HEADER AD

HEADER AD

GEKUL AYATAKA MASHIRIKA KUTUMIA RASILIMALI VIZURI KUWAFIKIA WALENGWA

 


Na Gustafu Haule, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul amezindua dawati la msaada wa kisheria lililoanzishwa na shirika la 'Utu Kwanza' huku akiyataka mashirika binafsi yanayoshughulika na masuala ya sheria kutumia rasilimali zake vizuri kuwafikia walengwa.

Aidha Gekul amesema ni lazima mashirika hayo yakashirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya watu kwa kuzingatia kipaumbele cha Utu kwenye haki jinai na kwamba wote wana wajibu wa kuwatumikia Watanzania katika kudumisha amani na mshikamano.

     Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul katikati mwenye kofia nyekundu katika uzinduzi wa dawati la msaada wa kisheria chini ya Shirika la Utu Kwanza.

Gekul ameyasema hayo Septemba 10 mwaka huu wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa kisheria katika hafla ya ufunguzi wa dawati hilo lililofanyika viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam chini ya Shirika lisilo la Kiserikali la Utu Kwanza .

Amesema kuwa Wizara inatambua jitihada za Shirika la Utu Kwanza katika kuboresha maisha na utu kwa wafungwa na mahabusu kwa kipindi cha miaka sita tangu kuanzishwa kwake hususani kwa mkoa wa Dar es Salam na kwamba kutokana na na umuhimu huo lazima Serikali iwape ushirikiano wa kutosha.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mansoor Industries Ltd Altaf Hirani akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa dawati la msaada wa kisheria chini ya Shirika la Utu Kwanza.

Gekul ameongeza kuwa kwakuwa jambo hilo ni muhimu kwa maslahi ya Taifa Wizara itashirikiana na  Mahakama ili kuona namna ya kuridhia kuanza kwa dawati hilo bila kuathiri shughuli za kimahakama.

"Wizara inathamini mchango unaotolewa na Shirika la Utu Kwanza katika kusaidia jamii, sasa na mimi nitoe wito kwa Mahakama kuona namna ya kusaidiana na Utu Kwanza katika kuhakikisha dawati la msaada wa kisheria tunalolizindua leo linafanikiwa bila kuathiria shughuli za Kimahakama," amesema Gekul.

Gekul amelipongeza shirika hilo kwa kuanzisha dawati hilo huku akiomba shirika la Utu Kwanza kusambaa na maeneo mengine lakini wahakikishe wanatoa huduma hiyo kwa kufuata Sheria za nchi .

katika kusaidia dawati hilo kusonga mbele Serikali ya awamu Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imechangia mpango huo kiasi cha Sh.milioni 2 na kwamba Serikali itaendelea kuchangia zaidi kwa maslahi ya Taifa.

Mkurugenzi wa Utu kwanza Wakili Shehzada Walli, amesema lengo la kuanzisha shirika hilo ni kusaidia wafungwa ambao wengi wao wamefungwa bila kuwa na hatia pamoja na  watu ambao wanafikishwa polisi na wanakosa msaada wa kuweza kuwajulisha ndugu zao kuhusiana na kile kinachoendelea.

"Tumeona tukiweka dawati letu Mahakama ya Mwanzo na Wilaya litaweza kuwasaidia watu katika kuwauliza hali zao na kuwauliza kama wamewapigia ndugu au marafiki ambao wanaweza wakawasaidia",amesema Walli.

Walli amesema pia wataweza kutoa mafunzo ya nini kinafanyika anapoenda mbele ya Hakimu, anapataje dhamana kwa kutumia kitambulisho cha Taifa NIDA  au barua kutoka Serikali ya Mtaa na kwamba mtumishi wa shirika hilo atasaidia kufanikisha ili mhitaji aweze kupata dhamana na msaada mwingine.

Amesema kwa kufanya hivyo itapunguza idadi ya watu ambao wangeenda kukaa gerezani ambao wangeweza kupata msaada na kwasasa wameanza na Mahakama zilizopo Kinondoni ikiwemo Mahakama ya Mwanzo na Wilaya na tayari wameomba ruhusa ya kuweka dawati hilo.

Mkurugenzi huyo amesema  mbali na hilo lakini pia upo mradi wa nyumba salama kwa watoto ambao wazazi wao wapo gerezani na wale ambao wanazaliwa gerezani na wakirudi mtaani hawana wakuwatunza.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Mansoor Altaf Hiran alisema  kuwepo kwa dawati hilo ni jambo la muhimu kwani itasaidia wananchi kupata haki zao kwa wakati na kwamba kila mtu akipata haki yake amani itakuwepo.

Inspekta Msafiri Kundi kutoka gereza la Keko lililopo Jijini hapa amesema kuwa  dawati hilo likianza litakuwa na msaada kwa wafungwa na mahabusu kwani wapo baadhi yao hawana uwezo wa kupata Mawakili.

No comments