HEADER AD

HEADER AD

MCHUNGAJI AKAMATWA KWA ULAGHAI

>>Ni baada ya kutaka kupata waumini kwa kisingizio cha mchawi kudondoka kanisani.

>>Aliyejifanya mchawi na kudondoka kanisani akamatwa.

Na Gustafu Haule, Pwani

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata na kuwashikilia watu wawili akiwemo mchungaji wa kanisa la Pentekoste Gospel Mission lililopo Kibaha kwa ulaghai wa kutaka kupata waumini kwa kusingizia mchawi amedondoka kanisani hapo kutokana na maombi ya mkesha yaliyofanyika ndani ya kanisa hilo.

Mbali na mchungaji huyo lakini mwingine aliyeshikiliwa ni Basenga Matheo(59) ambaye ndiye mchawi wa uongo aliyedondoka kanisani hapo kwa kushirikiana na mchungaji huyo ili wawaaminishe wananchi na waumini kuwa kanisa hilo lina nguvu ya ajabu.

      Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo, amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa tukio hilo limetokea Agosti 24 mwaka huu majira ya saa 1 usiku huko Miswe Wilayani Kibaha.

Lutumo amesema kuwa taarifa za mchawi wa uongo kudondoka kanisani hapo zilifika katika kituo cha Polisi Kibaha kuwa mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Basenga Matheo mkazi wa Miswe Kata ya Mbwawa Wilayani Kibaha amedondoka kanisani .

Amesema kuwa mchawi huyo baada ya kufanya tukio hilo alileta taharuki kubwa kwa waumini na wananchi wakiamini kuwa maombi ya kanisa hilo ndio yamesababisha mchawi huyo kudondoka na ungo wake.

Aidha Lutumo ameongeza kuwa baada ya Jeshi lake kufanya ufuatiliaji na uchunguzi wa kina lilibaini kuwa tukio hilo limetengenezwa na watu wawili akiwemo mchungaji wa kanisa hilo.

Amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwataka walaghai waumini wake na wananchi wa maeneo ya jirani kuvutiwa na kanisa hilo ili kusudi hapate waumini wengi ambao watakuwa chanzo cha kujipatia mapato kanisani hapo.
    Kanisa la Pentekoste Gospel Mission

"Hawa watu wawili walitengeneza mbinu ya kuwalaghai waumini kuwa mchawi amedondoka kutokana na maombi ya kanisani hapo ili wajipatie fedha lakini Jeshi la Polisi baada ya kufuatilia lilibaini kuwa aliyedondoka ni mchawi feki", amesema Lutumo.

Hatahivyo Kamanda Lutumo amesema watu hao mpaka sasa bado wameshikiliwa kwa mahojiano zaidi lakini ametoa tahadhari kwa watu kuacha tamaa ya kujipatia kipato kwa njia ya ulaghai kwakuwa atakayedakwa atachukuliwa hatua kali.



No comments