TAWA YAWAONYA WANAOJIHUSISHA NA UJANGILI
Na Boniface Gideon, Tanga
MAMLAKA ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania (TAWA) imewaonya watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili wa wanyama pori katika hifadhi na mbuga za wanyama nchini kuacha kazi hiyo mara moja kwakuwa mamlaka hiyo kwakushirikiana na mamlaka nyengine wapo imara na kwamba sheria ya sasa ni kali.
Aidha imewataka wananchi waliopo karibu na hifadhi za wanyama kujiepusha na vitendo vyovyote vya ujangili wa wanyama katika hifadhi na maeneo mbalimbali nchini na kwamba matukio ya ujangiri kwa sasa yamepungua.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania (TAWA) Proches Rongoma wakati wa maonesho ya 10 ya Biashara na Utalii yanayofanyika mkoani Tanga kila mwaka.
Afisa Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania (TAWA) Proches Rongoma
Amesema kuwa hivi karibuni Waziri wa Mali asili na Utalii Mohammed Mchengerwa alizindua mpango kabambe utakaosaidia kwa kiasi kikubwa kuwadhibiti wale wote waliokuwa wakikiuka sheria za kuuwa wanyama pori bila kibali maalum.
"Suala au kitendo chochote cha kuuchukua mali ya wanyama pori bila kibali huo ni ujangiri na ujangili upo wa aina tofauti upo wa kibiashara na wa chakula, kuna watu wanaoua wanyama kwa ajili ya chakula na kwaajili ya kufanya biashara.
" Mamlaka ya wanyama pori Tanzania inapenda kuwasihi sana watanzania wajue kwamba wao ndio wahifadhi wa kwanza wa wanyama pori wa nchi hii.
"Serikali yetu imeleta mfumo wa kupatikana kwa nyama za wanayama pori katika bucha kwahiyo hakuna sababu ya kusema mtu anawinda ili apate kitoweo, tuna mfumo unaokubalika ambao unakuruhusu vinginevyo utakutwa na mkono wa sheria hivyo ni vyema watanzania wajiepushe na ujangili wa aina yeyote ile" amesema Rongoma
Pamoja na hayo amewataka wananchi wanaoishi karibu na hifadhi mbalimbali hapa nchini kutoa taarifa mamlaka husika na kujiepusha kujichukulia hatua mkononi pale wanyama pori wanapokuwa wamevamia katika maeneo ya shughuli za kibinadamu.
"Yapo baadhi ya maeneo yenye changamoto za wanyama pori kutoka hifadhi mbalimbali kutoka nje ya hifadhi na kwenda kuvamia maeneo ya shughuli za kibinadamu kama kilimo na makazi.
"Ninachoomba wananchi mnapoona wanyama pori msiwasogelee karibu na msichukue hatua mkononi ni hatari Sana nivyema mkatoa taarifa kwenye Mamlaka husika" amesisitiza Rongoma.
Awali akizungumza, afisa mhifadhi daraja la pili kutoka mamlaka hiyo Veronica Mollel amewasisitiza na kuwahimiza watanzania kuendelea kufanya utalii wa ndani katika hifadhi mbalimbali zilizopo hapa nchini ili kujionea vivutio na kujifunza amali mbalimbali zilizopo.
Amesema kuwa kuzinduliwa kwa Royal Tour iliuofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumekuwa na muamko mkubwa wa watalii si tu wageni kutoka mataifa mbalimbali bali hata watanzania wamehamasika na kujitokeza kujionea vivutio huku ushiriki wa wanawake katika sekta mbalimbali ukiongezeka.
"Tanzania tuna vivutio mbalimbali ushiriki wa wanawake katika sekta mbalimbali za utalii umekuwa ni mkubwa wapo kwenye doria, kuongoza watalii niwasihi watanzania wote kuwa mabalozi wa rasilimali zetu za Wanyama pori" amesema Mollel.
Maonyesho ya biashara na utalii ambayo hufanyika kila mwaka mkoani Tanga yakishitikisha makampuni, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali mwaka huu 2023 yamebebwa na kauli mbiu ya "Kilimo, viwanda utalii na madini ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi".
Post a Comment