CCM SIMIYU YATOA MAAGIZO KUHAMISHWA MNADA WA DUTWA
Na Samwel Mwanga, Simiyu
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Simiyu imeielekeza Serikali kurejesha mnada wa Igaganulwa-Dutwa.
Mnada huo ulihamishwa kwenda eneo la Mwamabu-Dutwa umbali wa kilomita tatu kutoka eneo la awali kwenda eneo jipya lililotengwa na serikali na ambalo limezua mgogoro na malalamiko kwa wananchi.
Hayo yameelezwa Septemba,30 na Katibu wa Siasa na Uenezi CCM mkoa wa Simiyu, Mayunga George wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari kufuatia kumalizika kwa kikao maalum cha Kamati hiyo kilichofanyika Septemba 28 mwaka huu kujadili mgogoro huo.
Katibu wa Siasa na Uenezi CCM mkoa wa Simiyu,Mayunga George akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari(hawapo pichani)maalekezo ya Kamati ya Siasa ya mkoa huu juu ya mgogoro na malalamiko ya kuhamishwa kwa mnada eneo la Dutwa wilayani Bariadi
Serikali imeelekeza kuwa eneo la Mwamabu miundo mbinu yake haitoshelezi kufanya shughuli zote za biashara kwa sasa hivyo mnada wa mifugo kwa maana ya ng'ombe,mbuzi na kondoo uendelee kufanyika Mwamabu kwani eneo hilo ni rafiki kwa mnada wa mifugo kwa sasa hasa kufuatia uwepo wa bwawa la maji kwa ajili ya mifugo.
Pia mnada wa bidhaa zingine yaani gulio kama vile nguo,nafaka,vyombo na mbogamboga uendelee kufanyika eneo la Igaganulwa -Dutwa mpaka pale ambapo serikali itakapokamilisha miundo mbinu muhimu inayohitajika kwa biashara ya bidhaa hizo eneo la Mwamabu-Dutwa kutoka eneo ulipo sasa.
Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo katika kikao chake hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mgogoro na malalamiko ya wananchi ambao ni wafanyabiashara wa eneo la Igaganulwa-Dutwa.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed(mwenye miwani)akisisitiza jambo kwenye Mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi alipofika kusikiliza malalamiko ya wananchi kupinga kuhamishwa kwa mnada wa Kijiji hicho kupeleka Kijiji jirani cha Mwamabu.
Wafanyabiashara hao waligoma kufungua biashara zao yakiwemo maduka kwa muda wa siku tatu wakipinga kitendo cha serikali ya wilaya ya Bariadi kuhamisha mnada huo bila kuwashirikisha.
Awali wakiwakilisha malalamiko yao kwa Mwenyekiti CCM,Shemsha Mohamed katika mkutano wa hadhara uliofanyika Septemba 24 mwaka huu katika eneo la Dutwa walisema kuwa wameshangazwa na tangazo la serikali ya wilaya hiyo kuhamisha mnada huo bila Wananchi kushirikishwa.
Mwananchi,Veronica Warioba Mkazi wa Kijiji cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi akitoa malalamiko yake mbele ya Mwenyekiti wa CCM wa Simiyu,Shemsha Mohamed (hayupo pichani)juu ya kuhamishwa kwa mnada kwenye eneo lao.
Walisema kuwa mnada huo katika eneo la Igaganulwa-Dutwa ulianzishwa mwaka 1974 na wamekuwa wakifanya Biashara zao bila usumbufu wowote kwa muda mrefu lakini kilichowashangaza ni tamko la eneo la mmada kuhamishwa ghafla kulikofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
"Mnada huu umekuwepo tangu mwaka 1974 tunafanya biashara kwenye eneo hili bila usumbufu wowote lakini hivi majuzi tu tunapata tangazo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Bariadi kuwa mnada unahamishwa kwenda Mwamabu na wala sisi wananchi hatujashirikishwa,"Alisema Mashaka Goba.
Walisema kuwa pamoja na kuomba Viongozi wa wilaya hiyo ambao ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bariadi na Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi ili wafike waweze kuwasilikiza hawakufika isipokuwa walikwenda kufanya Mkutano kwenye eneo la Mwamabu huku wao wakiwapuuza na kuwaita wahuni.
Mwananchi,Amos Lubacha Mkazi wa Kijiji cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi akitoa malalamiko yake mbele ya Mwenyekiti wa CCM wa Simiyu,Shemsha Mohamed (hayupo pichani)juu ya kuhamishwa kwa mnada kwenye eneo lao.
"Tuliwaomba Viongozi wetu wa wilaya wakiwemo wa serikali na CCM Wilaya ili waweze kuja kutusikiliza lakini hakufika wakaenda eneo la Mwamabu kufanya Mkutano wa hadhara huko walituita majina mengi likiwemo sisi ni Wahuni ambao tunalalamikia kwa kweli matamshi hayo yalituumiza sana,"
"Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anasisitiza viongozi kufika kuwasikiliza Wananchi na kutatua changamoto zetu lakini kwa hili kwetu hatujasikilizwa na Viongozi wa wilaya na aliyefika ni Mbunge wetu wa Jimbo,Nkundo Mathew tu Sasa nawe umekuja huenda mgogoro huu utapatiwa ufumbuzi,"Alisema Charles Somanda.
Walisema kuwa baadhi ya akina mama wamechukua mikopo kwenye taasisi mbalimbali za fedha zikiwemo benki hivyo wanashindwa watarudisha vipi kwani siku ya mnada ndiyo wanafanya biashara mbalimbali zikiwemo za kuuza chakula na mbogamboga
"Sisi wakinamama wajasiliamali tunafanya biashara siku ya mnada na mitaji yetu wengine tumekopa benki tunatarajia kuirudisha sasa mnapohamisha mnada wetu ghafla hivi hata bila kutushirikisha ni kutaka tufilisiwe maana tutashindwa kurejesha fedha tulizokopa,"Alisema Mariam Mandalu
Akizungumza na Wananchi hao Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed amewahakikishia kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwani serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa ni sikivu haipendi wananchi wake wasimbuliwe hivyo wawe na subira wakati linafanyiwa kazi.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed akijitambulisha kwa wananchi katika Kijiji cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi alipofika kuwasikiliza malalamiko yao.
Mwenyekiti huyo akijitambulisha kwa wananchi katika Kijiji cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi alipofika kuwasikiliza malalamiko yao.
"Mie nimefika na nimewasikiliza malalamiko yenu CCM ndiyo inayoongoza serikali iliyoko madarakani hivyo kuweni na subira jambo hili linakwenda kupatiwa ufumbuzi maana serikali yetu chini ya CCM ni sikivu kuweni na subira ila poleni kwa yote yaliyotokea niwahakikishie jambo hili linakwenda kumalizika na kuweni na Amani kabisa,"Alisema.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Saimon Simalenga alisema kuwa moja ya sababu kubwa ya kuhamishwa kwa mnada huo ni kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara kwa watu kugongwa na magari kutokana na mnada huo kufanyika ndani ya hifadhi ya barabara.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed(wa pili toka kushoto)na Katibu wa CCM mkoa wa Simiyu,Leah Ndegeleki(wa pili toka kulia)wakiwa wanasikiliza malalamiko ya wananchi wa kijiji Cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi baada ya mnada wao kuhamishwa na serikali.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed akijitambulisha kwa wananchi katika Kijiji cha Igaganulwa-Dutwa wilaya ya Bariadi alipofika kuwasikiliza malalamiko yao.
Post a Comment