MAUWASA KUANZA KUFUNGA MITA ZA MALIPO
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa(Mauwasa)iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ina mpango wa kufunga Mita za maji za malipo kabla(Prepaid Meters)kwa wateja wake kwa lengo la kufanya majaribio ya mita hizo za kulipa ankra kabla ya matumizi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias amesema hayo mara baada ya Mamlaka hiyo kupokea mita hizo ambazo zitawasaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mauzo ya maji ili taasisi iweze kujiendesha ipasavyo.
"Tutaanza kwa majaribio kwa kufunga kwanza mita 20 hizi za kulipa kabla ya matumizi na tutalenga kwa taasisi za serikali pamoja na watumiaji wakubwa wakiwemo wafanyabiashara ili kuhakikisha mamlaka inamudu gharama za uendeshaji na matengenezo ,"amesema.
Mhandisi Nandi amesema kuwa mita hizo zina faida na miongoni mwa faida ni pamoja na kutatua changamoto za malalamiko kwa baadhi ya wateja kuhusu bili kubwa na bili bambikizi.
Pia amesema mteja ataweza kununua maji akiwa sehemu yoyote na mara tu atakaponunua yataanza kutoka bila kumlazimu yeye kufika kwenye mita na kuingiza tokeni.
"Kuna baadhi ya wateja wetu wamekuwa wakilalamika mara wanapopewa bili za Maji waliyotumia kwa Mwezi kwa kudai kuwa bili kubwa za maji na bili bambikizi kwa mita hizi ninaamini malalamiko hayo yatamalizika,"amesema.
Mhandisi Nandi ameeleza kuwa iwapo mita zitaonyesha mafanikio mazuri hivyo zitafungwa kwa wananchi na watakaokuwa wanatumia huduma hiyo ni wale wale wa maisha ya juu,kawaida na wa chini kama ilivyo kwa luku za umeme.
Wafanyakazi wa Mauwasa wakionyesha baadhi ya Mita za maji watakazozitumia kwa wateja wao.Aidha Mhandisi Nandi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu kwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya maji kwamaendeleo endelevu ya uchumi.
Baadhi ya wananchi wa mji wa Maswa wameipongeza Mauwasa kwa hatua hiyo na kusema kuwa maamuzi hayo yamechelewa sana na kuwatakanwananchi kutokuwa waoga.
"Mauwasa walichelewa kuleta mita hizi mie ninaamini ya kuwa utekekezaji wake utakuwa mzuri na kwamba mwanzo huwa unatia hofu lakini hakuna sababu ya kuogopa,"amesema Esther John.
Pia wamependekeza utaratibu wa mita hizi kuanza kutumiwa na viongozi wa Serikali wakiwemo na wabunge ili iwasaidie kujifunza namna ya kuzitumia na kuwaelimisha wananchi.
Post a Comment