MBUNGE NDAKI AJIVUNIA MAFANIKIO JIMBO LA MASWA MAGHARIBI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki mkoani Simiyu amesema amefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika Jimbo hilo kwenye sekta za afya, elimu, maji na barabara.
Mbunge Ndaki ambaye yuko kwenye ziara katika jimbo hilo amesema hayo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata ya Seng'wa na Kata ya Masela wakati akihutubia mikutano hadhara na kukagua miradi mbalimbali katika sekta ya elimu,afya,maji na miundo mbinu ya barabara.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akisisitiza jambo kwenye Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwasayi kilichoko wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Amesema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili tangu achaguliwe kuwa mbunge wa Jimbo hilo Serikalini imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imeleta fedha hizo katika jimbo hilo kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari,Vituo vya afya, Miradi ya Maji na miundo mbalimbali ya barabara.
"Kwa kipindi huku cha miaka miwili Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Jimbo letu hivyo hatuna budi kumshukuru sana mheshimiwa Rais,"amesema Mashimba.
Amesema kuwa katika sekta ya Afya wameweza kuwa na vituo vya Afya vitano ambavyo vitawahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki(mwenye kipaza sauti)akihutubia kwenye Mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Masela.
"Kwa sasa tuna Vituo vya Afya vitano kwenye Jimbo letu ambavyo ni Mwasayi,Mwabayanda,Shishiyu,Badi na Malampaka kwa Jimbo letu ni lazima tujivunie maana kuna majinbo mengine wanakituo cha Afya kimoja tu,"alisema.
Amesema kuwa kwa sasa jimbo hilo barabara nyingi zimejengwa kutoka eneo moja kwenda jingine japo bado kuna changamoto kwa baadhi ya maeneo kuwa na barabara mbovu na kwamba atahakikisha nazo zinafanyiwa matengenezo ili ziweze kupitika kama zilivyo nyingine.
Mbunge Mashimba amesema kuwa katika miradi ya maji baadhi ya vijiji vilivyoko katika Jimbo hilo vinapata maji ya Ziwa Victoria kupita katika wilaya ya Kushapu mkoani Shinyanga .
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (kulia)akimtisha ndoo ya Maji mama mmoja katika Kijiji cha Mandela wilayani Maswa mkoani Simiyu baada ya Mradi wa maji kukamilika kijijini hapo.
"Katika mkoa wa Simiyu maji ya Ziwa Victoria ambayo ni safi na salama yanapatikana katika Jimbo hili kufuatia kukamilika kwa mradi wa maji Kijiji cha Seng'wa na sasa yanasambazwa katika Vijiji vya Mandela,Mwabomba na Mwanundi ambavyo vyote viko kwenye Kata ya Seng'wa hili ni jambo la kuishukuru sana serikali,"
“Kwa muda wote tangu mnichague mwaka 2020, nimekuwa na harakati za kusimamia na kuchochea utekelezwaji wa miradi ya maendeleo na hata ninyi ni mashahidi, maana mmekuwa mkishiriki kwa namna moja au nyingine katika kutekeleza miradi hiyo,” amesema.
Pia ameongeza kuwa katika jimbo hilo vijiji vyote na taasisi zote za serikali zimepatiwa huduma za nishati ya umeme ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku na sasa kila kitongoji kitapatiwa umeme.
Sehemu ya Wananchi wa Kijiji Cha Masela wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu waliojitokeza kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki(hayupo pichani).
Naye,Sitta Mashala ambaye ni Katibu wa Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Maswa amewaomba viongozi kuanzia ngazi ya tawi hadi Kata kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao.
"Kwa sasa kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa shule katika jimbo letu la Maswa Magharibi hivyo viongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika ngazi zote simamieni miradi hiyo mkishirikiana na wataalam wa serikali"amesema.
Post a Comment