MADAKTARI BINGWA WATUA IGUNGA, WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KUFANYIWA UCHUNGUZI, MATIBABU
Na Lubango Mleka, Igunga
WANANCHI Wilayani Igunga Mkoani Tabora wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kliniki itakayotolewa na Madaktari Bingwa kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na hospitali ya Rufaa ya Nkinga.
Madaktari hao wapo katika hospitali ya wilaya ya Igunga kwa siku tano ili kutoa huduma ya uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu wananchi.
Magonjwa ambayo yatachunguzwa na kupatiwa tiba ni upasuaji, magonjwa ya ndani, magonjwa ya kinamama na uzazi, macho, masikio, pua na koo ambapo madaktari hao bingwa watatoa huduma hiyo kuanzia Juni 24,2023 hadi Juni 28,2023.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi hospitali ya wilaya ya Igunga Melchedes Byabato Magongo amesema kuwa walibaini changamoto yao na kugundua kuwa wanauhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa.
Amesema kutokana hivyo wakaanzisha ushirikiano na hospitali zenye madaktari bingwa watakao weza kutoa huduma hizo katika hospitali ya wilaya ya Igunga ambapo wananchi wamekuwa wakizifuata katika wilaya na mikoa ya mbali.
"Tulifanya mawasiliano na wenzetu wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma na hospitali ya Rufaa Nkinga ambayo ni ya binafsi iliyopo wilayani Igunga na tumefanikiwa na wamefika na leo wameanza kutoa huduma hizi za kibingwa kwa awamu ya kwanza na watatoa huduma hizi kwa siku tano yaani kuanzia Juni 24,2023 hadi Juni 28,2023," alisema Magongo.
"Awamu ya kwanza ambayo tumeona kuanza nayo ni huduma kutoka kwa madaktari bingwa katika vitengo vya madaktari wa upasuaji, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, magonjwa ya kina mama na uzazi, madaktari bingwa wa Macho, madaktari wa masikio, Pua na Koo, huduma hizi ndizo tumeanza nazo."
Aidha, amebainisha kuwa kwa siku ya kwanza muitikio wa wananchi kujitokeza kupima, kuchunguza na kupatiwa matibabu ya kiafya umekuwa mkubwa sana hivyo amewataka wananchi wilayani Igunga na maeneo jirani kujitokeza ili kuweza kuonana na madaktari hao bingwa.
Kwa upande wake daktari kiongozi na bingwa wa magonjwa ya kina Mama na uzazi kutoka hospitali ya Rufaa ya Nkinga Gilbert Ng'wamkai, amesema kuwa lengo kuu la kufika katika hospitali ya wilaya ya Igunga ni kuboresha mahusiano mazuri waliyonayo kwa lengo la kusaidia wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na kuwataka kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupatiwa huduma za matibabu hayo.
"Huduma hizi hazipo kibiashara, tupo hapa kuwasaidia wananchi wa Igunga na maeneo ya jirani, kwa hiyo tunawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kupata fursa hii ya matibabu bora na kwa urahisi zaidi," amesema Ng' wamkai.
Naye Happy Nyabukika Diwani viti maalumu Kata ya Igunga ni mmoja wa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma ya matibabu ya kibingwa, amesema kuwa watu wengi wilayani hapa wanapata tabu sana kwenda kupata huduma ya matibabu ya kibingwa hospitali zingine au katika mikoa ya mbali.
Amesema asilimia kubwa ya wananchi hushindwa kumudu gharama za matibabu, nauli au malazi, hivyo ameiomba Serikali kupita Wizara ya Afya kuipatia hospitali ya wilaya ya Igunga madaktari bingwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa zaidi ili kuwasaidia wananchi wenyevipato vya chini kupatiwa matibabu ya kibingwa kwa ukaribu.
" Mimi ni mwanafunzi wa Sekondari ya St. Marigaret Maria alakok, nimekuja kupima Macho, nashukuru huduma ni nzuri nimehudumiwa kwa wakati ninaomba watufikie katika shule zetu ili kutupatia huduma hizi za kibingwa, kwani wanafunzi wengi tuna magonjwa mbalimbali kwa kutufikia watakuwa wametusaidia kutambua na kuyatibu magonjwa yetu mapema," amesema Sara Ibrahim.
Huku Anthony Salumu akimshukuru Mkuu wa wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, Uongozi wa hospitali ya wilaya ya Igunga, Madaktari wote bingwa na wauguzi kwa kujitoa na kufanikisha jambo hili la kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.
Pia ameomba uongozi kuongeza muda zaidi kwani itasaidia kuwafikia wananchi wengi hasa wa vijijini ambao kwa namna moja ama nyingine hawajapata taarifa ya ujio wa madaktari hao bingwa.
Post a Comment