HEADER AD

HEADER AD

TAHADHARI YATOLEWA UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA


Na Samwel Mwanga, Maswa

WANANCHI wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wametakiwa kuwapeleka Mbwa wanaowafuga ili waweze kupata chanjo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wilaya hiyo kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha Mbwa.

Hayo yameelezwa Septemba 28 mwaka huu na Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Robert Urassa wakati wa maadhimisho ya siku ya Kichaa Cha Mbwa dumiani yaliyofanyika katika Uwanja wa Madeco mjini Maswa.

  Mkuu wa Divisheni ya MifugoKilimo na Uvuvi katika wilaya ya Maswa,Robert Urassa(mwenyewe kofia)akitazama Mbwa wakipata chanjo ya kichaa Cha Mbwa wakiwa kwenye toroli katika viwanja vya Madeco mjini Maswa

Amesema kuwa wilaya hiyo imepanga kutoa chanjo kwa wanyama ambao ni Mbwa na Paka ili kudhibiti ugonjwa huo ambao ni hatari kwa maisha ya binadamu iwapo utampata.

Amesema kuwa lengo hilo litakamilika iwapo wananchi watajitokeza kuchanja wanyama hao wenye dalili na wasio na dalili ya kichaa cha Mbwa ili kuzuia madhara yatokanayo na ugonjwa huo.

       Mbwa akipatiwa chanjo ya kichaa cha Mbwa kwenye viwanja vya Madeco mjini Maswa.

"Wilaya ya Maswa tumejipanga kuthibiti ugonjwa huu wa kichaa cha Mbwa hivyo malengo yetu ni kuhakikisha tunachanja Mbwa wote pia na Paka mlionao  kwenye nyumba zenu hivyo nitoe msisitizo kwa wananchi kuleta wanyama hao ili waweze kupatiwa chanjo,"

"Wale Mbwa ambao wanazurula hovyo mitaani ambao hawana uthibiti tutafanya utaratibu kwa kuwaondoa kwa kuwaua na kama una Mbwa wako ni vizuri ukamtunza vizuri nyumba usimuache azurule hovyo hovyo mtaani na hakikisha walao anapata chanjo walao mara  mojja kwa mwaka mmoja,"amesema 

Amesema kuwa chanjo hiyo inatolewa bure na serikali hivyo wananchi hawana budi kuleta wanyama hao ili waweze kupatiwa chanjo hiyo na mbwa ambaye ameupata hata kuwa na madhara hata kama atamng'ata mtu.

      Wananchi mjini Maswa mkoani Simiyu wajitokeza kupeleka Mbwa wao kwenye viwanja vya Madeco ili waweze kuchanjwa ili kuthibiti ugonjwa wa Kichaa Cha Mbwa wilayani humo.


"Hii chanjo inayotolewa bure na Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu na Mbwa akishapata chanjo hii hata akimng'ata mtu hakutakuwa na madhara yoyote ambaye mtu atayapata hivyo niwaombe tumieni fursa hii kuwachanja wanyama hao," amesema.

Amesema kuwa wilaya hiyo pia imechukua hatua mbalimbali ili kudhibiti ugonjwa huo na hadi sasa hatua mbalimbali zimeshachukuliwa ikiwemo amri ya zuio la Mbwa kuzurura.

Hatua nyingine ni utoaji wa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga ili wasipate maambukizi ya ugonjwa huo sambamba na kuwaondoa mbwa wa mitaani wasio na wamiliki ambao ndiyo wamekuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa ugonjwa na kuhatarisha usalama wa afya ya Jamii.

Naye Kaimu Daktari wa Mifugo wilaya ya Maswa, Dk Charles Msira amesema kuwa katika kipindi chaa Mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu kumekuwepo na Mbwa wenye dalili ya kichaa cha Mbwa na kushambulia baadhi ya wananchi ambapo ugonjwa huo umeripotiwa katika Kata za Nguliguli,Isabga,Sukuma,Buchambi, na Lalago .

       Kaimu Daktari wa Wanyama wilaya ya Maswa,Dk Charles Msira(mwenye koti rangi nyeupe)akitoa chanjo  kwa Paka aliyeletwa kwa ajili ya kupata chanjo ya wanyama hao.

Kata nyingine ambazo ugonjwa huo umeripotiwa ni pamoja na Binza,Nyalikungu ,Shanwa na Sola ambapo vifo vilivyoripotiwa ni watu watatu.

"Kwa binadamu virusi vya kichaa cha mbwa huweza kuingia mwilini kwa njia ya kung'atwa au kulambwa jeraha na mnyama aliyeathirika na kusambaa kupitia mfuko wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo hadi kwenye ubongo.

"Sisi wataalamu wa mifugo katika wilaya ya Maswa tunaungana na dunia kwa ujumla kutumia siku hii muhimu katika kuhamasisha Wananchi wa wilaya ya Maswa kuchanja Mbwa wao wote kwani chanjo ni njia pekee inayoaminika kitabibu katika kudhibiti kuenea kwa magonjwa mbalimbali dumiani kutokana inamuwezesha kiumbe kijitengenezea kinga yake ya mwili dhidi ya vimelea vya ugonjwa husika"amesema.

       Kijana (ambaye jina lake halikuweza kupatikana)akiwa ameleta Mbwa kwa ajili ya kupata Chanjo ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika viwanja vya Madeco mjini Maswa.

Baadhi ya wananchi walioleta Mbwa wao kupata chanjo George Nyagawa mkazi wa uwanja wa ndege  na Elia Masanja mkazi wa Sola wilayani hapa wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti waliiomba Serikali kulifanyia zoezi hili kuwa endelevu na kuwafuata Wananchi katika maeneo yao wanayoshi hasa maeneo ya vijijini ili wanyama hao wapate chanjo.

Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa dumiani hufanyika Septemba 28 kila mwaka na Kauli Mbiu ya mwaka huu inaeleza kuwa 'KICHAA CHA MBWA,KWA WOTE,AFYA MOJA KWA WOTE'.

        Mbwa akipatiwa chanjo kwenye viwanja vya Madeco mjini Maswa.

No comments