HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI YAWAONDOA HOFU WANANCHI KUHUSU BANDARI YA TANGA

>>Waliovujisha nyaraka za siri za Serikali kusakwa na kuchukuliwa hatua

Na Boniface Gideon, Tanga

SERIKALI imesema Bandari ya Tanga haipo kwenye mpango wa kutafutiwa wawekezaji wa ndani au nje kuwekeza kutokana na kujimudu kiutendaji hivyo wananchi wa mkoa wa Tanga wasiwe na wasiwasi.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa wakati akizungumza na Watumishi wa Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi na Menejimenti za Taasisi za Wizara hiyo kwenye kikao kazi cha siku tatu kilichofanyika mkoani Tanga.

     Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza

Waziri huyo amewaondoa hofu wananchi kutokana na sakata la Bandari ya Dar es Salaam kuonekana kuwa gumzo hasa kwenye mitandao ya kijamii huku wakazi wa mkoa wa Tanga wakihoji nini hatma ya Bandari ya Tanga baada ya kufanyiwa maboresho makubwa ikiwamo uchimbaji wa kina cha Bahari, ujenzi wa magati pamoja na ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kupakua na upakiaji wa mizigo Bandarini hapo.

"Bandari ya Tanga haipo kwenye mpango wa kutafutiwa mwekezaji kwakuwa haina changamoto, tulichokifanya nikuifanyia maboresho makubwa na tutaleta mitambo mingine ya kisasa zaidi ili iwe na ufanisi mkubwa zaidi ya hapa kwahiyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya hilo" amesisitiza prof.Mbarawa

Amesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam imetafutiwa mwekezaji kwa magati mawili kati ya 12 ili kuongeza Teknolojia kubwa zaidi ya utendaji kazi Bandarini hapo.


"Kampuni tuliyoingia nayo mkataba ndio kampuni kubwa Duniani na imewekeza zaidi ya nchi 30 kwahiyo jamii isipotoshwe juu ya hilo " amesisitiza Mbarawa.

Pia Waziri Mbarawa amewatahadharisha Watumishi wa Umma kuzingatia Maadili ya kazi zao na kujiepusha na vitendo visivyofaa ikiwamo uvujishaji wa siri za Serikali.

Amesema kwamba wote waliohusika na uvujishaji wa siri za Serikali watatafutwa na kuchukulia hatua huku akionekana kushangaa mkataba huo kusambazwa sasa hivi wakati ni wamuda mrefu.

Aidha akizungumzia sakata la nyaraka za siri za mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya DP zilizozagaa mitandaoni amesema;

"Watumishi jiepusheni na vitendo vya kuvujisha Siri za Serikali, ukivujisha ni lazima ukamatwe kwakuwa Teknolojia ni kubwa sana, mpo hapa kwaajili ya kueleza changamoto zenu fungukeni na kueleza changamoto zenu msiogope ili tukitoka hapa kila mmoja wetu akatekeleze majukumu yake vizuri" amesema Mbarawa.

Kufuatia kauli ya Serikali juu ya Bandari ya Tanga kutobinafsishwa kwa mwekezaji baadhi ya wakazi wa Tanga wameishukuru Serikali kwakutomweka mwekezaji.

" Sisi kama wananchi hususani wa maeneo haya ya Bandari tulikuwa na wasiwasi juu ya Bandari yetu na vibarua vyetu hapa Bandarini maana tunayaona kwenye mitandao tu juu ya Bandari ya Dar es Salaam"Amesema Hassan Jamal mkazi wa Tanga Mjini.


No comments