TANZANIA YAJIVUNIA UTOAJI HUDUMA ZA CHANJO BILA MALIPO
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
MPANGO wa Taifa wa Chanjo kupitia Wizara Afya umebainisha kuwa hadi sasa tayari Tanzania imefikisha Chanjo 10, ambazo ukinga magonjwa 14, ikiwemo UVIKO 19 na Virusi vya HPV vinavyosababisha Saratani ya mlango wa kizazi.
Akizungumza wakati wa warsha ya siku moja kwa Wanahabari mkoa wa Dar es salaam, Afisa Mpango wa Chanjo Taifa, Rotalis Gadau ameeleza kuwa, tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1975, walianza na chanjo Tatu pekee na kadri muda ulivyoenda zimeongezeka na kufikia 10.
Afisa wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Rotalis Gadau Akizungumza katika tukio hilo
Gadau amezitaja baadhi ya chanjo hizo na ambazo hutolewa bila malipo katika Hospitali na vituo vya Afya vya Serikali na vya binafsi; ni chanjo ya Pepopunda, Kifua Kikuu, Surua, Pepopunda, Polio, Kifaduro na Donda koo.
Pia zipo chanjo za Rubela, Kuhara vikali, Kichomi, UVIKO 19, HPV na zingine.
"Nchi yetu imekuwa ikijitahidi sana kutoa huduma za Chanjo kwa kiwango cha hali ya juu sana.Chanjo zetu zinatolewa bila malipo.
Chanjo sio bure, ila zinatolewa bila malipo kutokana zinafadhiliwa na Wadau wetu". Amesema Gadau.
Amesema Chanjo moja ina gharama kubwa, hivyo mfadhili mkuu ulipia fedha na Serikali pia ikitoa asilimia kadhaa.
"Wazazi wapeleke watoto wao kupata chanjo. Chanjo zipo za kutosha kipindi chote na ni bure na ni salama kwani Serikali inalinda watu wake, kukinga majonjwa na hata vifo." Amesema Gadau.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa jiji Dar es Salaam, Dk. Milca Mathania amewataka Waandishi wa Habari kuendelea kutoa taarifa sahihi juu ya chanjo zinazotolewa.
Dk. Milka Mathania Akizungumza katika tukio hilo"Tutoe taarifa sahihi ilikuepusha taharuki kwa wananchi. Mkoa wa Dar es Salaam chanjo zote zipo kuanzia ngazi zote za huduma" amesema Dk. Milca Mathania.
Naye Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Ilala Omary Kumbilamoto aliyefunga semina hiyo, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo hizo zinazotolewa nchini.
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Ilala Omary Kumbilamoto"Mtoto asipopatiwa chanjo anaweza akakumbwa na magonjwa ya mlipuko kama Polio, surua na rubella na kuweza kumsababishia ulemavu au hata kifo" Amesema Kumbilamoto.
Aidha Kumbilamoto amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wakike walio chini ya miaka 14 wanapatiwa chanjo ya Saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.
Waandishiwa Habari walioshiriki semina hiyo wamepongeza juhudi za Mpango wa Chanjo wa Taifa kutoa mafunzo hayo.
Post a Comment