HEADER AD

HEADER AD

RPC JONGO: WATAZAMENI WASICHANA KAMA DADA ZENU NA WATOTO WENU

>>Ni kutokana na kuwepo ongezeko la mimba kwa wanafunzi 

>>Polisi kuwakamata wazazi watakaoshindwa kusimamia watoto wao

Na Daniel Limbe,Chato

KATIKA kukabiliana na wimbi la mimba za umri mdogo nchini, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita Safia Jongo,ametoa ushauri kwa vijana wa kiume kuwatazama wanafunzi wa kike kama dada zao sambamba na wanaume watu wazima kuwaona mabinti kama watoto wao.

Ushauri huo umetolewa kufuatia ongezeko la mimba za umri mdogo kwa wananfunzi wa shule za msingi na sekondari jambo linalodaiwa kukatisha ndoto za mtoto wa kike kupata elimu bora.

Kamanda Jongo ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kachwamba, Nyamirembe na Bwongera wilayani Chato mkoani Geita huku akiwatahadharisha wazazi kwa malezi mabovu kwa watoto wao.

   Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita,Safia Jongo akizungumza na Wananchi

"Jamani kama ningepewa ujauzito nikiwa shuleni nisingekuwa kamanda, basi niwasihi kila kijana amwone binti mwanafunzi kama dada yake na kila baba amuone binti mwanafunzi kama mtoto wake tuwalinde watoto wa kike".

"Wewe mzazi ambaye mwanao anatoroka shule anakwenda huko kwenye machimbo anaenda kutumwa huko kwenye kilimo huchukui hatua nilielekeza na bahati nzuri nimepata wasaa wakuzungumza na wananchi, tutawakamata wazazi ambao hawasimamii watoto wao" amesema Jongo.

Kadhalika amesema iwapo watoto wakisimamiwa vizuri na kupelekwa shule itasaidia kupunguza vibaka na wahalifu wengine mtaani hali itakayosaidia wananchi kuishi kwa amani na kufanya kazi za maendeleo kwa amani.

              Wananchi wakimsikiliza RPC Safia

Akiwa kwenye kata ya Bwongera,Jongo amewasisitiza wananchi kushirikiana katika ulinzi shirikishi kwa kile alichoeleza kuwa usalama wa mtu unaanza na yeye mwenyewe badala ya kusubiri huduma ya polisi ambao hata hivyo hawawezi kuwa kila eneo kulingana na uchache wao.

Mbali na hilo, ameonyesha kusikitishwa na wingi wa matukio ya kihalifu yanayotokana na imani potofu za kishirikina ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwaua wazazi wao na wengine wake zao jambo linalochafua taswira nzuri ya mkoa wa Geita.


                         

No comments