MME WA MWENYEKITI WA KITONGOJI AUAWA KWA KUCHOMWA KISU NYAMONGO
Na Dinna Maningo, Tarime
MKAZI wa Kitongoji cha Lamboni Kijiji cha Nyangoto Kata ya Matongo-Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara, Mwita Tontora jina maarufu Mwita Bakungu ameuawa kwa kuchomwa kisu akiwa kwenye Baa (Bar) yake iliyopo Kijiji cha Murito Kata ya Kemambo na kisha mtuhumiwa kutokomea.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Murito Yakobo Ryoba Irondo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Mwita Tontora alichomwa kisu na kijana wa Kijiji hicho Mei,8, 2023 majira ya saa tano usiku na amekimbia baada ya kutenda kitendo hicho cha kinyama.
"Mwita Tontora ameuawa kwa kuchomwa na kisu na mlevi mmoja kijana aliyekuwa anakunywa bia kwenye Baa yake, ilikuwa mida ya saa tano usiku wa kuamkia leo Mei, 9,2023, mtuhumiwa aliambiwa na Mwita kuwa muda wa kufunga baa umefika ondoka akakataa ndipo akamchoma kisu kisha akakimbia.
"Hajakamatwa nipe muda nifatilie kujua ni nani aliyemchoma maana kwenye nyumba yao wapo vijana watatu sasa sijajua kati yao aliyemchoma ni nani" amesema Mwenyekiti.
Mke wa Marehemu ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lamboni katika Kijiji cha Nyangoto, Veronica Marwa Mnanka amesema alipata taarifa ya kifo cha mmewe mida ya saa sita usiku.
"Alikuwa kwenye Baa yake iliyopo Kijiji cha Murito wakamchoma kisu, amechomwa kisu mida ya saa tano usiku mimi nimepigiwa simu mida ya saa sita kuelekea saa saba, hajakamatwa baada ya kumchoma kisu alikimbia ila walimtambua"amesema Veronica.
Mwita Tontora amefariki wakati akipatiwa matibabu katika kituo cha Afya Nyangoto na mwili wake umehifadhiwa katika kituo hicho cha afya.
Wajumbe wa Serikali ya Kijiji walaani matukio ya uhalifu
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu mkoa wa Mara Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwl. Chacha Sultan amekemea vikali vitendo vya uhakifu na kusema vinachafua taswira ya mji wa Nyamongo huku akiiomba Serikali kukomesha vitendo vya uhalifu.
"Tunasikitika mme wa kiongozi mwenzetu kuuawa akiwa kwenye Bar yake bila kosa lolote, aliyemchoma kisu aliambiwa aondoke Bar ifungwe kwamba muda wa kufanya patroo umefika.
"Wale walevi wakagoma kuwa hawawezi kutoka kuwa wanatokaje wakati hawajashiba, walivyoona wamelazimishwa kutoka ili afunge geti ndipo mmoja akamchoma kisu, tunaomba Serikali itusaidie kukomesha hivi vitendo vya uhalifu" amesema.
Mwl. Sultan amesema kuwa mauaji yanayoendelea Nyamongo ni ya kinyama hivyo jamii inatakiwa kupinga vitendo hivyo na kuwaomba wananchi kujitokeza kutoa ushahidi pindi wanapowabaini wahalifu.
"Tunalaani hivi vitendo wananchi hatuvikubali kabisa na hakuna mtu anayefurahia hivi vitendo vya mauaji, niwaombe watu wanaoshuhudia matukio ya uhalifu wajitokeze kutoa ushahidi ili wahusika wa kesi watiwe hatiani.
"Watu wasipotoa ushirikiano ushahidi unakosekana matokeo yake watu wanaachiwa huru na kurudi kijijini kuendelea na uhalifu" amesema Mwl. Sultan.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati Josephat Elias Haruni ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama Kijiji hicho amesema kuwa ulinzi na usalama Nyamongo umekuwa hafifu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini Kati Josephat Elias Haruni" Ulinzi na usalama umekuwa hafifu watu wanatembea na silaha ovyo na yote haya ni kwasababu kamati za ulinzi na usalama za Vijiji na Kata hazikai vikao mara kwa mara ili kubaini matatizo yaliyopo, maana tunakaa mara moja kila baada ya miezi mitatu na Kamati ya ulinzi na usalama ya Kata tunakaa mara moja kwa mwaka, hapa utaona bado ni tatizo.
" Na hata vikao tunavyokaa yale tunayojadili utekelezaji wake ni mdogo na mwitikio kwa wananchi ni mdogo, inatakiwa kuwa na ulinzi shirikishi imara, matukio ya uhalifu Nyamongo ni mengi, ndani ya miezi miwili nakumbuka matukio ya mauaji yametokea si chini ya matano" Amesema Mwenyekiti huyo wa Kitongoji.
Josephat amesema kuwa mbali na mauaji mji wa Nyamongo umekuwa ukikabiliwa na matukio ya uhalifu yakiwemo ya uporaji wa simu, fedha na watu kuchomwa visu na kukatwa mapanga.
Amewaomba wananchi kushirikiana pamoja kukomesha vitendo vya uhalifu ambavyo vimesababisha kutoweka kwa amani na watu kuishi kwa hofu.
Ameongeza kuwa wananchi wana wajibu wa kuwataja wahalifu na sio jukumu hilo kuwaachia Polisi pekee huku akiviomba Vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha usalama wa raia Nyamongo.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kijiji cha Murito - Nyamongo Yakobo Ryoba Irondo amesema mkazi wa Kitongoji cha Morogo Senta Seth Mwita Kichonge amekutwa amekufa akiwa ndani ya shimo la uchimbaji wa dhahabu linalomilikiwa na mchimbaji wa dhahabu Mwita Masiaga.
" Amekutwa amekufa ndani ya shimo Clemu ya Mwita Masiaga,amekutwa leo asubuhi Mei, 9,2023 Wakati wa usiku hayo mashimo huwa yanafungwa sasa hatujui alidondoka au laa na ni muda gani. Taarifa zimekwenda Polisi ili waje kuchunguza" amesema Mwenyekiti huyo.
Post a Comment