TAMASHA LA MUZIKI WA CIGOGO KUFANYIKA CHAMWINO
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TAMASHA la 14 la Muziki wa Cigogo linatarajia kufanyika Julai 22 na 23 mwaka huu katika Kijiji cha Chamwino Ikulu, Mkoani Dodoma, huku vikundi 40 vikitarajiwa kutoa burudani.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sanaa Chamwino (CAC), Frank Mgimwa amesema tayari maandalizi yanaendelea.
"CAC tumejiandaa vyema katika kukuza na kuendeleza utamaduni wa mtanzania kupitia muziki wa Cigogo wa Kabila la Wagogo ambapo mwaka huu kauli mbiu ni "Kuza Sanaa, Maadili kwanza". Vikundi vitawasilisha jumbe mbalimbali na kuonesha umahiri wao kupitia ngoma na nyimbo.
Vikundi 40, kati ya 34 vinatoka mkoa wa Dodoma na vingine 6 vinatoka nje ya Dodoma katika mkoa wa Iringa, Singida na Zanzibar" amesema Frank Mgimwa.
Amevitaja baadhi ya vikundi hivyo ni pamoja na Nyati, Faru, Swala, Nyota Lamali, Nyerere na Ufunuo, Muhubiri, Afri kabati, Muungano, Ilula Orphanage Cultural group.
Amesema kutakuwa na Utalii wa kiutamaduni wa zao la Zabibu ambapo wageni watatembelea mashamba ya zao hilo na kupata fursa ya kula na kuonja Zabibu (wine test).
"Siku moja kabla ya Tamasha, yaani Julai 21, mwaka huu, tutakuwa na Utalii wa utamaduni wa zao la zabibu.
Wageni mbalimbali wa ndani na nje tutawatembeza kwenye mashamba hayo ya zabibu na kutakuwa na vyakula vya asili ya kabilaa Wagogo". Amesema Frank Mgimwa.
Aidha, amesema wakati wa tamasha hilo, kutakuwa na warsha na Makongamano pamoja na Hadithi simulizi na mengine mengi.
Frank Mgimwa amezitaja baadhi ya Taasisi zilizopata mwaliko kwenye tamasha hilo ni pamoja na Taasisi ya Sanaa Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, COSOTA, Bodi ya Filamu, Dane wine, Uswazi Born Talented, pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, BASATA na Nafasi Art Space.
Wadhamini wa tamasha hilo mwaka huu ni Ubalozi wa Uswizi Tanzania na Chamwino Connect USA.
Post a Comment