RC TABORA AWAONYA WENYE VIWANDA BUBU VYA KUTENGENEZA MIFUKO YA PLASTIKI
Na Lubango Mleka, Igunga
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amepiga marufuku na kuwaonya wafanyabiashara na wawekezaji wenye viwanda bubu vya kutengeneza mifuko ya Plastiki iliyopigwa marufuku nchini.
Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya mazingira Duniani yanayofanyika kila mwaka Juni 5, ambapo kwa mkoa wa Tabora yamefanyika wilaya ya Igunga katika viwanja vya Sabasaba, amewataka wananchi, wafanyabiashara na wenyeviwanda bubu vya kutengeneza mifuko ya Plastiki iliyopigwa marufuku na serikali kuacha kuitumia na kuzalisha mifuko hiyo kwani imeonekana kuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani akipewa mti kwa ajili ya kuupanda katika viwanja vya Sabasaba Wilaya Igunga katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya mazingira Duniani.
" Ndugu Wananchi siku ya mazingira Duniani ni siku ya umoja wa mataifa kuwaelimisha na kuwahimiza watu duniani kote kuchukua hatua katika kuyatunza na kulinda mazingira.
" Nchi zina mipaka lakini mazingira hayana mipaka, napenda kuwakumbusha kaulimbiu ya siku ya Mazingira Duniani inayosema masuluhisho kwa uchafuzi wa plastiki au Komesha Uchafuzi wa Plastiki (Beat Plastic Pollution)," amesema Balozi Dkt Buriani.
Anasema kuwa, zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka hapa Duniani na nusu yake hutumika mara moja tu na kutupwa na kati ya hizo ni asilimia 10 tu hurejeshwa tena kwa matumizi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora akihutubia wananchi wa Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora katika kilele cha wiki ya mazingira Duniani yanayofanyika kimkoa wilayani Igunga katika viwanja vya Sabasaba.
Mkuu huyo wa mkoa amesema vipande vidogovigogo vya plastiki huweza kupenya kwenye vyakula tunavyokula, maji tunayokunywa na kwenye hewa tunayoivuta na kusababisha matatizo katika afya zetu.
" Naomba tuadhimishe siku ya mazingira duniani kwa vitendo, tukifanya usafi na kuondoa taka zote ngumu na hasa za plastiki, tukitumia nishati mbadala mfano Solar na gesi, majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo na kuwa na mpango kabambe wa hifadhi ya mazingira.
"Ni marufuku kwa viwanda bubu vinavyotengeneza mifuko ya plastiki katika mkoa wa Tabora, kwa yoyote atakayebainika kutengeneza, kutumia au kuingiza mifuko hii hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni kufikishwa Mahakamani au kupigwa faini," akisema Balozi Dkt Buriani.
Kwa upande wake afisa mazingira mkoa wa Tabora Abrahaman Mdeme amesema kuwa, ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Tabora kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 mkoa wa Tabora ulikuwa na idadi ya wakazi 2,291,622.
Katapila likiondoa dampo lisilo rasmi katika viwanja vya Sabasaba ambalo lilianzishwa na wananchi baada ya kukosekana kwa wazoataka, hivyo Serikali imeliondoa na kuchonga barabara ikiwa ni jitihada za kuendelea kuuweka mjini wa Igunga kuwa safi.
Amesema hio ni ongezeko la watu takribani 1,100,056 ndani ya miaka kumi 2021-2022 na linaenda sambamba na uharibifu wa mazingira unaosababibishwa na shughuli nyingi za kibinadamu.
" Taarifa na takwimu mbalimbali zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuwa kiwango cha ukataji wa misitu kwa mwaka nchini kinakadiriwa kuwa takribani hekta 372,816, kulingana na taarifa ya NAFORMA ya mwaka 2015.
"Makadirio ya karibuni ya mwaka 2018 kutoka kituo cha Taifa cha utafiti wa hewa ukaa (NCMC) yanaonesha uharibifu wa misitu kwa mwaka nchini umeongezeka na kufikia takribani hekta 469,420," amesema Mdeme.
Ameongeza kusema kuwa, uharibifu huo unatokana na mambo mbalimbali ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya mbao, fito na nguzo kwa ajili ya ujenzi, kuni kwa ajili ya ukusanyaji wa tumbaku na kupikia majumbani,
"Pia makaa kwa ajili ya kupikia na ufyekaji wa misitu kwa ajili ya upanuzi wa mashamba, maeneo ya makazi na maendeleo, haya yote ni mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka kwa jinsi wananchi wanavyoongezeka.
Amesema kuwa zipo jitihada wanazochukua kukabiliana na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kwa mfano Halmashauri ya wilaya ya Igunga na Urambo zimeunda vikundi vya wajasiriamali vya uzoaji taka.
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuna malori mawili ya uzoaji taka, kuwepo kwa wajasiriamali wanaorejeleza matumizi ya vyuma chakavu na chupa za plasiki.
Pia kuamasisha matumizi ya mkaa mbadala na kuwa na wadau wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, kuanzishwa kwa hifadhi za jamii nane katika vijiji 12 kupimwa na kuandaliwa mpango wa matumizi ya sheria ndogo za usimamizi.
Vilevile kuanzishwa kwa hifadhi mbili za Taifa za mto Ugala na Kigosi, kuanzishwa kwa viwanda vinne vya uchakatiji mazao ya nyuki, kuandaliwa kwa mpango bora wa matumizi ya aridhi na kuhimiza upandaji wa miti kufikia lengo la taifa.
Kwa Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 50 ya siku ya mazingira Duniani, baada ya kuanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1972 na itaadhimishwa katika Taifa la Côte d'Ivoire wakishirikiana na Nchi ya Uholanzi .
Côte d'Ivoire inaongoza katika Afrika katika kampeni za kupigana na uchafuzi wa plastiki na nchi ya Uholanzi inayongoza katika kurejeleza taka za Plastiki kutumika tena, ambapo kwa Tanzania yamefanyia mkoani Dodoma.
Post a Comment