RC CHALAMILA AOMBA KUANZISHWA KANDA MAALUM KAGERA
>> Ni kutokana na kukithiri matukio ya mauaji
>>Aomba Bugarama kuwa Wilaya ya Kipolisi
>>Polisi, Tembo Nickel wasaini makubaliano ya ulinzi na usalama kwa jamii
Alodia Babara, Ngara
MKUU wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amemuomba Kamishna wa Polisi wa oparasheni na mafunzo nchini Awadh Juma kufikisha ombi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camillius Wambura la kuanzisha Kanda maalum ya Kagera kutokana na matukio ya mauji yanayotokea kila siku wastani wa mtu mmoja na kwa mwezi watu 28 hadi 30.
Chalamila ametoa ombi hilo Mei 12, 2023 wakati kampuni ya Tembo Nickel inayochimba madini ya Nickel wilaya ya Ngara mkoani Kagera ilipokuwa ikisaini mkataba wa makuliano ya ulinzi na usalama kwa jamii na Jeshi la Polisi Tanzania mkataba uliofanyika shule ya msingi Bugarama wilayani Ngara.
Chalamila licha ya kuomba Kagera kuwa kanda maalumu pia ameomba kata ya Bugarama kuwa wilaya ya kipolisi kutokana na kata hiyo kujengwa kituo cha polisi chenye hadhi ya kituo cha mkoa na ipo mpakani ambapo yamekuwa yakijitokeza matukio mbalimbali ya uhalifu.
Aliyevaa suti ni mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila akiwa pamoja na Kamishna wa Polisi Oparasheni na mafunzo Awadh Juma wakishuhudia picha ya kituo cha polisi na nyumba ya mkuu wa kituo hicho vitakavyojengwa kata ya Bugarama
“Niombe maombi machache kwako Kamishna wa polisi utupelekee, najua kwa dhamana yangu ninao uwezo wa kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi lakini kabla sijazungumza naye wewe uondoke nayo kwamba hapa kitajengwa kituo cha polisi chenye hadhi ya mkoa.
"Kituo hicho anapaswa kukaa mtu mzito kidogo, sasa niombe kwamba labda anzeni kuangalia mtu atakayekaa hapa naye aitwe mkuu wa polisi wilaya (OCD) maana yake oneni kama mnaweza kufanya wilaya maalum ya kipolisi”
“Kwa maana kwamba ukianzia Murusagamba kwenda hadi Bukoba yote hayo ni maeneo ya mipaka yawezekana huyu mkuu wa polisi wilaya maalum (OCD) atakaye kuwa huku tukampa pia jukumu la kuangalia vizuri hayo maeneo tuliyoyataja.
"Huyu mkuu wa polisi wilaya ya Ngara akawa na kazi ya kuangalia eneo jingine kwa sababu mgodi wa Tembo Nickel utakaribisha watu wengi sana kwa hiyo ningeomba muanze kuangalia namna gani mnaweza kufanya hadhi ya kituo iendane na hadhi ya mkuu wa kituo na iendane na hadhi ya ukanda kwa ujumla kuwa angalau maalum” Amesema Chalamila
Chalamila amekazia ombi lililotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Wiliam Mwampagahle la kuongeza askari zaidi ya 100 katika kituo cha polisi kitakachojengwa Bugarama kutokana na kwamba askari hao watalinda maeneo ya mgodi masaa 24 pia watatakiwa kuwekwa maaskari katika mradi wa umeme Rusumo unaozihusisha nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi na katika benki za CRDB na NMB zinazojengwa Rulenge.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Oparasheni na Mafunzo Awadh Juma amesema kuwa, maombi aliyoyatoa mkuu wa mkoa kwa niamba ya jeshi la polisi ameyapokea na atayafikisha kwa kwa mkuu wa jeshi hilo nchini (IGP).
Pia atafikisha ombi la uanzishwaji wa wilaya ya kipolisi na uwepo wa askari wengi kwakuwa ni mambo yanayowezekana wanaweza kwenda nayo haraka ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo unakuwepo na hasa ikizingatiwa kwamba wameishakuwa na uhakika wa kujengwa kituo kikubwa cha polisi chenye hadhi kubwa, usafiri na mambo mengine.
Kwa upande wake Meneja wa Mgodi wa Tembo Nickel Manny Ramos ametaja mambo ambayo wamekubaliana kwenye mkataba kuwa ni pamoja na kuboresha kituo cha polisi cha Bugarama kuwa daraja A.
Pia kuongeza kituo kidogo cha polisi katika kijiji cha Muganza na nyumba za askari watakaokuwa wanafanya kazi katika jamii ya tarafa ya Rulenge na kulipatia gari jeshi hilo katika kituo kitakachojengwa ambavyo thamani yake ni zaidi ya Tsh Bilioni moja na mkataba utakuwa wa miaka mitatu.
Kampuni ya Tembo Nickel,Polisi ikisainiana mkataba wa makubaliano ya ulinzi na usalama wa jamii ya kata ya Bugarama
Post a Comment