafu utumishi wanaeleza jinsi walivyofuatilia madai yao bila mafanikio jambo ambalo limesababisha wanachama kujiondoa kwenye SACCOS kutokana na kutolipwa fedha zao walizokuwa wakikatwa na Serikali kupitia Halmashauri hizo.

Mwenyekiti mwanzilishi wa SACCOS ya UMAWANYA Mwl. Mstaafu Benedicto Nsiko ambaye pia alikuwa Mratibu Elimu Kata ya Nyamimange anasema Chama hicho kilisajiliwa na Serikali mwaka 2001 na kupewa Hati Na. MAR, 474 iliyotolewa Juni, 2004 iliyoandikishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.15 ya mwaka 1991 kifungu cha 30.

Mwenyekiti mwanzilishi wa SACCOS ya UMAWANYA Mwl. Mstaafu Benedicto Nsiko

"Serikali ilihimiza uanzishaji wa Vyama vya Ushirika vya kuweka na kukopa, Kata nyingi zilishindwa kuanzisha ila Kata yetu ya Nyamimange ikafaulu wakati huo Wilaya ikiwa ya Musoma kabla ya kuanzishwa wilaya ya Butiama, baada ya kuanzishwa wilaya mpya SACCOS ikahesabika Wilaya ya Butiama.

"Wanachama wetu wengine wamestaafu utumishi wengine bado ni watumishi katika Halmshauri ya Butiama, Musoma na Manispaa ya Musoma, tuliweka amana ili kujisaidia, tulijiwekea kiasi cha kuanzia Tsh. 20,000 kulingana na akiba.

Mwenyekiti huyo anaongeza "Kila mwezi watumishi ambao ni wanachama walikuwa wakikatwa mshahara kimo cha chini 20,000, fedha zilikuwa zinatoka hazina zinakatwa kupelekwa kwenye mifuko alafu unapata fedha zako.

"Fedha za makato yetu ya mshahara zilipitia Halmashauri kisha wao wanatupatia hundi tunapeleka benk wanatuwekea fedha kwenye akaunti ya Chama, baadae halmashauri hizo zikawa zinaingiza fedha moja kwa moja kwenye akaunti ya Chama hapo ndipo shida ilipoanzia.

"Wakawa wanaweka pesa kidogo kidogo wakalimbikiza madeni ambayo ni fedha za akiba ya wanachama wetu kwa ajili ya kuwawezesha kuweka na kukopa fedha kupitia SACCOS" anasema .

Benedicto anasema kuwa mwanzoni halmashauri zilikuwa zinalipa vizuri makato hayo katika SACCOS ya UMAWANYA, lakini ilipofika mwaka 2011-2019 Halmashauri ya Musoma ilisuasua kutoa fedha huku ikiendelea kukata fedha, mwaka 2018-2020  Halmashauri ya Butiama ilistisha kutoa fedha hizo licha ya kuendelea kukata mishahara.

"Hazina ndiyo inaandaa mshahara na mgawanyo wa makato kulingana na mwajiri alivyochanganua mshahara kisha hazina inalipa kupitia Halmashauri unapokea mshahara wako na makato yako yanapelekwa kwenye mfuko husika ambapo wanachama wetu mfuko wao ulikuwa ni SACCOS ya UMAWANYA .

Anasema wamekuwa wakifuatilia madai yao bila mafanikio " Upande wa Halmashauri ya Manispaa Musoma wao tulikuwa tunawadai 180,000 walitulipa hawana deni ila halmashauri ya Butiama na Musoma imeshindikana kulipa.

"Tumeshaandika barua nyingi sana tumegharamika nauli za usafiri kufuatilia kwenye halmashauri hizo. Malalamiko tulishayafikisha hadi kwa wakuu wa Wilaya hizo, Wenyeviti wa halmashauri, mbunge, Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara, Mrajisi Msaidizi Ushirika Mara na Ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Mara lakini ufumbuzi wa hatima yetu ya malipo haujapatikana.

"Ma- DC wa hizo wilaya waliwaita Wakurugenzi wa halmashauri hizo kuhusu madai yetu wakatuahidi kutulipa lakini ilishindikana kutulipa, ukirudi kwa DC anakwambia alishatoa maelekezo ni kama walipuuza maagizo ya DC" anasema.

Anasema kuwa kitendo cha kutolipwa fedha hizo za makato imesababisha SACCOS isiendelee baada ya kushindwa kujiendesha kutokana na kukosa fedha zilizokuwa zikipokelewa kama makato ya kila mwezi zilizosaidia kujiendesha.

" Baada ya madeni hayo kuyafuatilia bila mafanikio, Mwezi, Juni, 2020 tulisimamisha makato baada ya mwajiri kutoleta fedha kwenye Chama, madeni yalikuwa yanalimbikizwa tukaona tusimamishe kwanza, hata waliokuwa wamekopa wameshindwa kurejesha fedha.

Mhasibu wa SACCOS hiyo ambaye kwa sasa amestaafu kazi Mwl. Joseph Bunyinge aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Nyamihuru anasema wanachama 61wanadai fedha zao za makato ya mshahara.

    Mhasibu wa SACCOS ya UMAWANYA ambaye kwa sasa amestaafu kazi Mwl. Joseph Bunyinge 

Anasema watumishi 57 ni wa halmashauri ya wilaya ya Butiama na wanne ni halmashauri ya wilaya ya Musoma ambapo kati yao 29 wamestafu utumishi.

"Tunaidai Halmashauri ya wilaya ya Butiama kiasi cha Tsh. 16,971,000 ambazo ni fedha za makato ya akiba na marejesho ya mikopo yaliyokatwa kwa watumishi ambao ni wanachama na kwa Halmashauri ya wilaya ya Musoma ni Tsh. 3,195,768 madai ya walimu wanne waliokatwa mishahara yao.

" Watumishi wengine wamestafu wakiwa hawajapewa stahiki zao, halmashauri zimesababisha chombo hiki kulegalega, tumefuatilia sana bila mafanikio, tumetuma barua nyingi za kukumbushia madai zikiambatana na orodha ya wanaodai, cheki zao, miezi daiwa na kiasi daiwa lakini bado hatujalipwa" anasema Joseph.

Faida walizopata kupitia Chama hicho

Mhasibu huyo Joseph Bunyinge anasema Chama hicho cha Umawanya kiliwasaidia kwani waliweka akiba na kukopeshana fedha zilizosaidia kusomesha watoto na kuwezesha mahitaji ya familia.

"Ulikuwa ukifiwa Chama kinagharamia mazishi, ukiwa huna pesa unakopa unamlipia mtoto ada ya shule, mzunguko wa fedha haupo maana fedha za wanachama ziliwezesha mzunguko wa fedha unakopa unaenda kununua kitu, SACCOS ilitupunguzia changamoto" anasema Joseph.

 Mwal. Mstaafu Joseph Ododa aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Nyamihuru anasema SACCOS ilimsaidia kusomesha watoto wake ambao wamefanikiwa kupata ajira na imemwezesha kujenga Nyumba kabla ya kustaafu kazi.

Mwal. Mstaafu Joseph Ododa

"Kupitia SACCOS ya UMAWANYA nimesomesha watoto hadi wameajiriwa, imeniwezesha kujiendeleza kielimu nikiwa kazini, kufa kwa SACCOS hii imeniathiri sana maana mambo yangu hayaendi, nikienda kukopa fedha kwa watu binafsi wengine wananibeza.

"Wananiambia kwamba muda wote nilipokuwa kazini kwanini nilikuwa situnzi fedha benk, imesababisha watoto wangu hawasomi shule nzuri maana ingekuwa hai ningekopa fedha wanangu wangesoma shule nzuri" anasema Joseph.

Gebore Mtegetu ni mwalimu mstaafu aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Kiagata anasema kupitia SACCOS amesomesha watoto wamepata ajira, matibabu na kujenga nyumba kabla ya kustaafu kazi.

     Gebore Mtegetu ni mwalimu mstaafu

"Pia tulikuwa na mfuko wa maafa mtu alipofiwa kabla mwajiri hajakusaidia tuliweza kusaidiana wenyewe kupitia fedha zetu za kuweka na kukopa, sasa hivi tunapopata msiba tunadhalalika hakuna fedha" anasema.

Gebore anaongeza " Kupata fedha kwa ajili ya mahitaji ya familia haipatikani kwa urahisi, imenifanya kwenda kujidhalilisha kwa wakopeshaji binafsi ambao wana riba kubwa, riba yetu ilikuwa asilimia kumi lakini hawa watu binafsi riba zao ni asilimia 30 hadi 50.

"Kupitia SACCOS tulisaidiana kwenye misiba kuna mwalimu mwenzetu alifiwa akakosa gharama ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kuzika kwao wilaya ya Ukerewe, ikabidi aombe eneo akazika hukuhuku Butiama, SACCOS ingekuwepo angegharamiwa kupitia mfuko wa maafa lakini kimekufa baada ya Halmashauri kushindwa kulipa madeni"anasema Gebore.

Mwalimu huyo mtaafu anaongeza kuwa endapo halmashauri itawapa fedha zao watakutana na wenzao kujadiliana ili kuifufua SACCOS yao pamoja na kulipa madeni ya wanachama ambao walitunza akiba.

"Kutokana na usumbufu huo tulipofuatilia hazina tukashauriwa fedha zetu zisipitie tena halmashauri tukaambiwa kwamba hazina itakuwa inaweka moja kwa moja kwenye SACCOS, lakini ndiyo hivyo Chama kilishindwa kujiendesha kutokana na madeni hayo kuyafuatilia bila mafanikio.

"Tulimwomba mwajiri akate fedha za mishahara ya wanachama na kuziweka kwenye akaunti ya Chama kama njia ya kuturahisishia maana awali ilikuwa inakulazimu uende kwa mkurugenzi ukae karibu na dirisha la kuchukulia mshahara mtu akichukua mshahara unambana anakupa fedha.

"Njia hiyo tuliona siyo nzuri na siyo rafiki kwenda kumsubiria mtu dirishani achukue mshahara akupe, pia njia hiyo haikuwa salama kwakuwa ilikuwa ni rahisi hata kuvamiwa kwakuwa tarehe za kuchukua mshahara zilijulikana ilikuwa ni tarehe 1-5.

"Kwahiyo tulipofuata fedha watu walijua, usalama wetu ukawa matatani ndiyo tukalazimika kuchukua fedha za Chama kupitia kwa waajiri ambao ni wakurugenzi wa halmashauri hizo"anasema Gebore.

Anaongeza " Tumefuatilia sana madai yetu bila mafanikio barua tulipeleka ofisi mbalimbali na tumekuwa tukikumbushia madeni yetu mara kadhaa bila mafanikio, barua tulipeleka pia hadi kwa mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Mara kuhusu madai.

"Tumepeleka hadi ofisi ya CCM mkoa, kwa mbunge Sagini, kwa wakurugenzi , ma- DC wa wilaya hizo hadi ofisi ya Ras mkoani lakini bado suala letu halijapatiwa ufumbuzi, tunaomba Serikali itutendee haki zile ni pesa zetu za mishahara yetu kwanini hatupewi na ni stahiki zetu, wengine sasa ni wastaafu tunaomba Serikali itutendee haki" anasema.

Mwalimu mstaafu Daud Nyahurya aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Butiama anasema baada ya kuvunjika kwa Chama hicho cha walimu ushirikiano kati ya walimu umeisha na kusababisha lawama kwa wanachama kwa viongozi wao.


  Mwalimu mstaafu Daud Nyahurya

"Ushirikiano kati ya walimu umeisha mpaka leo hii wanachama wanaamini kuwa viongozi ndiyo tumekula fedha zao na kupelekea wanachama wengi kujitoa, kikundi kikafa kutokana madai ya fedha hizo" anasema Daud.

Mwal. Mstaafu Thomas Magabe aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Kiagata anasema wakati SACCOS hizo zimeanzishwa viongozi mbalimbali wa kiserikali walihamasisha uanzishwaji wa Vyama vya walimu vya kuweka na kukopa fedha lengo kujijenga kiuchumi.

     Mwal. Mstaafu Thomas Magabe

Pia kuinuana kimaisha na kusaidiana katika matatizo lakini mwisho wa siku imekuwa ni maumivu kwao baada ya halmashauri kuwadhulumu fedha zao baada ya kuzifuatilia bila mafanikio badala yake huishia kuahidiwa ahadi zisizofikia ukomo.

Watumishi hao wakiwemo wastaafu wanaiomba Serikali kusikia kilio chao cha muda mrefu ili waweze kupata fedha zao ambazo ni makato ya mishahara yao iliyokuwa ikikatwa ofisi ya mkurugenzi na kwamba ni haki yao kulipwa.

Wanasema kwamba UMAWANYA ni SACCOS iliyoundwa na Watumishi (Walimu) wa shule za msingi na Sekondari kwa usajili wa MAR/474 ya mwaka 2001 kwa makusudi ya kujiwekea akiba zao ili kukopeshana.

Ofisi ya Ded yagoma kuzungumza

Mwandishi wa habari wa DIMA Online akafunga safari hadi ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama kufahamu sababu ya wanachama hao kutolipwa stahiki zao.

Hata hivyo Mwandishi wa Habari hii alipofika ofisini alimkuta Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Revocatus Lutunda ambaye hakutoa ushirikiano na kudai kuwa msemaji ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Patricia Kabaka ambaye alisema yupo safari kikazi.

Mwandishi alimweleza Kaimu huyo malalamiko ya wanachama hao didhi yake kwamba wanapompigia simu kaimu huyo kuhusu madai yao amekuwa akiwajibu vibaya na kuwaambia kuwa wamekuwa kero.

Pia amekuwa akiwapiga tarehe na wanapofika hawasaidii zaidi ya kuwapiga tarehe bila kujali gharama za nauli wanazozitumia kufuatilia madeni yao.

          Revocatus Lutunda

Kaimu huyo Revocatus badala ya kutoa ufafanuzi wa madai ya watumishi hao na tuhuma zinazoelekezwa kwake alikataa kujibu na kudai kwamba mwandishi huyo amekuwa akiiandika vibaya halmashauri hiyo. 

"Nimeona habari zako nyingi kwenye mitandao kwanza wewe utakuwa unanirekodi lete simu yako niione kwanza, kama hutaki nenda utakuja siku nyingine mkurugenzi hayupo " anasema Revocatus.

Mwandishi huyo wa habari hakumpatia simu na hivyo aliondoka baada ya kaimu huyo kutoa sharti ya kupekua simu ndipo azungumze.

Hivi Karibuni DIMA Online imekuwa ikiripoti habari mbalimbali katika Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa zikiwemo za miradi iliyojengwa chini ya kiwango isiyoendana na fedha halisi zilizotolewa.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Zahanati, Choo, changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa na malalamiko ya wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha za vyanzo vya mapato katika Kijiji hicho.

Mwandishi wa Habari akawasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Patricia Kabaka kwa njia ya simu kufahamu sababu ya watumishi hao waliofika ofisini kwake kumweleza madai yao na kuwatuma kwenda kwa  kaimu huyo Revocatus ili awasikilize lakini wamekuwa wakipigwa tarehe bila kutatua madai yao.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Patricia Kabaka

Mkurugenzi huyo alisema yupo safarini na kwamba hawezi kuzungumza kwa simu wala kujibu kwa ujumbe wa maneno (SMS) na kuahidi kuzungumza atakaporudi ofisini lakini hadi sasa hakuweza kutoa ushirikiano wowote licha ya kumtumia maswali kupitia ujumbe wa maneno.

Watumishi hao madai yao yanaendelea kupigwa chenga licha ya barua zao kupitishwa na afisa ushirika wa wilaya ya Butiama ili kufanyiwa malipo ikiwemo barua ya Septemba, 07, 2018 iliyosainiwa na kugongwa mhuri ikisisitiza walipwe madai yao ya muda mrefu.

Pia Octoba, 04,2019 alipitisha barua ya madai ya wanachama hao na kusisitiza walipwe huku alieleza kuwa athari za kutowalipa ni pamoja na kuvunjika kwa SACCOS hiyo lakini bado hawajalipwa.

Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Musoma April,04,2013 ilikiri kulipa kwa awamu deni la watumishi wa SACCOS ya UMAWANYA.


Hata hivyo halmashauri hiyo haikuweza kukamilisha deni lote licha ya kuendelea kukata fedha zao kila mwezi na deni kufikia Tsh. 3,195,768 kwa kipindi cha mwaka 2011- 2019.

Je Mrajisi Msaidizi mkoa wa Mara na Mufilisi wanasema nini kuhusiana na madai ya Chama hicho ? 

Endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza

No comments