DC MASWA ATAKA WATENDAJI KUADHIMISHA SIKU YA LISHE VIJIJINI
Na Samwel Mwanga, Maswa
WATENDAJI wa Kata katika halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wametakiwa kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa mkataba wa Lishe hususani katika kuadhimisha siku ya lishe ngazi ya vijiji.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema hayo katika kikao cha tathimini ya mkataba wa Lishe ngazi ya Kata na Kijiji kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisini kwake mjini Maswa.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichowashirikisha Watendaji wa Kata 36 na baadhi ya wajumbe wa kamati ya lishe ya wilaya hiyo amesema kuwa siku hiyo ni muhimu kwani hapo ndipo inapotolewa elimu ya lishe na afya.
Amesema katika maadhimisho hayo ndipo wanapojitokeza watu wengi hivyo ikitolewa elimu hiyo inawafikia walio wengi kwa wakati mmoja na hiyo itasaidia wilaya hiyo kufikia malengo yake iliyojiwekea juu ya masuala ya lishe.
Watendaji wa Kata katika halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha kamati ya Lishe cha wilaya hiyo
"Maadhimisho ya siku ya lishe kwa ngazi ya kijiji ni muhimu sana hapo ndipo mahali unapowapata watu wengi kwa wakati mmoja na wanapatiwa elimu ya Lishe na Afya hivyo ni lazima tuitekeleze kwenye maeneo yetu,"
” Tupange mikakati ili Vijiji vyote viweze kuazimisha siku ya lishe kwa wakati hii itatusaidia sana kama wilaya kufikia malengo yetu katika wilaya,"amesema.
Pia amesisitiza suala la utoaji wa chakula kuanzia shule za Awali, shule za msingi na shule za sekondari katika wilaya hiyo kwani ni mojawapo ya kuwafanya wanafunzi kuongeza ufaulu.
Amesema kuwa ni vizuri kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa kila shule walao inatoa uji au chakula cha mchana kwa wanafunzi kwani kuna baadhi ya wanafunzi hawapati chakula wanapokuwa nyumbani.
"Hakikisheni kwa zile shule ambazo hazijaanza kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi au uji ni vizuri washirikisheni wananchi ili wanafunzi wapate chakula hii ni agenda ya mkoa ni lazima tuitekeleze maana kuna wanafunzi hawapati chakula kabisa mchana wanaporudi nyumbani,"amesema.
Aidha amewapongeza watendaji hao kwa kutekeleza vizuri afua za lishe katika maeneo yao hasa wale walioweza kuazimisha siku ya lishe na afya katika maeneo ya vijiji vyao.
Awali Afisa Lishe wa wilaya ya Maswa,Abel Gyunda amesema kuwa katika kupitia kadi Alama ya Robo ya tatu ya mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.
Afisa Lishe wilaya ya Maswa,Abel Gyunda(aliyesimama)akitoa taarifa ya Lishe ya wilaya hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye shati la kitenge)
Amesema maeneo mengi yamefanya vizuri katika afua ya lishe na hivyo ni vizuri watendaji hao kwenda kusimamia mambo yote ya utekelezaji ambayo wanakubaliana kwenye vikao
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Simon Berege ametoa motisha ya sh 50,000/- kwa kila mmoja ambayo ni watendaji wa Kata waliofanya vizuri katika masuala ya lishe katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Simon Berege (kulia)akimpongeza Mtendaji wa Kata ya Ipililo,Bahati Masekelo(kushoto)baada ya kuwa ni miongoni mwa Kata zilizofanya vizuri kwenye Afua za Lishe kwa kipindi Cha Mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.
Watendaji waliopewa zawadi hizo ni kutoka Kata za Buchambi, Ipililo, Mwamanenge na Bugarama.
Pia amesema Vijiji vinatakiwa kuweka suala la lishe kama kipaumbele cha kwanza na kuhakikisha kidogo kinachopatikana kinatumika katika masuala ya lishe.
Post a Comment