HEADER AD

HEADER AD

MASHINDANO YA MPIRA WA MIGUU 'CHATO SAMIA CUP' YAZINDULIWA

Na Daniel Limbe, Chato

KATIKA kuenzi kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya ya Chato mkoani Geita chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya sita, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Hamis Mwijuma (Mwana FA) amezindua rasmi mashindano ya mpira wa miguu ya 'Chato Samia Cup' yatakayosaidia kuibua vipaji vya soka kwa vijana.

Mashindano hayo ni ya kwanza kulindima kwenye wilaya hiyo tangu Rais Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania,Hayati Dk. John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia kwa tatizo la moyo kisha mazishi yake kufanyika nyumbani kwao Mlimani Rubambangwe wilayani humo.

Akizindua mashindano hayo ya mpira kwa niaba ya Naibu Waziri yaliyofanyika katika Kijiji cha Katemwa kata ya Muganza, Mkuu wa wilaya ya Bukombe,Said Nkumba amesema anatarajia kuona mashindano hayo yanaongeza chachu ya wananchi kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kujipatia maendeleo ya familia na Serikali kwa ujumla.

    Mgeni rasmi Said Nkumba, akisalimiana na wachezaji wa mpira wa pete

Hata hivyo Nkumba ameonesha kuvutiwa na ubunifu mkubwa uliofanywa na mkuu wa wilaya ya Chato,kwa kuwaunganisha wananchi pamoja kupitia michezo mbalimbali sambamba kutumia fursa hiyo kuenzi kazi kubwa zinazotekelezwa na rais Samia kwenye wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Deusdedith Katwale,amesema amelazimika kutumia michezo hiyo kuenzi jitihada kubwa za kimaendeleo zinazotekelezwa na Rais Samia kupitia sekta ya Miundombinu, afya, kilimo, mifugo, uvuvi na uwekezaji jambo ambalo limezidi kuipaisha wilaya hiyo kiuchumi.

Kadhalika Katwale amesema mashindano hayo yatafanyika kwa takribani mwezi mmoja na kwamba watakaoibuka washindi watapewa zawadi mbalimbali ikiwemo fedha,mipira na jezi.

    Mkuu wa wilaya ya Chato,Mhandisi Deusdedith Katwale,akisalimiana na wananchi wa kata ya Muganza

Mbali na mpira wa miguu, ufunguzi huo umeambatana na mchezo wa mpira wa pete kwa wanawake, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kukimbia na kijiko chenye ndimu, kucheza bao pamoja na drafti.

Akizungumza na DIMA Online Katibu Mkuu wa Chama cha mpira wa miguu wilaya ya Chato(CDFA), Wilfred Machugu, amesema mashindano hayo yamezingatia sheria, taratibu na kanuni zote za michezo jambo ambalo limeshawishi chama hicho kutoa kibali cha kuendesha mchezo huo.

    Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Mandia Kihiyo,akimkabidhi zawadi ya kuku mmoja wa washiriki wa shindano la kukimbiza ndege huyo.

  Baadhi ya wakazi wa Muganza wakimpokea mgeni rasmi kwa bango lenye kuashiria mashindano ya Chato Samia Cup.
      Mkuu wa wilaya ya Bukombe,Said Nkumba,akisalimiana na wachezaji wa timu ya Muganza

No comments