NADO YAZINDUA MRADI KUSAIDIA WAKULIMA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI
Na Andrew Chale, Njombe
SHIRIKA la Maendeleo ya Kilimo Mkoa wa Njombe (NADO), limezindua mradi wa "From Reactive to Proactive adaptation" ambao utamsaidia mkulima kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kabla hayajatokea katika maeneo yao badala ya kusubiri yatokee.
Awali akizungumza wakati uzinduzi huo, Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika hilo la NADO,Ernest Ng'umbi amesema wakulima elfu Nne (4,000) wa mikoa ya Njombe, Iringa na Songwe wanaenda kunufaika na mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne huku ukiwa umetengewa kiasi cha fedha Tsh.Milioni 850.
Aidha, Ng'umbi ameeleza kuwa Shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali kwenye sekta ya kilimo, misitu na masuala mtambuka kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi.
"Kupitia Wizara ya mambo ya ndani ya nchi ya Finland na Shirika lisilo la kiserikali la nchini humo FFD, tumepata mradi huu kwa maana 2023-2026.
Mradi huu umelenga kujihakikishia usalama wa chakula, lishe na kipato kwa Wakulima ambao watafikiwa." Amebainisha Ng'umbi.
Aidha, Mkurugenzi wa Shirika hilo la NADO, Jonathan Ngilangwa amesema kuwa, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni lazima wakulima wafundishwe namna ya kulima kilimo hifadhi ikiwa ni pamoja na kupanda miti.
Kwa upande wake, Afisa kilimo mkoa wa Njombe, Joel Wilson akizungumza kwenye uzinduzi huo, amesema kutokana na baadhi ya maeneo kukumbwa na ukame unaosababishwa na mvua kunyesha chini ya wastani kumesababisha uzalishaji wa mazao mbalimbali kushuka na kusababisha kupanda kwa bei kwa mazao hayo nchini.
"Imeripotiwa kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo vyakula na bidhaa mbalimbali kutokana na mvua kunyesha chache na kuchangia uzalishaji kushuka." Amesema Joel Wilson.
Nao maafisa kilimo, Mkuu wa idara ya kilimo mifugo na uvuvi kutoka halmashauri ya wilaya ya Makete, Aniset Ndunguru na Afisa kutoka Halmashauri ya mji wa Makambako, Telesphory Danda wamesema mradi huo unaenda kuwanufaisha wakulima kwa kuwa watafundishwa namna ya kulima kilimo hifadhi ambacho kitatunza mazingira na kuongeza kasi ya uzalishaji.
Nao baadhi ya wakulima, Huruma Mgaya na Andrew Mbata wamesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wamekua wakipata hasara katika uzalishaji wa mazao yao kutokana na mvua kunyesha chache na wakati mwingine kunyesha kubwa na kusababisha washindwe kuweka mbolea.
Post a Comment