HEADER AD

HEADER AD

MUUNGANO FC YATWAA UBINGWA NA KUJINYAKULIA KITITA BAADA YA KUICHAPA BUYOGA FC

>>Ni katika Mashindano ya Chato Samia Cup 2023

>>RC Geita aahidi ushirikiano

Na Daniel Limbe, Chato

MICHUANO ya Kombe la Chato Samia Cup 2023 imehitimishwa kwa kumpata bingwa wa mashindano hayo, ambapo timu ya Muungano FC imefanikiwa kutwaa taji hilo pamoja na kitita cha shilingi 1,000,000 baada ya kuichapa timu ya Buyoga FC kutoka Buseresere wilayani Chato mkoani Geita.

Ushindi huo umeamuliwa kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika bila kufungana hali iliyosababisha timu hizo kwenda kwenye mikwaju ya penati ili kumpata mshindi.

    Nahodha wa timu ya Muungano FC akishangilia kwa ushindi wa kikombe cha mshindi wa kwanza.

Haikuwa ridhiki kwa timu ya Buyoga FC ambayo imepoteza penati 2 na kufunga 2 huku moja ikishindwa kupigwa baada ya wapinzani wao Muungano FC kufanikiwa kutikisa nyavu kwa mikwaju yote mitano.

Kutokana na hali hiyo vijana wa Muungano FC kutoka kata ya Muungano Chato,wametawazwa kuwa mabingwa wa kwanza kabisa kutwaa kikombe pamoja na fedha za mashindano ya "Chato Samia Cup 2023" ambayo yalizinduliwa hivi karibunI wilayani hapa.

     Kikosi cha timu ya Muungano FC

Hata hivyo, Buyoga FC ambao wameshika nafasi ya pili katika mashindano hayo wameambulia kutwaa kitita cha fedha kiasi cha 500,000 huku mshindi wa tatu Butarama FC wakichukua shilingi 300,000.

Awali mdhamini mkuu wa mashindano hayo, Mahandisi Deusdedith Katwale,ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita,amesema malengo makuu ya kuanzishwa kwa michuano hiyo ni kuwaweka watu pamoja ili kuongeza ushirikiano,urafiki na kudumisha undugu baina ya wanamichezo na jamii kwa ujumla.

Pia kuenzi kazi kubwa za maendeleo zinazotekelezwa na rais Samia Suluhu Hassan kwenye wilaya ya Chato ikiwemo kuendeleza miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake Hayati Dk. John Pombe Magufuli.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela,akisalimiana na wachezaji wa Buyoga FC.

Pia kutumia michezo hiyo kuwahamasisha wananchi kulima mazao ya chakula na biashara hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zimeanza kunyesha maeneo mbalimbali wilayani hapa.

Akikabidhi zawadi hizo kwa washindi, Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo,amempongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa ubunifu mkubwa wa kuwaweka watu pamoja kupitia soka huku akizitaka wilaya zingine kuiga mfano huo.

Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Chato,Mhandisi Deusdedith Katwale,katikati ni Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela, na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mbogwe.

Hata hivyo,amepongeza vipaji vilivyoibuliwa kupitia mashindano hayo huku akiahidi kushirikiana na timu zote zilizopo mkoani humo kukuza vipaji kwa vijana ili watimize ndoto zao kwa kuwa sasa michezo ni ajira.

Katika mashindano hayo,wadhamini wenza walikuwa ni Benk ya CRDB,NMB,TCB na Rwaikondo Investment Ltd.

      Kikosi cha timu ya Muungano FC

Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela,akikabidhi kikombe cha mshindi wa kwanza kwa Muungano FC.

No comments