HEADER AD

HEADER AD

BENKI YA MAZIWA YA MAMA SULUHISHO KWA WATOTO WACHANGA

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam 

UTAFITI uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Mloganzila, Dar Es Salaam  umebaini kuwa asilimia 53 ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu chini ya kilo moja na nusu huchelewa kuanzishiwa kupewa maziwa ya mama kwa zaidi ya siku mbili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mama kuwa mgonjwa baada ya kujifungua, kufariki, kutokuwa na maziwa ya kutosha pamoja na mtoto kuwa mgonjwa.

Utafiti huo wa mwaka mmoja ambao ulianza  Mei 2018 hadi Mei 2019 ulibaini kuwa tatizo hilo linasababisha mtoto kupewa maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama jambo ambalo linawanyima lishe bora watoto mara baada ya kuzaliwa.

Baadhi ya  wanawake waliokumbana na kadhia kutonyonyesha watoto wao mara baada ya kujifungua wamesema kuwa, walalazimika kuwapa watoto wachanga maziwa ya kopo ili aweze kunywa kutokana na wao kupata matatizo mbalimbali ya kiafya.

" Nilijifungua mtoto akiwa na uzito pungufu (njiti) maziwa yangu yalikua hayatoki kutokana na hali yangu ya kiafya, ndugu zangu walilazimika kununua maziwa ya kopo ili waweze kumsaidia mtoto wangu ambaye kwa sasa ana umri wa miezi mitano," amesema Amina Omary mkazi wa Kinondoni.

Ameongeza kuwa, hivyo basi kuanzishwa kwa benki hiyo  kutawasaidia watoto kupata maziwa ya mama mara baada ya kuzaliwa hali ambayo itawasaidia kupata lishe bora wakiwa wachanga, Kwa sababu baadhi yao wakitumia maziwa ya kopo wanaharisha.

Naye Josephine Kamugisha anasema kuwa, mtoto wake ambaye kwa sasa ana umri wa miezi saba alilazimika kutumia maziwa ya kopo mara baada ya kuzaliwa kutokana na maziwa yake kutoka na kushindwa kumnyonyesha.


" Nilipojifungua maziwa yangu yalikua hayatoki, nilikua naumwa, nikashindwa kumnyonyesha mwanangu,  familia yangu ililazimika kununua maziwa ya kopo na kumpa mwanangu ambaye kwa sasa ana umri wa miezi saba na wiki mbili, hivyo basi tunaamini benki hiyo itasaidia wazazi wenye changamoto ya kutokuwa na maziwa au kuugua  watoto waweze kupata maziwa bora ya mama," amesema Kamugisha.

Ameongeza kuwa, kuna baadhi ya wazazi wanapojifungua wanafariki, hivyo basi mtoto ataendelea kupata maziwa ya mama kutoka kwenye benki hiyo ambayo itasaidia kuimarisha afya yake na kupata lishe bora.

Hata hivyo, Serikali Iko kwenye mpango wa kuanzisha benki ya maziwa ya mama ambapo utasaidia kupunguza changamoto za baadhi ya watoto wachanga wanaoanza kunywa maziwa ya kopo katika siku zao za kwanza toka kuzaliwa kwao.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Lishe Wizara ya Afya, Neema Joshua amesema kuwa wizara ya Afya inaunga mkono uanzishwaji wa benki ya maziwa ya mama na ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali Ili kuhakikisha mpango huo unakamilika.

" Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali Ili kuhakikisha mpango wa kuanzisha benki ya maziwa ya mama unakamilika,  lengo ni kuboresha hali ya afya na lishe za watoto wetu hususani wanaozaliwa na uzito pungufu au kabla ya wakati na mama zao kukosa maziwa ya kutosha jambo linalosababisha watoto hao kutokuwa vizuri” amesema Joshua.

Kwa upande wake Daktari wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk. Lucy Mpayo amesema, kuwa benki ya maziwa ya mama ni huduma inayowawezesha akina mama kupata maziwa ya ziada, ambayo huchangiwa na wamama wengine kwa hiari na kuhifadhiwa kwa usalama kisha kupatiwa watoto wenye mahitaji. 

Amesema kuwa, uwepo wa benki hiyo kutawezesha watoto kupata maziwa ya mama kwa muda muafaka na kusaidia kuimarisha afya zao, hususani kuongezeka uzito kwa haraka zaidi Kwa sababu mtoto anayezaliwa na uzito pungufu akiwahi kupewa maziwa ya mama katika siku za mwanzo baada za kuzaliwa humsaidia kumkinga dhidi ya maradhi na kumuwezesha kukua vizuri na hivyo kumpunguzia siku za kukaa hospitalini.

" Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila ilifanya utafiti wa mwaka mmoja kutoka Mei 2018 hadi Mei 2019 na kubaini kuwa asilimia 53 ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu chini ya kilo moja na nusu huchelewa kuanzishiwa kupewa maziwa ya mama kwa zaidi ya siku mbili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mama kuwa mgonjwa baada ya kujifungua, kutokuwa na maziwa ya kutosha pamoja na mtoto kuwa mgonjwa, jambo ambalo linamrudisha nyuma Katika ukuaji wake," amesema Dk. Mpayo.

Daktari wa watoto kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya PATH-Nairobi, Kenya Dk. Emily Njuguna amesema kuwa nchi hiyo ilianzisha benki ya maziwa ya mama Ili kuwasaidia watoto wachanga kupata lishe bora mara baada ya kuzaliwa endapo mzazi wake atakumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya na kushindwa kumnyonyesha, ,jambo ambalo limefanikiwa.

"Kwa Afrika Mashariki, Kenya ndo nchi ya kwanza kuanzisha benki ya maziwa ya mama Mwaka 2019 ambapo wachangiaji wanapimwa afya zao na maziwa yanachujwa Ili mtoto aweze kupata maziwa bora ambayo yatamsaidia kwenye lishe na afya yake," amesema Njuguna.

Uanzishwaji wa benki ya maziwa ya mama ulianza rasmi mwaka 1909 nchini Austria na kufuatiwa na Amerika ya Kaskazini mwaka 1919 na kisha kuenea katika nchini nyingine. Duniani.

Mwaka 1980 benki nyingi za maziwa ya mama zilifungwa kutokana na hofu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, lakini baada ya mikakati mingi ya  kuzuia maambukizi ya vijidudu vya ugonjwa huo kuanzishwa, waliweza kuwafanyia vipimo akina mama wanaochangia maziwa hayo na kisha kuyahifadhi kwa usalama zaidi benki hizo zilifungiliwa tena. 

Kwa upande wa Afrika, benki ya kwanza ya maziwa ilianzishwa nchini Afrika Kusini mwaka 1980, na kisha kufuatiwa na Cape Verde 2011.

Mwaka 2021, Serikali ilizinduliwa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ikiwa na malengo mbalimbali yakiwamo  kuboresha afya ya mtoto kuanzia akiwa tumboni hadi anapozaliwa.


No comments