HEADER AD

HEADER AD

ZAKAYO WANGWE AMUOMBA RAIS SAMIA KUWAHAMISHA WANANCHI WALIOPO HIFADHINI


Na Dinna Maningo, Tarime 

MKAZI wa Tarime Zakayo Chacha Wangwe kijana wa Chacha Zakayo Wangwe aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahamisha wananchi wanaodaiwa kuishi ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Zakayo amemuomba Rais Samia kufanya hivyo kama alivyowahamisha wananchi wa Ngorongoro kwenda kuishi katika Kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoani Tanga ili kupisha maeneo kwaajili ya uhifadhi.

    Mkazi wa Tarime Zakayo Chacha Wangwe kijana wa Chacha Wangwe

Ameyasema hayo kufuatia kuwepo mgogoro wa mpaka baina ya wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Serengeti kikiwemo Kijiji cha Nyandage na Kegonga wanaodai kuporwa ardhi na hifadhi ya Serengeti huku hifadhi ikidai kuwa wananchi ndio wavamizi.

Zakayo akizungumza na Waandishi wa habari amemuomba Rais Samia kuwaonea huruma wananchi hao wanaodaiwa kuwa hifadhini kwakuwa wameishi kwenye maeneo hayo kwa miaka mingi na wengi wao maisha yao ni duni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan

Amesema ni vyema wakalipwa fidia ili waende kutafuta makazi ama Rais Samia awatafutie maeneo mengine kisha atangaze kuwahamisha kama alivyofanya kwa wananchi wa Ngorongoro.

Zakayo amesema kwamba mpaka wa GN Na. 235 wa mwaka 1968 ambao ndiyo unaotumika, GN hiyo ni ya miaka mingi iliyopita kwani kwa wakati huo wananchi walikuwa wachache ambao kadri miaka ilivyokwenda walizidi kuzaliana na kuongezeka hali ambayo imesababisha kupungua kwa maeneo.

"Namuomba Rais wangu Dkt. Samia Suluhu atangaze kuwahamisha wananchi wanaoishi eneo la hifadhi awatafutie maeneo mengine wakaishi kama alivyofanya kwa wananchi wa Ngorongoro waliohamishwa na Serikali na kupelekwa katika Kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni.

"Ardhi ya wananchi wanaopakana na hifadhi ni finyu, huo mpaka uliwekwa tangu 1968 wakati huo watu walikuwa ni wachache saizi wameongezeka na spidi ya kuzaliana kwa wakurya ni kubwa na wanaoa wake wengi.

"RC, Mwenyekiti wa CCM mkoa kwasababu ardhi ni finyu na hawawezi kuongezwa eneo basi Rais Samia atangazie wananchi walio tayari kuhamishwa wahamishwe kwenda maeneo mengine kama walivyofanyiwa wa Ngorongoro" amesema Zakayo.

Amesema wananchi wana madai ya msingi hivyo wasikilizwe na mawazo yao yafanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na kuwatatulia changamoto ya maji ili wapate maji safi na salama.

"Wananchi wanasema kwamba kuna visima walivitumia kuchota maji na kunywesha mifugo, baada ya zoezi la uwekwaji bikoni lililofanyika siku chache zilizopita vile visima vimeingia hifadhini, tunaomba wachimbiwe visima na mabwawa ili mifugo yao ipate maji na wananchi wapate maji, madai ya wananchi ni ya msingi yasikilizwe na yafanyiwe kazi" amesema Zakayo.

Pia ameiomba Hifadhi ya Serengeti kutoa ajira kwa vijana wanaopaka na hifadhi kama njia ya kujenga mahusiano mazuri na wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi.

Wakati huohuo, Zakayo Wangwe amewatupia lawama Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara na Diwani wa Kata ya Nyanungu Tiboche Richad kwa kuwagomesha wananchi kutoshiriki mkutano wa mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee aliyefika katika kata hiyo kuzungumza na wananchi kuhusu uzinduzi wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka ya hifadhi (Bikoni).

"Mbunge kuwazuia wananchi kushiriki mkutano ni kosa, kuwazuia wananchi kuisikiliza Serikali yao ni kosa, alitakiwa ashughulikiwe amefanya uchochezi amegomesha wananchi anatishia kufanya vurugu. Vyombo vya ulinzi na usalama vimuite Waitara na Tiboche viwahoji na viwape onyo.

"Wananchi wana sheria zao ndogo ndogo kuwa usipohudhulia mkutano utachukuliwa hatua, wewe unawazuia sasa kero zao zitatatuliwaje wakati umewazuia kutoshiriki mkutano wa viongozi wao wa Serikali !.

"Waitara alipokuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wananchi wanaoishi kandokando na barabara nyumba zao zilibomolewa ikiwemo ya babu yangu iliyojengwa 1948 tukamwambia mbona mnatuambia tubomoe bila kulipwa fidia wakati nyumba zimejengwa zamani akasema tulivamia barabara tutake tusitake nyumba zitabomolewa na kweli nyumba zikabomolewa" amesema.

Zakayo ameongeza "Kwanini kwa sasa asiwaelimishe na hao wananchi kuwa wapo hifadhini wabomoe nyumba wahame kutoka ndani ya hifadhi.  

"Anawashitaki vijana kwa wazee wa mila waliohusika kwenye uwekaji wa bikoni, vijana waliomba vibarua ili wajipatie fedha unaenda kuwashitaki kwa wazee wa mila washughulikiwe na kushughulikiwa ni kuwaadhibu kimila, niwaombe wazee wa mila tunawapenda sana tunaomba msitumike vibaya kisiasa.

Ameongeza " SENAPA walishafanya vikao isipokuwa zoezi lile la kufanya nao mkutano na wananchi lilisimama baada ya Diwani kugomesha kwamba wanataka majadiliano mapya, anatishia kujiuzulu kwani yeye ndiye atakuwa wa kwanza kujiuzulu hata Lowasa alijiuzulu lakini nchi bado ilisonga.

"Serikali ndiyo wanajua GN wananchi wao wanasema mwaka 2013 wataalam wa ardhi walifika wakawaonesha mipaka ambayo ni tofauti walifanya makosa kwenye utambuzi wa mipaka ndiyo maana Serikali imesahihisha makosa hayo na kuweka hizo bikoni" amesema Zakayo.

Zakayo amesema ametoa maoni kama mwananchi na mzaliwa wa Tarime pia anatekeleza haki yake ya Kikatiba ibara ya 18 haki ya uhuru wa mawazo.

Rejea

>>>Hivi Karibuni mwishoni mwa mwezi Machi, 2023, Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee akiwa Kata ya Nyanungu akiwa ameongozana na viongozi wa wilaya na mkoa na wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alilalamika wananchi, Diwani na Mbunge kutohudhulia mkutano wake kwa ajili ya uzinduzi wa uwekaji alama za mipaka ya hifadhi.

      Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee

RC Mzee alisema kuwa Serikali kupitia timu ya Mawaziri nane wa kisekta walitoa mapendekezo yao kwa serikali likiwemo la uwekaji wa alama za mipaka ya hifadhi na kwamba yeye ni msimamizi kuhakikisha alama zinawekwa.

Alisema kuwa Serikali imewaachia wananchi mita 500 lakini baadhi ya viongozi akiwemo Diwani na Mbunge wamekuwa kikwazo cha kuwachonganisha wananchi na Serikali.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi hao kuheshimu maamuzi ya Serikali kwakuwa inatekeleza maagizo ya Chama cha Mapinduzi na kwamba wananchi waliopo ndani ya hifadhi taratibu zitafuatwa, wale wanaostahili kufidiwa watafidiwa na wasiostahili wabomoe nyumba zao na kuondoa ndani ya hifadhi.

Mbunge Waitara akiwa kwenye mkutano katika Kata hiyo ya Nyanungu baada ya kufanyika mkutano wa RC Mzee alisema hatambui alama mpya zilizowekwa kwa madai kuwa siyo zile zinatostahili kama ilivyo kwenye GN ya mwaka 1968.

       Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara

Waitara alitolea mfano bikoni mpya zilizowekwa hivi karibuni namba 45,46, 47,48 katika Kijiji cha Kegonga na Nyandage kuwa ni batiri hazipo kwenye GN ya 1968.

Aliongeza kuwa kilichotakiwa ni kufufua na kuhuisha bikoni ikiwemo namba 18, 273 na 271 na siyo kuweka bikoni mpya na kwamba watu wanaostahili kulipwa fidia siyo 40 ni zaidi.

Waitara alisema kuwa Mkuu wa mkoa hatakiwi kutumia nguvu na hana mamlaka ya kuweka bikoni bali wananchi na TANAPA walipaswa kukaa pamoja wakubaliane uwekaji wa mipaka. 

Waitara alisema viongozi 
lazima wajue mbivu na mbichi kwamba hawana muda wa kubembelezana, watatafutana koo yao ya Wairege waliopo nje ya Tarime kufanya mkutano wa pamoja kujua hatma ya mgogoro huo.

Waitara aliongeza kuwa wao sio waoga na kwamba Wenyeviti wa vijiji vinavyopakana na hifadhi watakapokwenda kinyemera kukutana na uongozi wa Hifadhi kabla ya kuzungumza kupitia mkutano wa wananchi watawahesabu kuwa ni wasaliti.

Diwani Tiboche katika mkutano huo wa Mbunge alisema kuwa zoezi la uwekaji mipaka halikuwa shirikishi kwani SENAPA haijawahi kufanya mkutano na wananchi kuzungumzia mgogoro wa mipaka na kwamba hata vikao vya ndani vilivyowahi kuketi havikuwa na hitimisho kutokana kutokuwepo maafikiano.

        Diwani wa Kata ya Nyanungu Tiboche Richad
 

No comments