ALIYEKUWA MEYA TANGA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA
>>Adaiwa kughushi nyaraka kujipatia Tsh.Milioni 5 fedha za mikopo ya vijana, wanawake na makundi ya walemavu
Na Boniface Gideon, Tanga
ALIYEKUWA Mustahiki Meya wa Jiji la Tanga Mustafa Seleboss na watu wengine watano wamepandishwa kizimbani kwa makosa 4 yakiwamo ya kughushi barua ya maombi ya kufungua akaunti ya Benki ya NMB kwaajili ya mkopo wa kikundi.
Pia wanatuhumiwa kwa wizi wa Tsh.Milioni 5 ya Halmashauri ya jiji la Tanga , matumizi mabaya ya madaraka ya umma pamoja na kuisababisha hasara Halmashauri ya Jiji la Tanga .
Wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Omari Ali Salehe, Amina Rajab Mbwana, Pilly Salum Shomari, Mwajuma Sabdallah Mwaimu na Mwanbakondo Kichui Mwalimu ambao wamefikishwa mahakamani hapo Juni, 13, 2023.
Imedaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Joseph Mulebya ,mbele ya Hakimu wa mahakama ya ya hakimu Mkazi Suniva Joseph Mwajombe kuwa kati ya Mei, 28, 2019 na Mei 2022 washtakiwa
walifanya makosa hayo kwa makusudi hali wakijua kuwa kufanya hivyo
ni kosa kisheria.
Ameendelea kudai kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja walighushi nyaraka
mbalimbali kwa ajili ya kujipatia Tsh. Milioni 5 ambazo ni fedha za umma
zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa ajili ya mikopo ya
asilimia 10 za vijana, wanawake na makundi ya wenye ulemavu.
Mwendesha mashtaka huyo
amesema kuwa Seleboss anashtakiwa
kwa maoksa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa fedha za umma kinyume na sheria ya matumizi ya madaraka.
Washtakiwa wengine wamefikishwa mahakamani hapo kwa madai ya
kuisababishi hasara ya Tsh. Milioni 5 Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Kesi hiyo Na. 7 ya mwaka 2023 imeahirishwa hadi Juni, 20 mwaka huu
kwa ajili ya kutajwa tena ambapo washtakiwa wote wamerejeshwa rumande baada ya kukosa wadhamini.
Post a Comment