HEADER AD

HEADER AD

TMDA YAMKAMATA MSAMBAZAJI WA DAWA BANDIA ZA BINADAMU

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki imefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa kuzalisha na kusambaza dawa bandia za binadamu William Japhet Mwangile mkazi wa  maeneo ya Matembele Lodge Kipunguni Kata ya Kipawa, Ilala, Dar es Salaam.

Mtuhumiwa huyo amekuwa akitafutwa na TMDA tangu mwezi Machi, 2023 kufuatia kukamatwa kwa baadhi ya dawa anazodaiwa kuzizalisha na kuzisambaza pamoja na watu aliokuwa anashirikiana nao katika usambazaji.

Akielezea katika eneo la tukio, Mkaguzi wa Dawa wa TMDA Kanda ya Mashariki,  Japhari Mtoro amesema kuwa TMDA ilikuwa inamtafuta mtuhumiwa huyo  kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza dawa hizo bandia zikiwa zimefungashwa kwenye makopo kinyume cha kifungu cha 76 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura  219.


"Mtuhumiwa amepatikana April 14, 2023 mchana kufuatia taarifa za kiinteligensia na mtego uliokuwa umewekwa na vyombo vya dola. TMDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali za mitaa, tumefanya upekuzi nyumbani kwake maeneo ya Matembele  na nyumbani kwa wazazi wake maeneo ya Kitunda relini " Amesema Japhari Mtoro.

Amesema kuwa vitu mbalimbali vinavyohusiana moja kwa moja na tuhuma zinazomkabili vimepatikana.

"Nyumbani kwake tulibahatika kupata lebo 537 za ambazo zimekwishachapishwa taarifa za dawa(printed labels) mfano Quinine Sulphate, Erithromycin, Ampiclox, Paracetamol, tulikuta makopo 12  matupu ambayo hutumika kufungasha dawa.

Pia tulikuta viroba vitatu , kiroba kimoja unga wa njano na viwili unga mweupe unaodhaniwa kuwa ndizo malighafi zinazotumika kutengeneza dawa hizo.


"Lakini pia kwa upande wa nyumbani kwa wazazi wake  tumefanikiwa kukamata  jumla ya lebo 142 zilizokwishachapishwa taarifa za dawa na kufanya jumla ya lebo zilizokamatwa kuwa 679, vilevile, tumekuta virobo viwili vyenye kapsuli za dawa aina ya Ampiclox zikiwa hazina kitu" amesema Jafari.

Amesema kuwa mtuhumiwa huyo ataunganishwa na wenzake waliokwisha kukamatwa  na watafikishwa  kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuwajibika na tuhuma zinazowakabili.

Japhari amesema tukio hilo ni la uhalifu dhidi ya binadamu kwani ni  la unyama na ukatili wa hali ya juu kwani mtu anazalisha dawa bandia, dawa ambazo pengine hamna kitu humo ndani, mtu anatumia dawa anategemea atapona, lakini anakutana na dawa bandia zinazoweza kusababisha mtu kupoteza maisha.


"Lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa serikali ya mtaa, jeshi la Polisi, na wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa uliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu" amesema Japhari.

Mjumbe wa shina namba 6 wa Matembele ya kwanza maarufu Matembele Lodge,Marygrogory Mambo
aliyekuwa akishirikiana na TMDA na jeshi la Polisi kwenye upekuzi huo, ameomba wananchi waendelee kushirikiana kutoa taarifa kwa TMDA kufichua hali kama hiyo ya watu wanaofanya ama kutengeneza dawa bandia.




No comments