WAKULIMA WA TUMBAKU B'MULO WAONJA ADHA YA UHABA WA DOLA NCHINI
Na Daniel Limbe,Biharamulo
CHANGAMOTO ya uhaba wa dola nchini umetajwa kuwatesa wakulima wa zao la tumbaku wilayani Biharamulo mkoani Kagera ambapo kwa zaidi ya miezi mitatu hawajalipwa hadi sasa.
Hatua hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima hao na kwamba upo uwezekano mkubwa wa kupungua kwa uzalishaji wa zao hilo msimu ujao 2023/24 kutokana na wakulima kukosa fedha za maandalizi ya mashamba yao.
Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method,akiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake.Malalamiko ya wakulima hao yamewasilishwa na Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method,wakati akiwasilisha taarifa za kata yake leo agosti 22 kwenye baraza la madiwani wa halmashauri hiyo huku akiiomba serikali kuwaonea huruma wakulima hao.
"Suala hili la malipo ya tumbaku limekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wa kata yangu kutokana na kuendelea kusota kwa zaidi ya miezi mitatu huku wakiwa hawajui hatma ya malipo yao kutokana na mkanganyiko wa serikali na kampuni ya ununuzi wa zao hilo".
"Tumekuwa tukiwafuata viongozi wa kampuni ya Mkwawa ambao ndiyo walikuwa wanunuzi wa tumbaku yetu tukitaka kujua hatma ya malipo yetu, majibu yao ni kwamba wanazo fedha nyingi tu za kutulipa wakulima wote tatizo ni serikali ambayo imewazuia kulipa kwa shilingi badala yake wanapaswa kulipa kwa dola" amesema Method
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,wakiwa kwenye kikao chao leo.Kutokana hali hiyo,Method ameitaka serikali kuacha kuwatesa wananchi kwa kigezo cha malipo kufanyika kwa dola,huku akidai kuwa miaka yote wakulima hao hulipwa kwa shilingi na kwamba baadhi yao hata mwonekano wa dola hawaujui tangu kuzaliwa kwao.
Kutokana na malalamiko hayo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,akamtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutoa majibu ya kina sababu za kucheleweshwa malipo ya wakulima wa tumbaku wilayani humo.
Akitoa majibu ya serikali,kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dk. Sospeter Mashamba,amekiri kuwa baadhi ya wakulima wa tumbaku wamekwama kulipwa kutokana na uhaba wa dola nchini huku akiwataka kuwa subira wakati serikali kuu ikiendelea kulifanyia kazi ili kuondoa adha hiyo.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Dk. Sospeter Mashamba,akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wakulima wa tumbaku."Kwanza ifahamike kuwa tatizo siyo halmashauri yetu kuwazuia wanunuzi wa tumbaku kuwalipa wakulima fedha zao, mkwamo umetokana na maelekezo kutoka serikali kuu kuwataka wanunuzi kuwalipa wananchi kwa dola
"Kama tunavyojua kuna changamoto ya uhaba wa dola hizo nchini kikubwa tuendelee kuwahimiza wananchi wetu kuendelea kuwa na subira na mambo yatakapo kaa sawa watalipwa hela zao ili kuepuka kupunjwa"amesema Dk.Mashamba.
Post a Comment