JOYCE SOKOMBI: JICHO LA TANZANIA LINA MALENGO MAZURI KWA JAMII
>> Asema Shirika la Jicho la Tanzania limejipanga kuzifikia jamii zinazoishi porini
>> Lengo kuwapa elimu ya kufanya biashara ya matunda pori
>>Asema matunda pori yana faida kibiashara na ni tiba
>>Sokombi ni mfanyabiashara wa matango pori nchini Ujerumani na Uingereza
Na Dinna Maningo, Mara
MFANYABIASHARA na aliyewahi kuwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara, ambaye pia ni Mweka Hazina wa Jicho la Tanzania Organization Taifa, Joyce Sokombi amesema Shirika limejipanga kuzifikia jamii zinazoishi porini zinazokula matunda pori.
Akizungumza na DIMA Online amesema lengo la kuzifikia jamii hizo ni kupata fursa kubaini aina za matunda pori yanayoliwa na jamii hizo na yanayotumika kama dawa ya kutibu magonjwa.
Amesema baada ya kutambua matunda hayo Jicho la Tanzania Organization watatoa elimu kwa jamii hizo ili kutumia fursa hiyo kufanya biashara ya matunda pori ili kujiingizia kipato.
Sokombi ambaye ni mfanyabiashara wa biadhaa mbalimbali za matunda yakiwemo matango pori anayesafirisha kwenda kuuza nchi ya Ujerumani na Uingereza amesema matunda pori yana faida kibiashara na ni tiba ya mwili.
"Jicho la Tanzania Organization lina lengo zuri katika jamii zetu, tutafika katika jamii inayokula matunda pori kuona aina ya matunda wanayokula na tiba zake ili tuelimishe jamii zingine kuona umuhimu wa matunda pori.
"Wananchi wakishaona umuhimu watajihusisha na biashara za matunda pori hivyo wataweza kuvuna matunda kwa kushirikiana na jamii zinazoishi maporini kisha kufanya biashara ya matunda ili kijipatia kipato." Amesema Joyce.
Joyce amesema matunda pori yana faida hivyo ni vyema watanzania wakatumia fursa hiyo kujikuza kiuchumi badala ya kuyaona na kuyapuuza.
"Watu wakiyaona matunda pori wanaona ya kazi gani lakini matunda pori ni mazuri na yana faida sana na kubwa katika jamii yetu hasa tukijua maana halisi ya matunda.
"Mfano mdogo tu enzi ya mababu zetu mtu alikuwa akiumwa huwezi kukuta foleni hospitali, unasikia mtu anakwambia chukua tango pori kula unapona, au amepungukiwa damu unaambiwa chukua ukwaju tengeneza juisi kunywa unapona, kuna viazi Pori vina faida kubwa mwilini.
"Mimi nafanya biashara ya matango pori nasafirisha kwenda nje ya nchi, yana faida kubwa mwilini yanatibu kisukari, yanasafisha njia za haja ndogo, watu wenye matatizo ya presha na magonjwa mengine.
Ameongeza "Zamani nilikuwa nikienda sokoni naona wazungu wananunua matango pori nikawa sielewi, siku moja nikajaribu kununua nikidhani labda ni kiungo, nilivyouliza wakasema unaweza kufanya juisi au kutafuna japo ni machungu lakini watu wanakula.
" Ni vitu ambavyo tunavipuuza lakini vina faida kubwa sana na sisi tunachukua tunapeleka nje tunaenda kuneemesha watu wa nje kwenda kulinda afya zao wakati sisi watanzania au waafrika tunazidi kuporomoka kwenye suala la afya" amesema Joyce.
Amesema kupitia Jicho la Tanzania watapita kwenye mikoa, wilaya, vijiji na Mitaa kuhamasisha watu namna ya kutumia matunda pori kujipatia kipato na kiafya.
Baadhi ya Viongozi wa Jicho la Tanzania Organization wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufika ofisi ya mkuu wa Tabora kwa mazungumzo
" Matunda pori yanatoka Tanzania yanapelekwa nje ya nchi, kule wanayasaga kwenye mashine yanakuwa unga unaongezewa thamani na kuwa tiba.
Amewaomba watanzania kuthamini vitu vyao vikiwemo vile vilivyoanzishwa na mababu ambavyo vinaliwa na havina sumu kwani vina faida kwenye mwili wa binadamu na kibiashara.
>> Jicho la Tanzania Organization (JTO) ni Shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu jijini Dodoma, linalounganisha watu kutoka katika mikoa mbalimbali ndani ya Tanzania Bara na Zanzibar bila kujali Itikadi za kidini, kabila na vyama vya kisiasa kwa lengo la kuweka nguvu pamoja katika kufanikisha masuala ya kijamii.
Shirika hilo pamoja na majukumu mengine limedhamilia kutoa elimu ya umuhimu wa wananchi kuzitumia fursa za rasilimali zilizosaulika ili kujipatia kipato na ajira.
Post a Comment