HEADER AD

HEADER AD

MAKATO YA MSHAHARA YAWAONDOA WALIMU CWT NA KUHAMIA CHAMA CHA CHAKUHAWATA

Na Waandishi wetu, Musoma

ZAIDI ya walimu 20 wa shule kongwe ya Sekondari Mara, iliyopo katika manispaa ya Musoma mkoani Mara wamekihama chama cha walimu Tanzania (CWT) na kujiunga na chama cha kulinda na kutetea haki za walimu Tanzania (CHAKUHAWATA).

Walimu hao wakiongozwa na Mwl. Josephat Nyarara na Sunday Magacha wamesema wamechoka kuibiwa fedha zao Kwa kulazimishwa kuwa wanachama wa chama ambacho hakina msaada kwao, zaidi ya kupora sehemu ya mishahara yao bila idhini yao.


Nyarara amesema ujio wa CHAKUHAWATA katika kipindi hiki imekuwa mkombozi wa walimu kwa kuwa watakuwa na fursa ya kuchagua chama cha kujiunga kwa ridhaa yao ambapo awali walimu walikosa chama mbadala.

"Kwa miaka yangu yote ya utumishi sikuwahi kukipenda CWT kwa kuwa hata sikumbuki ni lini niliomba uanachama nakujaza fomu ya kisheria Na.15, sasa nimepata chama sahihi na  sikivu kinachonifaa kujiunga kwa hiyari yangu mwenyewe" amesema Nyarara.

Amewaomba walimu kuamka na kudai haki zao Kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 kifungu cha 
61.- (1)(4). 61(1).

"Sheria hiyo inasema Mwajiri atalazimika kukata michango ya chama kilichosajiliwa kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi kama mfanyakazi huyo amemruhusu mwajiri kufanya hivyo katika muundo maalum.61(4) Mfanyakazi anaweza kufuta ruhusa kwa kutoa taarifa ya 
maandishi ya mwezi mmoja kwa mwajiri na chama cha wafanyakazi. 

Mwl. Sunday Magacha amesema ni wakati wa haki za walimu kuwekwa wazi ili kila mmoja awe huru kuchagua chama cha kujiunga nacho kwa mujibu wa sheria hiyo.

 Amesema shule ya Sekondari Mara kama ilivyo kongwe na inayobeba jina la mkoa imekuwa mfano kwa walimu wa mkoa wa Mara kufuata nyayo za kuokoa kiasi cha fedha kinacho katwa kwenye mishahara yao.

"Nitoe tu mfano mdogo mwalimu anachangia asilimia mbili ya mshahara wake, mfano kama ni 940,000 anakatwa Tsh. sh 18,800 kila mwezi sawa na sh, 225,600 Kwa miezi 12.

"Kiwango cha mshahara huo huo CHAKUHAWATA atachangia ada 5,000 kwa mwezi sawa na sh, 60,000 Kwa miezi 12, na kuokoa sh,165,000. Hii ni hesabu ndogo tu lakini wapo wanaokatwa kila mwezi 42,000",amesema Sunday.

Aidha amewaomba waajiri wasiwanyime walimu haki yao ya kufanya maamuzi ya chama kipi wajiunge nacho kwa kuwa ni takwa la kisheria kwani baadhi ya walimu wamekuwa wakinung'unika na kutonufaika na chama hicho kutokana na kukosa haki ya kufanya maamuzi.

Sunday ameongeza kusema kuwa, kujiunga na chama cha watumishi nchini Tanzania ni hiyari na hakuna Mwajiri anayemchagulia mtumishi chama cha kujiunga.

Adai kutimuliwa ofisini baada ya kujiondoa

Mwl.Amon Kimacha wa Mara Sec. amesema amejiondoa kwenye chama cha CWT kutokana na makato makubwa na kuamua kujiunga na chama cha CHAKUHAWATA.


"Nimeandika barua yangu ya kutaka kuondolewa uanachama wa CWT na kuipeleka ofisi za CWT zilizopo Manispaa ya Musoma kata Majita road. Nilipofika kwenye ofisi hiyo PS (Katibu Muhtasi) akaniruhusu kuingia ofisi ya Katibu CWT Magero Misana kuwasilisha kusudio langu.

"Nimempa barua yangu akaisoma baada ya kumaliza kusoma akabadilika akawa mkali akaniambia 'siwezi kusaini wala kujibu upuuzi wako na siwezi kusaini kwenye dispatch na hutofanya chochote na barua zako njaa zinakusumbua'.

 "Akaniambia hawezi kusaini barua na niondoke ofisini kwake nikawa mpole nikatoka ofisini". 

Mwalimu huyo ameongeza "Katibu huyo nimemuomba anirudishie barua zangu hakutaka kabisa kusikia hilo. niliamua kuendelea na msimamo wangu na kufika ofisi ya mkurugenzi kwa ushirikiano na viongozi wengine akiwemo Mwl. Sunday Magacha na Josephat Nyarara.

"Nimepata utaratibu mzuri wa kuandika barua ya kujitoa CWT , nikaenda nikawaeleza wenzangu ilivyotokea nao wakarekebisha barua zao, Walimu 22 wameandika barua za kujiondoa CWT, kuanzia sasa mimi ni mwana CHAKUHAWATA  chama chenye makato kidogo mimi sio mwanachama wa CWT tena na huo ndio msimamo wangu"amesema Mwal. Amon.

Je uongozi wa Chama cha Walimu Tanzania CWT Manispaa ya Musoma unasema nini kuondoka kwa waliokuwa wanachama? endelea kufuatilia DIMA Online

No comments