DC KAMINYOGE : UTOAJI CHAKULA CHENYE VIRUTUBISHO SHULENI NI MUHIMU
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAAFISA Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wametakiwa kuhakikisha chakula kinachotolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo yao vinakuwa na virutubisho ili kuondoa udumavu kwa watoto.
Pia Maafisa hao wametakiwa kuhakikisha kila shule ya Msingi na sekondari zilizoko kwenye maeneo yao zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema hayo Julai , 18, 2023 wakati wa kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe cha robo ya nne kwa Maafisa hao.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye miwani)akiongoza kikao Cha Kamati ya Lishe wilaya ya Maswa.
Amesema kuwa Watendaji wa Kata waangalie usalama na uhifadhi wa chakula kwani ni muhimu sana kwa usalama wa watoto hivyo wana wajibu wa kusimamia upelekaji wa chakula shuleni.
“Suala la utoaji wa chakula ni lazima na chakula hicho kinachotolewa lazima kiwe na virutubisho ilil kuondoa udumuvu kwa Watoto na hii itasaidia watoto kupata muda mzuri kuwa katika masomo yao”.
"Hata kama hatuwezi kutoa chakula Cha mchana ni vizuri Watoto hao wakanywa uji na unga wa kupikia uji huo ni lazima uongezwe virutubisho mbalimbali kama vile dagaa wakati wa kusaga unga huo,"amesema.
Pia amewasisitiza maafisa hao kufanya mikutano na wazazi wa wanafunzi katika maeneo hayo ili kueleza umuhimu wa kutoa chakula kwa wingi shuleni kwa ajili ya Watoto wao.
“Watendaji wa Kata niwaombe tusaidiane kuhimiza wazazi na walezi wa wanafunzi katika maeneo yenu umuhimu wa utoaji wa chakula shuleni na kitolewe kwa wingi,"alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa amesema kuwa wamewaagiza walimu wakuu wa hule za msingi na Wakuu wa shule za sekondari katika halmashauri hiyo kuhakikisha chakula kinachotolewa shuleni kwa wanafunzi kina virutubisho vya kutosha kwa ajili ya ustawi wa ukuaji wa mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akisisitiza jambo kwenye kikao Cha Kamati ya Lishe cha Wilaya hiyo.
Amesema kuwa chakula kinachokuwa na virutubisho vinamsaidia mtoto kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya vizuri kwenye mitihani yao shuleni.
"Halmashauri tumewaagiza walimu wakuu na wakuu wa shule zetu zote zilizoko hapa wilayani kwetu kutoa chakula cha wanafunzi chenye virutubisho na Moja ya faida yake ni uwezo wa mtoto kufikiri na kufanya vizuri kwenye Mitihani yake shuleni,"amesema.
Afisa Lishe wilaya ya Maswa,Abel Gyunda amesema kuwa ni vizuri unga unaoandaliwa kwa ajili ya uji wa wanafunzi shuleni ukazingatia mchanganyiko wa kitaalam kwani tayari katika wilaya hiyo kuna mashine za kusaga unga kwa mchanganyiko unaozingatia wa virutubisho kwa ajili ya matumizi ya watoto.
"Kwa sasa hapa mjini Maswa tuna mjasiliamali ambaye ana mashine ya kusaga unga kwa kuchanganya ili kuongeza virutubisho kwenye uji wa watoto maana hata huu mchanganyiko wa virutubisho kwenye unga ni vizuri ufanywe kitaalam kwa manufaa ya kuboresha Afya za Watoto wetu,"amesema.
Baadhi wa Wajumbe wa Kamati ya Lishe wakiwemo Maafisa Watendaji wa Kata zilizoko katika wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao Cha Kamati ya Lishe wilaya hiyo.
Post a Comment