CDEA, FIDEC, EMEDO WAADHIMISHA SIKU YA BAHARI DUNIANI
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki [Culture and Development East Afrika] –CDEA kwa kushirikiana na mashirika mengine ya FIDEC na EMEDO wamefanya maadhimisho ya siku ya bahari duniani
Maadhimisho hayo yamefanyika Juni 8,2023, yenye kauli mbiu isemayo 'Sahari bahari' mawimbi yanabadilika ‘’Bahari kwa uchumi wa bluu’’ tukio lililofanyika makao makuu ya CDEA, Mbezi, Dar es Salaam kwa kuwakutanisha wadau wakiwemo wavuvi na wadau wengine.
Awali akifungua tukio hilo, la siku ya bahari, Mkurugenzi wa CDEA, Ayeta Wangusa amesema wadau wanaotumia bahari wana nafasi kubwa ya kuelewa namna bora ya kulinda hivyo elimu sahihi itasaidia bahari kuwa salama.
‘’Kama tunataka kubuni vitu vizuri tunatakiwa kupata ufukwe mzuri kukaa na kujifunza. Leo tumepata kujifunza mengi kuhusu bahari naamini kutoka hapa tunaenda kuwa mabalozi wazuri katika kulinda bahari ambayo tumeambiwa ina utajiri mkubwa.
Huu ni mwanzo na maoni yote yatachukuliwa na Serikali kufanyiwa kazi, hata sisi hapa CDEA tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha tunalinda mazingira kwa kutotumia vitu vya plastiki, lakini pia vitu hivyo tunajaribu kuvitumia kwa matumizi mengine rafiki wa mazingira’’amesema Wangusa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la FIDEC, Grace Andrew amewashukuru wadau kwa kuto elimu sahihi juu ya utunzaji wa bahari.
‘’Tumeguswa na suala la takataka za pastiki zinazoingia baharini, kwani tafiti zinaonesha tani nyingi sana zinaingia baharini hivyo tunapaswa kuchukua hatua zaidi kulinda bahari.
"Nimependa maoni mbalimbali yaliyotolewa hapa na wadau ikiwemo suala la kuwekwa chujio kwenye kingo za bahari ilikuzuia takataka hizi hasa machupa ya pastiki kuingia kwenye bahari’’amesema Grace .
Nae Mkurugenzi wa EMEDO, Editrudith Lukanga amewashukuru wadau kwa pamoja kushiriki tukio hilo kwani linaenda kuwa tukio kubwa kwa ushiriako wa mashirika yote pamoja na wadau wengine.
‘’Leo mashirika matatu tumeweza kuandaa tukio hili, tunaamini huu ni mwanzo ila tutaendelea kufanya makubwa hapo baadae katika kulinda bahari.’’ Amesema Lukanga.
Aidha, wakichangia maoni yao wakati wa kuelezea umuhimu wa bahari, baadhi ya wadau wametoa maoni mbalimbali akiwemo Katibu wa wavuvi eneo la Msasani [KIWAM],Hujeje Mamboleo amesema kuwa joto baharini limeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokanan na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wanadamu ikiwemo kutupia vitu baharini.
‘’Tunapokuwa baharini kwa sasa takataka ni nyingi, mifuko ya sabuni ya unga, vifungashio vya ice cream, pempasi za watoto na wakubwa zimekuwa kero.
Mashine za boti zinazimika mara kwa mara kutokana na kunasa kwenye hizi pempasi, zinakuwa nyingi na watu hawazizingatii kuziondoa zaidi wanaondoa zile chupa tu ambazo zinaenda kuuzwa, tunaomba wadau waliangalie hili.’’ Amesema Hujeje,
Na kuongeza kuwa, watu wamekuwa wakipata mzio kwa kula samaki, hali hiyo inasababishwa kwa takataka za hospitali zinazoingia baharini hivyo jamii ichukue hatua.
‘’Takataka za hospitali zimekuwa kero kubwa, watu wanapaswa kuchukua hatua kwa kudhibiti hii hali. Vitu hivi vinapoingia bahari samaki wanaweza kuzalia mayai yao humo na baadae samaki hao wanabeba magonjwa ambayo ukija kula samaki unapata madhara ikiwemo mzio, tuchukue hatua kulinda bahari.
Aidha, amesema endapo bahari itaendelea kuharibiwa kuna uwezekano wa Visiwa vikakauka na kubakia milima na misitu mikubwa.
Kwa upande Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wamezishukuru taasisi zilizoandaa tukio hilo la siku ya bahari kwani wamewakutanisha watu muhimu wakiwemo wavuvi ambao ni watumiaji wakuu wa bahari.
‘’Kama Mabalozi, tumesikia na kupokea katika hii kwani tutaenda kufanyia kazi maoni yote yaliyotolewa hapa.
Tutaenda mpatia Waziri Jafo kuhusu maoni ya wadau.
"Safari yetu inazidi kuwa nzuri kutokana na wadau wetu kupitia bahari hivyo tuendelee kulinda bahari kwa manufaa kiuchumi’’. Amesema Grit.
Nae, Baraka Machumu mshawishi na mchechemuzi wa mitandao ya Kijamii kutoka Jukwaa la Mabadiliko ya tabianchi [Forum CC],amesema takwimu zinaonesha watu zaidi ya bilioni tatu wanategemea bahari hivyo ameomba kuhakikisha wanalinda bahari hiyo.
‘’Tunashukuru sasa hivi bahari ni ajenda. Hata Forum cc tulipokuwa tunaanza nchini mabadiliko ya tabianchi haikuwa ajenda, lakini sasa ni ajenda kuu duniani kote. Bahari inayo uwezo wa kunyonya hewa chafu duniani kwa asilimia 30, hivyo ni kitu kikubwa sana kwa dunia kuendelea kuilinda’’ amesema Machumu.
Aidha, amesema kuwa kina cha bahari kuongezeka ni mabadiliko ya tabia nchi lakini pia mabadiliko mengine ambapo pia binadamu wanachangia katika hali hiyo.’’ Amemalizia Machumu.
Wadau wengine walioshiriki katika maadhimisho hayo ni pamoja na Mashirika ya Africa Youth Transformation, Tanzania Youth Association, na wengine wengi ikiwemo jamii za ulinzi wa bahari wa maeneo mbalimbali nchini.
Post a Comment