HEADER AD

HEADER AD

MILIONI 2 YA CHONCHORI YAWALIZA MACHOZI YA FURAHA WANAKWAYA ANGLIKANA

Na Dinna Maningo, Tarime

WANAKWAYA wa PARADISO Kanisa la Anglikana Mabatini mkoani Mwanza wamejikuta wakibubujikwa na machozi ya furaha huku baadhi yao wakisujudu chini na kulia baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Mkoa wa Mara Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chonchori kuwachangia fedha Milioni mbili alizotoa papohapo.

Danie aliyekuwa mgeni rasmi alitoa fedha hizo wakati akizindua albam ya Kwaya ya PARADISO itwayo 'WANANE yenye Nyimbo 11, uzinduzi uliofanyika katika kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tarime ambapo alitoa pia Tsh. laki mbili ya kufungua box lililokuwa limebeba Flash zenye nyimbo hizo.

Mjumbe huyo wa mkutano mkuu Taifa aliendesha zoezi la uchangiaji fedha akiwa ameongozana na rafiki zake ambao wote pamoja na waumini wa kanisa hilo walichanga fedha kiasi cha jumla Tsh. Milioni 13.

Mwalimu wa Kwaya ya Paradiso akimkabidhi Daniel Chonchori Albamu ya kwaya ya Paradiso 

Uzinduzi huo ulifanyika Mei, 7, 2023 katika Kanisa la Anglikana mjini Tarime ambapo kwaya mbalimbali za kanisa hilo zilishiriki uzinduzi huo na kuchangia fedha.

Kitendo cha wanakaya kulia machozi ya furaha mgeni rasmi akaguswa na kwaya hiyo na hivyo kuwatangazia kuwa mlezi wao na kuahidi kuendelea kuwasaidia katika mahitaji yao ya kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.

Wakifurahi  huku wengine wakilia machozu ya furaha baada ya Daniel Chonchori aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albam yao baada ya kutoa Milioni mbili

Daniel Chonchori ambaye ni muumini wa kania la Waadventista Wasabato kabla ya kuzindua albam alimwomba mwezi Mungu kuibariki shughuli hiyo ya uzinduzi na kuomba waumini na wageni kuimba wimbo kutoka kitabu cha nyimbo namba 116.

Kiongozi huyo wa kisiasa ametoa shukrani kwa kanisa hilo kumualika katika uzinduzi wa albam huku akisisitiza kuwa kazi ya Mungu haichagui kanisa.

  Waliosimama mbele Kushoto ni Daniel Chonchori na Mlezi wa kwaya ya Paradiso Julius Johannes Mwita (Sheby) wakimtukuza Mwenyezi Mungu

"Nilipewa wito na Sheby mimi ni Mwadventista Msabato kwenye kazi ya Mungu hatuwezi kupungukiwa haijalishi ni kanisa gani ilimradi tunajitolea kufanya kazi ya Mungu.

"Mimi ni mfanyabiashara wilaya ya Tarime ni mzaliwa wa Tarime mkazi wa Tarime na Mwanza, naipongeza kwaya ya Paradiso kwa kazi wanayoifanya ya kueneza injili kwa njia ya uimbaji."amesema Daniel

Kiongozi huyo wa CCM ameongeza kusema" nimesikia mahitaji yenu ya gari na vifaa vya mziki, Mungu wetu wa mbinguni atatubariki na gari litanunuliwa. Nilipopata mwaliko huu sikusita niliona ni nyumbani kwakuwa niliwahi kuwa mpangaji kwenye moja ya vibanda vya kanisa hili na nilikuwa mlipa kodi mzuri" amesema.


Mbali na michango ya waumini wa kanisa hilo marafiki wa Daniel Chonchori nao hawakuwa nyuma kumuunga mkono mgeni rasmi nao walichanga fedha kuunga juhudi za waimbaji hao.

Diwani Mstaafu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ryoba Mang'eng'i amesema amekuwa pamoja na Kiongozi huyo kwenye shughuli za biashara tangu 1998.

       Ryoba Mang'eng'i (aliyesimama)

"Chonchori aliponiambia amealikwa kwenye mchango wa bwana nami sikusita kufika kwasababu ni kazi ya bwana namuunga kwa sh.300,000"amesema.

Chomete Samwel naye akasema" Chonchori ni ndugu yangu mimi ni Msabato nyie ni Anglikana sisi sote ni wana wa Mungu mimi nachangia Tsh. 200,000.

Zakayo Chacha Wangwe kijana wa Marehemu aliyewahi kuwa mbunge Jimbo la Tarime Chacha Wangwe yeye akamuunga Tsh. 50,000 ambapo aliahidi kulipa 50,000 kupitia M-Pesa.


Lucus Marwa Kirima alimunga kwa kuchangia Tsh. 55,000 huku Macheda Fedrick akimuunga kwa Tsh. 20,000 na wakamshukuru kiongozi huyo kuchagia kazi ya Bwana.

Askofu wa Kanisa hilo la Anglikana Dayosisi ya Tarime Dkt. Mwita Akili alimshukuru Daniel kwa huduma hiyo ya utoaji ambayo imewagusa wanakwaya .

    Kulia ni Askofu wa Kanisa hilo la Anglikana Dayosisi ya Tarime Mwita, kushoto Daniel Chonchori

"Huwa tunazuia wachungaji wasialike Viongozi wa kisiasa maana wengi wakipewa mwaliko hawafiki na wakifika wanatoa elfu 50,000 tukaona bora tufanye sisi wenyewe.

" Chonchori wewe ni wa tofauti nimebarikiwa sana na huduma yako unaona kazi uliyoifanya imegusa watu wamelia. Ninyi Paradiso twendeni tukamtumikie Mungu vizuri tukafanye vizuri, Chonchori umefika mbali nenda ukaishi katika imani" amesema Askofu Mwita.

Awali akisoma Risala ya Kwaya ya Paradiso kwa mgeni rasmi ya uzinduzi wa mkanda wa video uitwao (WANANE), Afisa Mipango wa kwaya hiyo Jenifa Balianga amesema kikundi cha kwaya kilianzishwa mwaka 1997 ikiwa na wanakwaya wanne na hadi sasa ina wanakaya 25.

    Afisa Mipango wa kwaya hiyo Jenifa Balianga

" Tumefanikiwa kurekodi Audio itwayo MUNGU TUNAKUOMBA USHUSHE AMANI iliyozinduliwa 2008 na kupata vyombo vya mziki ambavyo ni spika mbili zenye gharama ya Tsh. 1,400,000.

"Tumefanikiwa kutembelea wagonjwa hospitali kuwapatia huduma ya kiroho na kuchangia damu na kusaidia wasio jiweza pamoja na kurekodi mkanda wa Video uitwao WANANE iliyozinduliwa kanisani Angikana Tarime mjini.

Jenifa akaeleza kuwa kwaya inakabiliwa na changamoto ya gari la usafiri pindi inapotaka kwenda kufanya huduma sehemu mbalimbali hivyo inashindwa kufika kwa wakati.

              Kwaya ya Paradiso

"Kwaya haina vyombo vya kuhubiri injili pamoja na changamoto hizo kwaya imeweka kipaumbele cha kwanza ni kupata gari la usafiri aina ya Coster yenye thamani ya Tsh.Milioni 50  ambapo imekusanya Tsh. Milioni 5 na kipaumbele cha pili ni vyombo vya mziki vyenye thamani ya Tsh. Milioni 50.

Mtumishi katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tarime Julius Johannes Mwita (Sheby) ambaye ni Katibu wa CCM Kata ya Turwa Tarime na mlezi wa kwaya ya Paradiso yeye na wanakwaya wamemshukuru Daniel Chonchori kwa kutenga muda wake kwa ajili yao katika kushiriki kwenye uzinduzi na kumuomba kuendelea kuwaunga mkono huku wakimshukuru kuwa mlezi wao.



   Marafiki wa Daniel Chonchori walioshiriki kwenye uzinduzi wa Albam























No comments