HEADER AD

HEADER AD

MKOA WA PWANI WAPATA TUZO YA USHINDI MKATABA WA UTEKELEZAJI LISHE

 

Na Gustafu Haule, Dodoma

WAZIRI wa Nchi ,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Angellah Kairuki ameutangaza Mkoa wa  Pwani kuwa mshindi katika Mkataba wa utekelezaji wa masuala ya lishe katika kipindi cha mwaka 2022 /2023.

Kairuki ametangaza ushindi huo Agosti 29 Mjini Dodoma katika mkutano wa tathmini wa masuala ya lishe uliofanyika Mjini hapa kwa kuwakutanisha wakuu wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa .

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais(Tamisemi) Angellah Kairuki( kushoto) akimkabidhi tuzo ya ushindi wa mkataba wa lishe kwa mwaka 2022/2023  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na anayeshuhudia pembeni ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchata.

Aidha,kutokana na Mkoa wa Pwani kuibuka mshindi Waziri Kairuki amemkabidhi tuzo ya ushindi huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge huku akitaka mikoa mingine kuiga mfano huo.

Akizungumza katika mkutano huo Kairuki ,amesema kuwa Mkoa wa Pwani umeonyesha umakini katika usimamiaji na ufuatiliaji katika utekelezaji wa Mkataba wa lishe wa mwaka 2022/2023 na kwamba wanastahili kupewa heshima kwakuwa wamefanya kile wanachostahili.

Kairuki,ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa Mkuu wa Mkoa Abubakar Kunenge,na Katibu Tawala Rashid Mchata pamoja na watendaji wake.

" Mkoa wa Pwani umeibuka mshindi katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa mwaka 2022 na 2023 hivyo ninakabidhi tuzo maalum kwa Mkuu wa mkoa wa Pwani kwa ajili ya kutambua juhudi na kazi kubwa katika kusimamia mradi huo,"amesema Kairuki.

Kairuki,amesema hatua iliyofikiwa na Mkoa wa Pwani inapaswa kuigwa na Mikoa mingine ambapo kwa kufanya hivyo itaweza kusaidia kufikia malengo ya Taifa ya kupunguza hali ya udumavu kwa watoto.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amemshukuru Waziri Kairuki kwa namna alivyoutambua Mkoa huo juu ya utekelezaji wa mkataba wa lishe.

Kunenge amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya ofisi ya mkuu wa mkoa na watendaji wake hivyo ushindi huo ni heshima kubwa ndani ya mkoa.

"Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa kuutambua mkoa wa Pwani kuwa kinara wa masuala ya lishe na tuzo hii inakwenda kuwa sehemu ya kuongeza juhudi zaidi katika kuhakikisha masuala ya lishe ndani ya mkoa wangu yanapewa kipaumbele,"amesema Kunenge.

Kunenge amesema kuwa pamoja na kusimamia  vizuri mradi huo lakini bado wanaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo kama vile elimu, afya, maji, barabara na huduma nyingine za kijamii.

Amesema kuwa,katika kipindi cha miaka miwili Mkoa wa Pwani umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi za kutekelezaji miradi hiyo.

Hatahivyo, amesema mkoa umejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mradi unasimamiwa vizuri ili kusudi wananchi waweze kupata huduma nzuri na hivyo kufikia malengo ya Rais ya kutaka kila mwananchi aishi katika mazingira bora.



No comments