IGP WAMBURA AWAHAMISHA MA-RPC YUMO WA MARA, TARIME RORYA NA WENGINE
Na David A. Misime, Dodoma
MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillius Wambura amefanya mabadiliko ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa kwa kuwahamisha na wengine kupangiwa majukumu mengine.
Mabadiliko hayo yamefanyika Mei, 15, 2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Jeshi hilo Makao Makuu ya Polisi Dodoma ambapo baadhi ya Makamanda wa Polisi wa mikoa wamehamishwa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, David A.Misime- SACP amesema katika mabadiliko hayo IGP Camillius Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Longinus Alexander Tibishibwamu (RPC) kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma.
Nafasi ya ACP Longinus inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salum Ramadhani Morcase ambaye alikuwa Makao Makuu ya Polisi Dodoma.
Pia amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Geofrey Sarakikya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma.
Nafasi ya Sarakikya inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Michael Njera ambaye alikuwa Makao Makuu ya Polisi Dodoma.
Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi amesema aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Hamis Issah amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelekezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Makuri Imori.
David amesema aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu amehamishiwa mkoa wa Kagera kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Edith Swebe.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Willium Mwampagale amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Pemba.
Post a Comment