WANANCHI MASWA WATAKA UJENZI JENGO LA HALMASHAURI UANZE HARAKA
>> Ni baada ya kumalizika mvutano wapi lijengwe jengo la halmashauri
Na Samwel Mwanga,Maswa
WANANCHI katika Halmashauri ya Maswa mkoa wa Simiyu wametaka ujenzi wa jengo jipya la utawala na makao makuu ya halmashauri hiyo uanze haraka mara baada ya mvutano kumalizika mahali itakapojengwa.
Ni baada ya mvutano mkubwa ulikuwepo wapi lijengwe jengo hilo kati ya kilima kilichoko karibu na shule ya sekondari ya Wasichana ya Maswa na eneo la Ng'hami ambapo madiwani walipitisha lijengwe eneo la Ng'hami.
Wakizungumza mjini Maswa baadhi ya Wananchi hao wamendelea kuishukuru serikali kwa kutoa kiasi cha Tsh. Bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
Wamesema kuwa tangu fedha hizo ziletwe na serikali takribani miezi mitatu iliyopita lakini ulizuka mvutano mkubwa kati ya baadhi viongozi na madiwani kuwa ni wapi yajengwe makao makuu ya halmashauri hiyo lakini tayari wawakilishi wa wananchi ambao ni madiwani wameshafanya maamuzi kupitia vikao vyao likiwemo baraza la Madiwani
Wamesema kuwa kwa sasa ujenzi huo uanze mara moja kwani tayari fedha za kuanza ujenzi zimeshapokelewa na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.
"Hakuna haja sasa ya kuchelewa kuanza ujenzi wa makao makuu mapya ya halmashauri yetu ya Maswa tayari fedha imeletwa hivyo sisi wananchi matamanio yetu tuone ujenzi unaanza kama ni eneo tayari lilishapitishwa la Ng'hami katika Kata ya Nyalikungu,"amesema Naomi John.
Imeelezwa kuwa Halmashauri hiyo tangu ianzishwe kwa sasa ina miongo mingi na ndiyo kongwe katika mkoa wa Simiyu ni vizuri sasa nayo ikapata jengo la ghorofa la kisasa na kuondokana na majengo yaliyochakaa ya zamani.
"Hii ndiyo halmashauri kongwe katika mkoa wa Simiyu maana ndiyo imezaa wilaya ya Bariadi na Meatu na mjuukuu wake wilaya ya Itilima hivyo inapaswa kuwa na jengo jipya la kisasa ambalo ndilo litakuwa makao makuu ya halmashauri ya Maswa.
"Kwa sasa ofisi ya Mkurugenzi na wakuu wengine wa divisheni za halmashauri ziko kwenye majengo ya kizamani na nyingine ni za tangu wakati wa mkoloni ambazo zinatumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati,"amesema Paschal.
Boniphace Charles amesema suala la ujenzi huo lisifanywe siasa kwani tayari fedha zimeletwa na eneo limekwishapatika hivyo ni vizuri pande zote mbili zilizokuwa zinalumbana kuungana pamoja na kuhakikisha jengo hilo linajegwa kwa ubora.
"Tuache kuingiza siasa au ujanjaujanja katika ujenzi huu kutokana na maslahi binafsi maana kuna baadhi ya viongozi walianza kutengeneza tuvikundi ili washinikize wapi makao makuu yajengwe hilo limekwisha tuungane sote tuhakikishe jengo linajengwa Ng'hami na tusihujumiane maana wilaya hii ni yetu sote,"amesema Boniphace.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Paul Maige amesema kuwa tayari amekwisha muagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Simon Berege kuanza mara moja ujenzi huo baada ya eneo kupatikana baada ya Wataalam kulitembelea na kuona linafaa.
Jengo la zamani ambalo liko katika makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Maswa na linatumika kama Ofisi
Ameongeza kuwa ujenzi ukianza ambao huo ni mradi mkubwa atausimamia kwa karibu pamoja na madiwani wenzake na watakuwa wakitoa taarifa za mara Kwa mara juu ya ujenzi huo hasa Kwa wananchi wa wilaya hiyo ambao ndiyo wenye jengo lao.
"Ujenzi huu tutausimamia kwa karibu sisi madiwani na wananchi tutakuwa tukiwapatia taarifa za mara kwa mara kila hatua na wale walio na nafasi ya kufika kuona ujenzi huo hawazuiliwi maana hili ni jengo lao,"amesema.
Post a Comment