HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI WAKERWA NA UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI, MILIMA

>>Halmashauri ya mji Tarime yatupiwa lawama kutosimamia sheria

>>Ni kutokana na baadhi ya wananchi kujenga karibu na vyanzo vya maji na wengine kujenga milimani

Na Dinna Maningo, Tarime

MADIWANI wa Halmashauri ya Mji Tarime mkoani Mara wameitupia lawama halmashauri kwa kushindwa kusimamia sheria ili kuhakikisha vyanzo vya maji na milima vinalindwa.

Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani hivi karibuni Mei, 17, 2023, Madiwani wamesema kuwa kumekuwepo na wimbi kubwa la watu kujenga na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji wa samaki kwenye vyanzo vya maji na wengine wakijenga nyumba za kuishi na kulima mazao kwenye milima.

Diwani wa viti maalum Nuru Hando amesema anashangaa kusikia kuwa halmashauri imeendesha doria na wananchi kukamatwa waliojenga na kufanya shughuli kwenye vyanzo vya maji na milima hili hali wananchi wanaendelea kujenga nyumba na kufanya shughuli za kilimo.

   Diwani wa viti maalum Nuru Hando akizungumza

"Taarifa inasema doria imeendeshwa na wananchi wamekamatwa wanaoharibu vyanzo vya maji na milima na elimu ya uhifadhi wa mazingira imetolewa.

" Hii doria imefanyika wapi na lini? kwasababu mimi naishi karibu na mlima naona watu wanajenga mlimani wanaishi mlimani, hivi wazee wetu wangeharibu vyanzo vya maji na milima kizazi cha sasa kingekuweje?" amehoji.

Amesema vyanzo vya maji kuvamiwa limekuwa jambo la kawaida " Kuna watu wamejenga kuta kwenye maji na kulazimisha kusogeza mto upite njia nyingine.

" Jamani haya maji hayasahau mkondo wake ndio maana tunakutana na hasara. Idara ipo watu wapo na wanachukua mshahara wa Serikali na wala hawaendi kutumika ilivyo"amesema Diwani Nuru.

Diwani wa Kata ya Bomani Philimon Gotora ameongeza kusema " Kuna wananchi wamejenga ukuta karibu na mto na hivi karibuni mvua ilinyesha ukuta ukabomoka, watu watatu wakasombwa na maji bibi na wajukuu wake wawili na watu bado wanaendelea na ujenzi karibu na mto" amesema.

Diwani wa Viti Maalum Salma Abubakhar ameongeza kusema kuwa Kata ya Turwa mtoto mmoja alinusurika kifo baada ya kusombwa na maji.

                     Madiwani

Ameitaka halmashauri kuhakikisha inazuia wananchi kujenga kwenye vyanzo vya maji kinyume na utaratibu.

Akijibu malalamiko ya Madiwani, Diwani wa Kata ya Turwa ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Chacha Machugu amesema doria imefanyika na waliohusika na uharibifu wa vyanzo vya maji wamekamatwa na zoezi la wananchi kuondolewa kwenye vyanzo vya maji na milima linaendelea.

    Diwani wa Kata ya Turwa ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Chacha Machugu akizungumza

"Doria imefanyika maeneo ya mlima Chambili wapo waliokamatwa na wanachi wamepata elimu, tunaomba wananchi wasijenge kwenye vyanzo vya maji, wananchi wasivamie kujenga milimani .

"Tumejipanga vizuri na ndio maana tupo saiti, Watendaji wote wa Kata wamepewa barua na wanatakiwa kushirikiana na wataalam kuhakikisha wale wote waliojenga kwenye vyanzo vya maji wanaondoka wakiwemo na wanaoishi milimani.

"Tunaomba na wananchi waliopo hapa kama mmejenga mjiandae kupisha kwasababu wakati wowote halmashauri inaenda kubomoa nyumba zilizojengwa bila utaratibu" amesema Diwani Chacha.

Ameongeza kuwa kilimo, mifugo na uvuvi vinachangia uhalibifu wa vyanzo vya maji" Wakulima na wavuvi wanaingilia mazingira, kuna watu wanafuga samaki kwenye vyanzo vya maji vya mto, watu wanalima mashamba karibu na mto. Naomba wafugaji wa samaki wapewe semina wasifuge karibu na mto". Amesema Chacha.
Pia Madiwani wameitaka halmashauri kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umbali wanaotakiwa kuacha kutoka kwenye vyanzo vya maji kutokana na kuwepo mkanganyiko, baadhi wakidai ni umbali unaotakiwa kuachwa ni  mita 60 na wengine mita 30.

Wakati huohuo, Diwani Chacha Machugu amesema kuwa wananchi wanatakiwa kulipa fedha za takataka bila kujali ni nani ili zifike eneo husika la Magena. 

"Lori linahitaji mafuta, vibarua walipwe fedha, ikibidi Halmashauri itumie sheria ndogondogo mwananchi ambaye hataki kulipa hatua zichukuliwe"Amesema.

Diwani wa Kata ya Sabasaba Raymond Nelson amesisitiza usafi wa mazingira ikiwemo kuwepo kwa maeneo sahihi ya kuhifadhi takataka hasa katika mtaa wa mwangaza ambapo takataka zimekuwa kero kwa wananchi.

    Diwani wa Kata ya Sabasaba Raymond Nelson

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Tarime ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamisangura Thobias Ghati ameiagiza Halmshauri hiyo kutekeleza maagizo ya kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema Kamati hiyo ya siasa iliagiza kuhamishwa kwa takataka katika mtaa wa Mwangaza na kuzipeleka kwenye eneo husika Magena.

No comments