HEADER AD

HEADER AD

CCM BUTIAMA YAMPATIA BARUA MWENYEKITI WA KIJIJI BAADA YA KUMWONDOLEA DHAMANA SIKU 18 ZILIZOPITA


Na Dinna Maningo, BUTIAMA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama mkoani Mara kimempatia barua Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Kata ya Mwirwa, Wilaya ya Butiama mkoani Mara ya kumwondolea dhamana ya uenyekiti wa Kijiji.

Barua hiyo iliyoandikwa Agasti, 01, 2023, imeeleza kuwa kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Butiama kilichoketi Julai, 14, 2023, chini ya Mwenyekiti Christopher Marwa Siagi, pamoja na mambo mengine kilijadili mwenendo wa tabia za viongozi wa CCM kwa mujibu wa Ibara ya 76 (kifungu Na 7).

Imeelezwa katika barua hiyo kuwa, kikao kilipokea taarifa ya kamati ya maadili pamoja na kamati ya siasa ya wilaya, na kujiridhisha pasipo shaka kuwa amekiuka Ibara ya 5 na kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dora toleo la mwaka 2022 kifungu (i), (iii), (iv) na (v).
    Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Mkaruka Hamis Kura

Kwa kuzingatia vifungu hivyo vidogo hasa kifungu (v) kinanukuliwa "KIONGOZI WA CCM AWE MKWELI, MWAMINIFU KWA CCM NA MWENYE TABIA NA MWENENDO SAFI KWA JAMII".

Kwa mujibu wa barua imeelezwa kuwa mwenyekiti huyo wa Kijiji alituhumiwa kwa makosa 7 ambayo yote alishindwa kuyatolea maelezo likiwemo la kufungwa kifungo cha nje miezi 4 shauri la jinai Na.06/2020 Mahakama ya Mwanzo Zanaki.

Imeelezwa katika barua kwamba, akiwa kama kiongozi, ni dhahiri kabisa tabia yake na vitendo vyake kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili ya CCM na Jumuiya zake Ibara ya 8(9) amekichafua na kufanya kisiaminike kwa wananchi.

Hivyo basi kikao cha Halmashauri ya wilaya hiyo kimemuondolea dhamana kwa mujibu wa Ibara ya 39 kifungu (i)c cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la 2005.

Kwa maana hiyo ataendelea kuwa mwanachama wa CCM lakini amepoteza sifa za kuwa Mwenyekiti wa Kijiji na atakuwa chini ya uchunguzi kwa muda usiopungua miezi 42, na katika kipindi hicho anatakiwa kutimiza masharti na wajibu wote wa mwanachama.

Barua iliyosainiwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya hiyo Hamis Mkaruka Kura, nakala kwa katibu wa CCM mkoa wa Mara, kwa Taarifa, mkuu wa wilaya ya Butiama kwa Taarifa.

Pia nakala kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama kwa taarifa ambapo chama kimetaka kuendelea na taratibu za kisheria.

Machi, 25, 2023, DIMA Online illiripoti habari isemayo 'CCM BUTIAMA ILIVYOMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA KIJIJI'

Novemba, 10,2022 Chama hicho kupitia Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Mkaruka Hamis Kura kilimwandikia barua ya kumsimamisha uongozi wa uenyekiti wa kijiji ambapo alieleza kuwa alipokea barua ya tuhuma kutoka halmashauri kuu ya Kata ya Mirwa wakimtuhumu kwa mambo yafuatayo;

Tuhuma hizo ni kutosoma mapato na matumizi ya Kijiji, kukwamisha ujenzi wa choo, kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari, kuchukua matofali 500 ya Chama na mawe ya umoja wa vijana Kata na kutumia kwa manufaa yake bila ridhaa yao.

Kuchukua fedha ya mwananchi ya maji Tsh.367,000 bila kutoa stakabadhi na kufanyia shughuli zake. Pia amefungwa kifungo cha nje kwa kesi ya jinai Na. 6/2020 ZANAKI na kukatalia kwenye eneo la Serikali (Daire) na kufanya makazi.

Katibu huyo wa CCM kupitia barua hiyo alieleza "Kwa hoja hizo saba nakubaliana na uongozi wa Kata kwa ku
kusimamisha uongozi ili kupisha uchunguzi.

" Pia nakupa nafasi ya kujibu tuhuma zako kwa maandishi kwa mujibu wa kanuni na Maadili  Ibara ya 7 kifungu cha 4 (i), tuhuma hizo uzijibu ndani ya siku saba kuanzia siku utakapopata barua hii" barua imeeleza.

Barua aliyoisaini na kugongwa mhuri na nakala kwenda kwa Katibu wa CCM Kata - asimamie uongozi hadi uchunguzi utakapokamilika, Mkuu wa wilaya - Tuma vyombo vya ulinzi na usalama vimchunguze, Katibu wa CCM mkoa wa Mara na Katibu mkuu chama cha Mapinduzi Dodoma. Magige Mahera alithibitisha kupokea barua hiyo tarehe Novemba,10, 2022.

Hata hivyo Magige Mahera alipinga tuhuma hizo kama ilivyoripotiwa na chombo hiki cha habari Machi, 23,2023 na Mwandishi wetu wa habari aliyekuwepo Kijiji cha Magunga kwa siku kadhaa akifuatilia changamoto mbalimbali na sakata la Mwenyekiti huyo kusimamishwa uongozi na Chama chake cha CCM.

               Magige Mahera

Mwenyekiti wa Kijiji hicho alidai kuwa kusimamishwa kwake kunatokana na chuki binafsi kwa baadhi Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mirwa .

Machi, 19, 2023 Chombo hiki cha habari kiliripoti habari yenye kichwa cha habari isemayo 'CCM MIRWA YADAIWA KUTUMIA VIBAYA MADARAKA , Chama hicho kikiongozwa na Mwenyekiti CCM Kata Moris Onyango Odhiambo, Katibu Patrick Roche Pius. 

Baadhi ya wajumbe wa Serikali ya Kijiji wakiwemo wenyeviti wa vitongoji walishangazwa na hatua ya CCM Kata ya Mirwa kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji huku halmashauri ya Kijiji ikiwa haijawahi kumjadili katika vikao juu ya tuhuma zilizodaiwa na CCM.

Machi, 21, 2023 iliripotiwa habari isemayo CCM YAELEZA SABABU YA MWENYEKITI WA KIJIJI KUSIMAMISHWA UONGOZI.

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mirwa Moris Onyango Odhiambo alikanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao na kutoa sababu za kumsimamisha uenyekiti.

Machi, 23, 2023 iliripotiwa habari yenye kichwa cha habari kisemacho   'MWENYEKITI ALIYESIMAMISHWA UONGOZI MAGUNGA AFUNGUKA'  Mwenyekiti Magige Mahera Msyomi alisema kuwa kusimamishwa kwake kunatokana na chuki za baadhi ya viongozi wa chama baada ya kufuatilia matumizi ya fedha za miradi na alipoonekana kuhoji viongozi wakamuundia njama ya kumkataa ili kulinda maslahi yao katika Kijiji hicho.

Novemba, 10, 2022 Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya kilimsimamisha uongozi yeye pamoja na wajumbe watatu wa Serikali ya Kijiji ambao ni Joseph .M. Wambura, William Mriri Ghati na Juma Jumbe Wilson kwa tuhuma saba zikiwamo za matumizi mabaya ya madaraka. 

Habari zingine zilizoripotiwa kutoka Kijiji cha Magunga kuhusiana na sakata la Mwenyekiti wa Kijiji na viongozi wa CCM ni pamoja na habari ilivyoripotiwa Machi, 27, 2023,  'DIWANI : SIKUFANYA MAKOSA KUMTAMBULISHA MSIBANI MJUMBE'.

Machi, 29, 2023, iliripotiwa habari 'WASEMAVYO WENYEVITI WA VITONGOJI, WAJUMBE KUSIMAMISHWA MWENYEKITI WA KIJIJI'.

March, 31, 2023, iliripotiwa habari 'WANANCHI WAISHUKIA CCM BUTIAMA KUMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA KIJIJI'.


No comments