Home
/
HABARI KITAIFA
/
SSP MGEMA: WAANDISHI WA HABARI JIKITENI KWENYE UANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGUZI
SSP MGEMA: WAANDISHI WA HABARI JIKITENI KWENYE UANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGUZI
>>Asisitiza uandishi wa kiuchunguzi wa kufichua maovu yanayotendeka kwenye jamii.
>>Diwani Golden awashauri Waandishi wa Habari kuzunguka mitaani kutafuta habari na kuibua changamoto
Na Dinna Maningo, Musoma
WAANDISHI wa Habari mkoani Mara, wameshauriwa kujikita katika uandishi wa habari za kiuchunguzi ikiwa ni pamoja na kuibua maovu ukiwemo uhalifu na sintofahamu zinazojitokeza kwenye jamii.
Hayo yamesemwa na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Mara, SSP Mathew Mgema katika maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa Mei, 12,2023 mjini Musoma katika ukumbi wa John Rudin Mwembeni Coplex.
Waandishi wa Habari na wadau mbalimbali wameshiriki maadhimisho hayo kwa majadiliano mbalimbali yakiwemo ya utoaji taarifa.
"Waandishi wa Habari ni muhimu sana, niwashuri tujikite sana kwenye uandishi wa habari za kiuchunguzi. Uandishi wa kiuchunguzi wa kufichua maovu kwenye jamii ukiwemo uhalifu na sintofahamu zinazotokea kwenye jamii zetu"Amesema SSP Mathew.
Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi amesema kuna uhalifu unafanyika ndani ya jamii lakini haufanyiwi tafiti, hivyo wananchi kujikuta wakipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii ambazo hazijafanyiwa utafiti.
"Kuna suala la ushoga linaloendelea, je tumelifanyia utafiti kwa kiwango gani? wakati mwingine jamii inaingia kwenye taharuki ni kwasababu kwa namna moja au nyingine waandishi wa habari tumeshindwa kutimiza wajibu wetu.
"Kwahiyo unakuta jamii ikitegemea mambo yanayorushwa kwenye mitandao ambayo hayajafanyiwa utafiti. Tuibue maovu kwenye jamii "Amesema SSP Mathew.
Mrakibu huyo amesema kuwa ni wajibu wa Taasisi mbalimbali kutoa taarifa na kwamba kitendo cha Waandishi wa Habari kufika ofisini na kunyimwa habari huo ni urasimu.
"Kitendo cha kufika kufuata taarifa alafu unanyimwa taarifa huo ni urasimu. Jeshi la Polisi lina utaratibu wa utoaji taarifa ambapo msemaji ni RPC wa mkoa husika.
"Kwa upande wa Polisi unapozungumzia hali ya uhalifu au tukio limetokea katika mkoa kusika msemeji ni RPC, hivyo unatakiwa kupata taarifa badala ya kushughulika na mtu ambaye siyo msemaji wa Polisi alafu mtu anasema hapati taarifa lakini kumbe tunapaswa kujua taratibu zipoje katika upataji wa taarifa"amesema.
Pia, amewaomba waandishi wa habari kujikita pia kwenye taarifa zenye maslahi kwa jamii na Taifa kwa ujumla pamoja na kutoa taarifa kwa uhalisia.
Diwani awaasa Waandishi wa Habari kuripoti habari za kijamii
Diwani wa Kata ya Kitaji Golden Marcus kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amewapongeza Waandishi wa Habari kwa jitihada zao za kuhabarisha jamii.
Diwani huyo mbali na kuwapongeza waandishi wa habari amewahimiza kwenda kwenye jamii mitaani kuibua habari zikiwamo za changamoto, tatizo la ajira, kuwakumbusha watumishi wajibu wao na habari za maendeleo.
"Waandishi wa Habari kwa kiasi kikubwa mnaegemea sana kwa taasisi za Serikali kuripoti taarifa zao, lakini kuna sehemu kubwa mnaiacha ambayo ni wananchi.
"Waandishi wa Habari hamzunguki mitaani kutafuta habari, habari nyingi zinazoripotiwa ni za taasisi za serikali, Waandishi waingie kwenye jamii moja kwa moja kutafuta habari.
Ameongeza "Waandishi wa Habari waingie moja kwa moja kwenye jamii na kuibua mambo mbalimbali yanayowasaidia wanajamii katika kukabiliana na changamoto.
"Sijajua tatizo ni uwezesho au tunajali penye maslahi. Clouds Tv wana kipindi cha jicho la mwewe, kile kipindi kinasaidia sana kuibua kero kwenye jamii na serikali inazitatua.
"Lakini kwa kipindi kirefu tumeona waandishi wa habari wamekuwa kimya wanaripoti taarifa za serikali zaidi kuliko taarifa za jamii kwenda kwa Serikali.
Diwani huyo amewaomba Waandishi wa Habari kuyatumia maadhimisho hayo ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kufika kwenye jamii moja kwa moja kuibua changamoto ili kuisaidia jamii.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mara, Raphael Okelo amewaomba wadau mbalimbali wa Serikali na Taasisi kushirikiana na Waandishi wa Habari katika utoaji wa taarifa.
Post a Comment