KWANINI KAMPUNI YA AWESOME EXPEDITION KUHAMASISHA UTALII MARA ?
Na Dinna Maningo, Mara
MRATIBU wa Mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition amesema wameamua kuhamasisha Utalii katika mkoa wa Mara kwakuwa wanafuata nyayo za Royal Tour iliyoanzinshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzana DIMA Online Mratibu huyo amesema kuwa suala la kuhamasisha utalii ni la kila mwananchi zikiwemo sekta binafsi hivyo kila mmoja kwa nafasi yake anawajibu wa kuitangaza Tanzania kupitia vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
Mratibu wa Mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition.
"Nia yetu tunataka kuhamasisha watu wajue Utalii ni nini na faida zake, lakini pia tunafuata nyayo za Royal Tour iliyoanzishwa na Rais wetu, sio jambo la kumwachia yeye peke yake, sekta binafsi zinauwezo wa kufanya jambo hilo pia" amesema Buchebuche.
Je kwanini Kampuni hiyo yenye makao yake makuu mkoani Arusha imeamua kufanya uhamasishaji wa Utalii katika mkoa wa Mara? Mratibu Mraidizi wa Kampuni hiyo Mbinu Kipembe amesema;
Mratibu Msaidizi wa Mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Mbinu Kipembe kutoka Kampuni ya Utalii ya Awesome Expedition.
"Mkoa wa Mara ndio kina cha utalii na waanzilishi wa utalii walitokea mkoa wa Mara akiwemo Mwl. Julias Kambarage Nyerere. Lakini mkoa wa Mara unavyo vivutio vingi vya utalii na tunaona ni muda mzuri wa kuvitangaza vifahamike kimataifa.
"Na ili vitangazwe Kimataifa tumeamua kualika Waandishi wa Habari kutoka nchi mbalimbali zipatazo 24 ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Ghana, Uturuki, USA, Canada, India na Israel, kuripoti habari kuhamasisha utalii yakiwemo maonesho ya bidhaa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ameongeza " Waandishi hao wa Habari wataripoti habari na kuandaa vipindi na makala na kuvirusha katika vyombo vyao vya habari katika nchi zao kwa lengo la kutangaza vivutio vya mkoa wa Mara ili kuwavutia watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii mkoani Mara sambamba na kuitembelea hifadhi ya Serengeti" amesema Kipembe.
Mwandishi wa Habari hii alimuuliza Mratibu Buchebuche kufahamu kwanini hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ndio kubwa katika hifadhi zilizopo nchini lakini wananchi walio wengi mkoani Mara hawatembelei hifadhi hiyo ili kujionea vivutio, naye amesema.
"Watu wengi hawana mwamko wa kutalii ukilinganisha na matumizi yao binafsi, pia baadhi yao hawajapata elimu ya umuhimu wa Utalii na hawajui faida za kutembelea vivutio vya utalii.
"Hivyo kupitia jambo kama hili tunaloliandaa litaleta mafanikio ya watu kuhamasika kwenda kutemebelea hifadhi yetu ya Serengeti na kupitia habari zitakazoripotiwa na Waandishi wa Habari wa hapa nchini na wa kutoka nchi mbalimbali zitachochea na kuwahamasisha kutembelea hifadhi kwakuwa kupitia habari hizo wataelimika"amesema Buchebuche.
Je nini wananchi wa Mara na wageni wakitarajie kupitia uhamasishaji wa Utalii unaotarajiwa kufanyika Mei, 22-28,2023 mjini Musoma? na ni mambo gani wanatarajia kuwaeleza wageni katika mkutano wa Kimataifa utakaofanyika mjini Musoma?.
Buchebuche ameeleza "Kongamano hili litakuwa na mada sita ambazo zitajadiliwa kwa muda wa siku tatu.Travelling for businesses, Sports and Leisure (Safari), Ecotourism (Utalii) Canoeing (Mitumbwi ya makasia),Trekking (Kutembea kwa miguu).
"Kutakuwa na Cultural Festivals (Matamasha ya asili), Sport Fishing (Mchezo wa kuvua samaki). Baada ya nadharia kutafanyika vitendo kutokana na mada zilizotajwa kwani itahamasisha utalii zaidi baada ya kumalizika kwa kongamano na tutafanya Utalii kutembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mratibu huyo amesema kuwa mpango huo wa uhamasishaji wa Utalii mkoani Mara utakwenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa,maonesho ya biashara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na utawawezesha Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali kuonesha na kuuza bidhaa zao katika viwanja vya Mukendo mjini Musoma.
Ameongeza kuwa mpango wa Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, umelenga kuhamasisha utalii na kwamba ni wa kwanza kuanzishwa Afrika ya Mashariki utakaoanzia mkoa wa Mara.
Post a Comment