WANANCHI, VIONGOZI CCM WAIKOSOA TASAF UJENZI KISIMA REBU SENTA
>>>Utata gharama zilizotumika katika ujenzi kisima cha asili.
>>>Viongozi CCM wadai taarifa waliyo nayo ujenzi umegharimu Tsh 700,000
>>>Mwenyekiti wa Mtaa asema mradi ni wa Tsh 350,000 hatua ya ujenzi ilipofikia imegharimu Tsh 300,000, ujenzi unaendelea
>>>Mratibu TASAF asema hatua ilipofikia haizidi Tsh 400,000 ujenzi unaendelea
Na Dinna Maningo, Tarime
WANANCHI wa Mtaa wa Rebu Senta pamoja na viongozi wa kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Turwa wilayani Tarime, wamekosoa mradi wa ujenzi wa bomba katika kisima cha asili unaojengwa kwa fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa kushirikiana na wanufaika wa kaya masikini.
Ni baada ya kutolidhishwa na ujenzi ambapo Mwandishi wa DIMA Online alifika kwenye kisima hicho na kubaini malalamiko ya wananchi.
Bomba ambalo halitoi maji kutoka kwenye kisima cha asili, ujenzi wake unadaiwa kugharimu kati ya Tsh. 300,000- 700,000
Wananchi wamedai kuwa fundi amejenga bomba ambalo halipokei maji kutoka kisimani licha ya fedha kutumika na hivyo wananchi kuendelea kuchota maji kwa kutumia jagi na vibakuli badala ya kukinga ndoo kwenye bomba.
Marwa Kimito amesema "TASAF walimleta fundi ili ajenge bomba pembeni kidogo na kisima ili wananchi wawe wanakinga maji kwenye bomba badala ya kuchuchumaa kuchota maji kwa kutumia majagi na vibakuli.
"Chakushangaza maji hayatelemki kwenda kwenye bomba kwakuwa eneo walikojenga lipo kwenye mwinuko hivyo maji hayapandi kuelekea kwenye bomba. Tunaomba TASAF wamwambie fundi arekebishe kisima"amesema Marwa Kamito.
Mlinzi wa kisima hicho Balozi Chacha Sinyaro mkazi wa mtaa huo amesema; "Huyu fundi alijenga vibaya bomba amelipeleka mbali na kisima eneo la mwinuko wakati kisima kipo kwenye mtelemko.
"Sehemu walikojenga ili watu wawe wanachoteapo maji hayafiki, wamejenga kwenye mwinuko maji yanashindwa kupanda kwasababu kisima kipo bondeni.
"Alipaswa kuchimba kisha ajenge bomba likae chini ili maji yapite lakini yeye kaliweka juu" amesema Balozi.
Ameongeza "Nikawashauri wananchi tuchimbe mtaro ili maji yapite kusaidia maji yasituame na kuchafuka, tunaomba fundi aje arekebishe na kisima kijengwe kwa kuzungushiwa zege ili kuzuia mmomonyoko, ili hata mvua ikinyesha maji yasichafuke" amesema.
Mwanamke mmoja mnufaika wa TASAF amesema " Sisi sio mafundi hatuna utaalamu wa kujenga, sisi kazi yetu ni kusogeza mawe, kuchanyanya udongo, kusogeza maji n.k.
"Kazi zenyewe ni ngumu wengine ni wazee wengine wagonjwa lakini unawakuta wanaponda kokoto, wananchanganya zege. Pesa yenyewe hatujui tutalipwa sh. ngapi na lini maana tangu tumeanza hii kazi ya kufanya shughuli za kijamii mtaani hatujalipwa pesa, hali hii imesababisha wanufaika wengine kutofika kazini."amesema mnufaika wa TASAF .
Kumekuwepo na sintofahamu gharama zilizotumika ujenzi wa kingio la maji (bomba) katika kisima hicho cha asili, viongozi wa CCM wamedai taarifa waliyonao ni kwamba ujenzi umegharimu Tsh.700,000 na kusema kuwa kiasi hicho hakiendani na hali halisi ya ujenzi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Rebu Senta Imani Mnanka amesema hatua ya ujenzi ilipofikia imegharimu Tsh 300,000 huku Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo (TASAF) akidai hatua ya ujenzi ilipofikia haizidi 400,000 na ujenzi bado unaendelea.
Mwenyekiti huyo wa mtaa wa Rebu Senta amekiri kuwa ni kweli fundi alijenga eneo ambalo siyo sahihi na hivyo kusababisha maji yasifike kwenye bomba.
Amesema mradi ni wa Tsh 350,000 na kwamba haujakamilika na pindi utakapokamilika wanamtaa watasomewa taarifa ya mapato na matumizi.
""Kisima hakijakamilika na hakijatolewa taarifa ya kukamilika bado muda wa ujenzi haujakamilika. Tulikuwa tunapambana na kisima kingine kinachofahamika kwa jina la kisima cha Samwel Mnanka ambacho kilijengwa alafu maji yakawa yanapita pembeni.
"Tulimwita mratibu wa TASAF tukazungumza nae kuhusu malalamiko kuwa fundi alikosea aliweka bomba sehemu haikustahili kuwekwa, na fundi ameshapewa maelekezo kurekebisha atarekebisha"amesema Mwenyekiti wa Mtaa.
Mwenyekiti huyo wa mtaa amekanusha uvumi kuwa mradi umegharimu Tsh. laki saba.
" Siyo laki saba, tuna visima vitatu na kila kisima kinasimamia Tsh.350,000. hadi sasa gharama zilizotumika ni mawe trupu moja Tsh. 100,000, mchanga tripu moja Tsh. 1000,00 na saruji ilinunuliwa mifuko 5 jumla Tsh. 100,000, imetumika mifuko 3 imebaki mifuko 2 bado ujenzi unaendelea.
" Wananchi nao walichangia nguvu kazi kwa kusogeza mawe, kuchimba mtaro.Nikweli fundi alikosea amejenga sehemu ya mwinuko, mapungufu yalifanyika sisi hatukuwa karibu na fundi ambaye anashirikiana katika ujenzi huo na wanufaika wa TASAF "Amesema Imani.
Juni, 27, 2023 Kamati ya siasa ya CCM Kata ya Turwa ilifika kukagua mradi huo unaolalamikiwa ambapo Katibu wa Chama hicho Kata ya Turwa, Marwa Timoro amesema kamati ilibaini maji kutofika kwenye bomba kutokana na mapungufu katika ujenzi na kuagiza fundi afanye marekebisho.
"Kipo kisima kingine fundi huyuhiyu alifanya makosa, kamati iliagiza kisima kirekebishwe, kisima ni cha asili kinafanyiwa maboresho lakini bado wanajenga kinyume na mahitaji, tunaomba TASAF wasimamie vyema"amesema Marwa.
Katibu huyo ameongeza kusema "Taarifa tulizonazo ni kwamba kisima hicho chenye mapungufu katika ujenzi tayari kimegharimu Tsh 700,000 licha ya kwamba maji hayafiki bombani, na fundi wanayemtumia amekuwa akilalamikiwa kulipua kazi" amesema Marwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Turwa Andrew Oteigo amesema Kamati ya siasa ya Kata ilitembelea kisima hicho na kubaini mapungufu katika ujenzi ambapo wameitaka TASAF kusimamia vyema miradi na kuhakikisha kisima kinafanyiwa marekebisho.
Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya mji Tarime, Desmond Basaya amesema hadi hatua iliyofikia gharama haizidi 400,000.
"Hakuna kisima Rebu kilichojengwa kwa laki 7 hivyo nashangaa taarifa hizo zimetoka wapi. Ujenzi bado unaendelea
nakukaribisha wiki ijayo tutakuwa site kuendelea na ujenzi tutakujuza gharama ukifika....hadi kufikia hatua ile haijazidi laki 4." amesema Mratibu TASAF.
Post a Comment