WATAALAM 300 KUNUFAIKA NA UFADHILI WA MASOMO SEKTA YA AFYA
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
WATAALAM bingwa na bobezi wasiopungua 300, wanatarajiwa kunufaika na ufadhili wa masomo katika mpango maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan wa (Samia Health Super Specialisation Program In Tanzania) wa miaka mitano (2020-2025).
Hayo yamebainishwa Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya Mhe Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu mpango huo wa kila mwaka wa ufadhili wa masomo kwa Wataalamu wa Afya katika kada mbalimbali ambapo kwa mwaka huu ni mwaka wa Pili, na Rais Samia ameweza kutoa fedha kiasi cha Bilioni 9.
Amesema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ya Rais Samia ilitoa kiasi cha shilingi Bilion 8 katika mpango huo na sasa imetoa Tsh. Bilion 9, ni ongezeko la Tsh. Bil. 1.
Dkt.Mollel amesema, mageuzi makubwa yanazidi kufanyika ndani ya sekta ya afya lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ikiwemo yale ya kibingwa na kibingwa bobezi hapa hapa nchini.
“Kwenye eneo la ujenzi, tunaushuhudia uboreshaji wa miundombinu, ajira za wataalam, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi unaenda sambamba na kuendeleza taaluma za Wataalam wa Afya nchini ili waweze kutoa huduma bora za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini." Amesema.
“ Kama Wizara ya Afya ilijiwekea lengo la miaka mitano (2020-2025) la kusomesha wataalamu bingwa na bobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha. Kupitia mpango huu wa ufadhili wa kuongeza wataalam bingwa na bozezi Tanzania (Samia Health Super Specialisation Program In Tanzania). Ameongeza Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema fedha hizo zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu bingwa na bobezi 848 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza Serikali ya Dkt. Samia inatarajia kufadhili Wataalamu wapya wasiopungua 300 kwa utaratibu wa kawaida pamoja na wataalamu wengine wasiopungua 100 kwa utaratibu wa seti (Mfano seti ya; Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Muuguzi Bingwa, Dakatri Bingwa wa ganzi na usingizi).
Dkt. Mollel amesema, maombi yote yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti https://esponsorship.moh.go.tz . na kusisitiza maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yaliyowasilishwa kwa njia ya mfumo pekee, hivyo waombaji wanakumbushwa kufuata utaratibu uliowekwa.
Pia, amebainisha “Ufadhili huo ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo, posho ya kujikimu na nauli kwa wanafunzi watakaopata ufadhili nje ya nchi.
“pamoja na posho ya utafiti pindi mwanafunzi anapokuwa kwenye kipindi cha kufanya utafiti kama sehemu ya mafunzo yake.
Post a Comment