HEADER AD

HEADER AD

SABABU ZA WANANCHI KUSEMA SERIKALI YA RORYA INATAKA KUWADHULUMU ARDHI



 >>>Wananchi wawaomba waandishi wa habari kupitia kalamu zao waandike malalamiko yao ili yafike Ikulu kwa Rais Samia.

>>>Wasema wao ni masikini hawana uwezo wa kufungua kesi kwani uendeshaji wa kesi ni gharama.

>>>Wasema suluhisho la mgogoro wao ni CCM na Rais Samia.

Na Dinna Maningo, Rorya

SIKU tatu zilizopita wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Koryo, wilaya ya Rorya mkoani Mara, wanaoishi jirani na shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm) waliandamana ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya.

Wananchi wakiwa wameandamana ofisi ya CCM Rorya.

Wananchi hao wanawake kwa wanaume walifika ofisi ya CCM wilaya ya Rorya kuilalamikia Serikali ya wilaya hiyo kuwa inataka kuwadhulumu ardhi katika zoezi la uthamini wa fidia linaoendelea katika vitongoji hivyo.

Hata hivyo, hawakufanikiwa kueleza kero zao baada ya kukuta milango ya ofisi ya Chama hicho ikiwa imefungwa kwa kufuli.

          
Kwanini wahofu Serikali kutaka kuwadhulumu ardhi?

Wameiambia DIMA Online  kwamba, chanzo cha kuandamana ni baada ya Serikali hiyo kutowatendea haki katika zoezi la uthamini wa fidia kutokana na kukiuka makubaliano baina ya Serikali na wananchi waishio jirani na shamba la mifugo.

Herinest Olala anasema kuwa, katika mkutano wa wananchi uliofanyika Julai, 16, 2023 ulihusisha Vijiji viwili Kijiji cha Omuga na Majengo.

Mkutano uliwashirikisha Wathamini, viongozi wa Serikali ngazi ya Tarafa, Kata, Serikali za Vijiji , wasimamizi wa shamba la mifugo kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na wananchi ambao walikubaliana kuwa ardhi itafanyiwa uthamini pamoja na mali zingine zilizo juu ya ardhi lakini imekuwa tofauti.

Herinest Olala

Imeelezwa kuwa Serikali iliwaeleza kuwa baada ya kufanyiwa uthamini wa ardhi na mali zao, watalipwa fidia na kisha kupisha maeneo hayo ili Serikali iendeleze miradi mbalimbali ambayo imepanga kuendeleza japo haikubainishwa wazi aina ipi ya miradi itakayowekezwa. 

"Tumeandamana hadi ofisi ya CCM wilaya kufahamu haya tunayofanyiwa na wathamini je CCM inaelewa? je imekubali ? na kama wanaelewa wajue sio tulichokubaliana. Warudi watuambie kwanini hawapimi ardhi? kibaya zaidi wanasema mwenye ekali moja au 8 au 9 na zinginezo zote kipimo ni sawa.

"Katika kikao hicho Viongozi wa Serikali walikuwa wanatupatia elimu juu ya uthamini, wakatuelimisha tukakubaliana nao. Walitueleza kuwa watafanya uthamini wa ardhi , nyumba na uthamini wa vile vilivyopo juu ya hiyo ardhi, kama vile makabuli, mimea mbalimbali.

"Cha kushagaza uthamini ulivyoanza Jumanne, Julai 25, 2023 imekuwa kinyume chake. Wanatuambia wanafanya uthamini vitu vilivyopo juu ya ardhi, nyumba yako,miche na vitu vingine ambavyo hata uhesabuji wake baadhi ya miche na nyumba zina baguliwa .

Herinest anasema kuwa Serikali kutofidia ardhi za wananchi hiyo ni dhuluma kwani baadhi ya watu wana ardhi ambayo haijaendelezwa, huitumia tu wakati wa msimu wa kilimo, msimu ukiisha inakuwa tupu na wengine huitumia kwa ajili ya malisho ya mifugo.

"Unapima nyumba na kuhesabu mali zilizo juu ya ardhi lakini ardhi hauhesabu je bila ardhi hivyo vitu vingewekwa wapi? watu wasipofanyiwa uthamini wa ardhi wataenda kujenga nyumba kwenye viwanja vya nani? huu ni uonevu unaofanywa na Serikali yetu.

Charles Laurent anasema" Serikali inataka kutuhamisha kibabe, nimezaliwa 1970 Kwenye eneo naloishi alafu eti uhame bila kufidiwa ardhi, wakati kwenye mkutano tuliongea vizuri, nina watoto 6 nina nyumba moja ya nyasi na slopu, miche kama 10 na migomba miwili, nikilipwa zitatosha kwenda kununua ardhi ?" anauliza.

Wanajeshi kuongozana na wathamini 

Wananchi wamelalamikia Kitendo cha wathamini kuongozana na Wanajeshi wanapopita kwenye miji ya watu kufanya uthamini na kusema Kitendo hicho kinawaweka katika hofu na kutokuwa huru kwani huwapa vitisho.

Chachiru Makiri mkazi wa Kitongoji cha Begi anasema" Tulikubaliana kuwa wakati wa zoezi la uthamini wenyeviti wa vitongoji na kijiji wawepo lakini haijafanyika, wathamini wanapita kwenye nyumba za watu wakiwa na Mtendaji wa Kata na wanatembea na Wanajeshi.

           Chachiru Makiri

"Mi navyojua kazi ya Wanajeshi ni walinzi wa nchi na mipaka ya nchi, pale kuna Wanajeshi. Hivi sisi ni Magaidi Al-Shaabab au Boko Haram! hadi uthamini usimamiwe na wanajeshi! wanaohusika na ulinzi na mali za raia ni Jeshi la Polisi , wanajeshi wanaingilia majukumu yasiyo yao.

" Kwa hali hiyo tumepata hofu tunatafakari kwamba wapo tayari kutunyang'anya ardhi kwa mabavu, tuna hofu sana.

Imeelezwa kuwa wathamini wanapopita kwenye nyumba za watu hata kama watu hawapo majumbani wao huendelea kufanya uthamini na kisha kuchora namba zenye rangi nyekundu kwenye nyumba.

"Wito wangu kwa Rais mama Samia Suluhu tunaomba utusikilize sisi wanyonge pale kuna yatima, wajane, wazee, walemavu, waghane, wapo ambao hawakubahatika kupata watoto,  Kaya masikini wasipolipwa ardhi wataenda kuishi wapi?.

" Mtu ana nyumba moja ya nyasi na mpapai mmoja wanasema huwezi kulipwa ardhi, je pesa hiyo itatosha akatafute eneo jingine ajenge nyumba? kama hawatathimini ardhi watuambie wanatupeleka wapi?!." Anasema Chachiru.

Wamwangukia Rais Samia

Angelina Gunze mkazi wa Kitongoji cha Begi anasema " Jamani nimefika hapa ninasikitika, mme wangu alininunulia ardhi ameshazeeka, aliniambia hii ardhi ndiyo itakusaidia kulisha watoto na huduma nyinginezo.




"Nashangaa leo hii wapimaji wanapita wananiambia kwamba ardhi hailipwi ila ni nyumba, miti na mimea , jamani pesa ya nyumba itanunua ardhi? ardhi yenyewe kununua ni bei kubwa.

"Jamani tunaomba Rais wetu Samia Suluhu atusaidie tumekwama mme wangu amezeeka saizi ni kama mtoto analelewa "anasema Angelina.

Deus Angulo mkazi wa Kitongoji cha kiwandani mwenye ulemavu wa viungo anasema kwamba Serikali imekuwa ikidai kuwa maeneo wanayoishi ni ya shamba la mifugo kwamba walivamia hivyo hawatalipwa ardhi isipokuwa mali zilizopo juu ya ardhi kwa madai kuwa ardhi hiyo ni ya serikali.

Deus Angulo
"Mababu zetu wamefia pale kwenye ardhi wamekaa tangu miaka ya 1800 wakazaa watoto nao wakaendelea kuishi hadi kizazi cha sasa, makabuli  yapo. Mimi nimezaliwa hapo sasa hivi nina zaidi ya miaka 60 alafu wanasema tumevamia.

"Kama ni hivyo watuoneshe wanakotupeleka au basi tupelekwe kwa mkuu wa wilaya tuishi pale aendelee kutulea mpaka siku atakapotupatia mahala pakuishi.

Deus anawaomba Waandishi wa Habari kupitia kalamu zao waandike malalamiko yao ili yafike Ikulu kwa Rais Samia awasaidie wapate haki zao kwani wao ni masikini hawana uwezo wa kuendesha kesi mahakamani kwakuwa ni gharama.

Angela George Adero anamwomba Rais Samia kama mwanamke mwenzake awasaide " Rais Samia wewe ni mwanamke mwenzetu na wewe unatulea. Tunaomba utusaidie tupate haki zetu.

Angela George Adero


"Serikali ya Rorya inatuonea, tunatishiwa tunaletewa wanajeshi, tuna hofu tumekuja hapa CCM tangu asubuhi ili kujua haki zetu tunaomba Chama chetu Tawala kitusaidie. Mama Samia wewe ni mama unaujua uchungu tusaidie" anasema Angela.

Scola Akola Osiong'o anasema"Mimi ni mjane nilifiwa mme akaniacha na watoto akaniachia ardhi, nina watoto, mmoja yupo chuo mwingine kidato cha tatu na mwingine darasa la saba.



"Mimi ndiyo nafanya vibarua watoto wale nalima shamba, nashangaa ardhi haifanyiwi uthamini. Nina nyumba mbili za nyasi zimezeeka, miti ninayo sita tunaambiwa tutahama, pesa ya kwenda kununua sehemu nyingine naitoa wapi? Rais Samia naomba usikie kilio chetu sisi wajane" anasema.
 
Marisela Nyaranda anayekadikiwa kuwa na miaka (90) hajawahi kubahatika kupata mtoto, aliolewa na mme wake Samsoni Nyaranda Ang'uro aliyefariki mwaka 1987.

               Marisela Nyaranda

Anasema yeye hana la kusema ila kama Serikali itambeba au kumzika jinsi alivyo sawa maana hana pakwenda. 

"Kwanza mi ni mzee naumwa ardhi ni ya mme wangu nikiondoka napelekwa wapi wakati mi sijawahi kupata mtoto hapa nasaidiwa huduma na wajukuu wa mke mwenzangu tunaeishi nae hapa.

Anasema mme wake aliacha wake wawili yeye na mke mwenzake Angelina Nyaranda mwenye watoto 8, wanaishi katika ardhi waliyoachiwa na mme wao.

Anasema baada ya kukaa muda mrefu bila kupata mtoto aliamua mdogo wake aolewe na mme wake ili aweze kumsaidia kazi na kumzalia mmewe watoto.

Angelina Nyaranda

"Sina baba wala mama wala watoto mdogo wangu nilimleta akaolewa na mme wangu kama ilivyo utamaduni wa mjaluo usipobahatika kuzaa unaruhusiwa kumleta dada yako au mdogo wako wa kike kuolewa na mmeo ili amzalie watoto. Sijui nitaelekea wapi naomba Serikali inifikirie nikiondolewa nitaenda wapi?.

Yohana Ochieng'i anasema anaishi peke yake, mwanamke alimkimbia mwaka 2016 akaondoka na watoto wawili, anafanya kibarua cha kuchungia watu ng'ombe ambapo kwa mwezi analipwa jumla Tsh. 35,000.

Yohana Ochieng'i

"Naomba Serikali itufidie ardhi nitaenda wapi? hii nyumba unadhani nikilipwa watanipa shilingi ngapi ya kuniwezesha kujenga ?mimi ni masikini sina kitu na ardhi hii nilirithishwa na baba yangu" anasema.

Leonida Otieno ni bibi anayekadikiwa kuzaliwa mwaka 1940 anaiomba Serikali kuwasaidia wananchi ili wapate haki zao katika zoezi la uthamini wa fidia linaloedelea katika vitongoji hivyo.

Wenyeviti wa Vitongoji, Kijiji, Madiwani wanasemaje kuhusiana na zoezi la uthamini wa fidia?

.................. Itaendelea 

Leonida Otieno



















No comments