WAANDISHI WA HABARI ZA MAZINGIRA NA NISHATI WATEMBELEA KITUO CHA TAIFA GESI
Na Gustafu Haule, Pwani
WAANDISHI wa habari za utunzaji wa mazingira na uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala kutoka Mkoa wa Pwani wamefanya ziara ya kutembelea kituo kikuu cha kampuni ya Taifa Gas ya uingizaji na usambazaji wa gesi hapa nchini kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo imefanyika Septemba 6 mwaka huu ikiwa chini ya uongozi wa Taifa gas kupitia afisa mahusiano wake Ambwene Mwakalinga kwa uratibu wa afisa ushirika wa masuala ya ndani ya Taifa gas Anjellah Bhoke.
Lengo la ziara hiyo ni kujifunza masuala mbalimbali juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za uchakataji wa gesi kutoka katika kituo mpaka hatua ya mwisho ya kufika kwa jamii.
Wakiwa katika kituo hicho waandishi hao walipewa mafunzo mbalimbali ikiwemo ya masuala ya usalama,afya,ulinzi ,mazingira pamoja na matumizi yake mafunzo ambayo yalitolewa chini ya mkuu wa kitengo hicho Albert Gungayena.
Katika mafunzo hayo Gungayena,amesema kuwa kituo cha Taifa Gas ni kikubwa na ndio kituo cha kwanza nchini kinachoweza kuhifadhi gesi kwa kiwango kikubwa na kusema kwasasa uwezo wa kuhifadhi umefikia 7,440,huku akisema kazi kubwa ya kituo hicho ni kupokea gesi kutoka katika meli,kujaza na kusambaza katika mikoa mbalimbali.
Gungayena,amesema gesi ya Taifa Gas ni gesi ya LPG ( Liguidfield Petroleum Gas) inayotokana na mafuta ghafi (Crude Oil) ambayo haina madhara lakini ni nzuri kwa matumizi kwakuwa ina kiwango kidogo cha hydrocarbons.
Amesema kuwa, kutokana na kuangalia umuhimu wa watumiaji wa gesi hiyo Taiga gesi imekuja na mitungi ya kuanzia kilo 3 ,kilo 6, kilo 15 na kuendelea huku akiongeza kuwa mitungi yake ni salama kwakuwa imewekwa valvu za usalama(Safety Valve).
"Nawashauri Watanzania watumie gesi ya LPG ili kulinda na kutunza mazingira maana matumizi ya gesi yatapunguza ukataji wa miti hovyo kwa sababu ya kuchomea mkaa lakini ukitumia gesi unaokoa fedha kuliko kutumia mkaa,"amesema Gungayena.
Gungayena, amesema kuwa matamanio yake ni kuona baada ya miaka mitano mpaka kumi kila Mtanzania hawe anatumia Taifa gas kwakuwa nishati safi na inatunza mazingira na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira .
Amesema kuwa,jambo kubwa ni kuona matumizi ya mkaa na kuni vinaisha kwakuwa vinaleta madhara ya magonjwa ya pumu na mapafu ndio maana Taifa gas imeweka mkakati wa kuhakikisha kila Kata,Wilaya na Mkoa wanafikiwa na gesi hiyo.
Meneja Mkuu wa kituo hicho Juma Masese,amesema kampuni hiyo ilianza kama Mihani gas ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Irani lakini baadae ikauzwa kwa Mtanzania na mwaka 2019 jina likabadilika kuwa Taifa Gas.
Masese,amesema wakati wanapokea Taifa gas kutoka Mihani uzalishaji ulikuwa tani1,440 lakini kwasasa uzalishaji umefikia tani 7,440 ambapo ndio kampuni ya kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa gesi.
Amesema kwasasa Taifa gas inavituo 21 Tanzania na malengo ni kufika asilimia 100 ambayo itakuwa imefikia katika Vijiji vyote huku akiomba watanzania wanaponunua gesi wahakikishe mitungi inapimwa kwa ajili ya kudhibitisha uzito.
Afisa Uhusiano wa Taifa Gasi Ambwene Mwakalinga, amesema kuwa uwekezaji katika kampuni hiyo unaendelea na sasa wanajenga kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa mitungi katika Mji wa Kibaha kinachotarajia kuanza baada ya miezi mitatu kutoka sasa.
Mwakalinga,amesema kuwa asilimia 98.9 ya Watanzania bado wanatumia mkaa na kuni na kwamba matumizi ya nishati mbadala haijafika asilimia 1 na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati mbadala.
Amesema, waandishi wa habari wanatakiwa kuchukua hatua ili kusaidiana na Serikali kuokoa mazingira hasa katika kupunguza wimbi la ukataji miti hovyo kwasababu ya kuchomea mkaa na kuni.
Mwakalinga amesema ili kufikia malengo ni vyema Serikali ikapandisha bei ya vibali vya uchomaji mkaa na kwamba kufanya hivyo itapunguza wimbi la watu kukimbilia kwenye mkaa na hivyo kutumia nishati mbadala kwa wingi.
Hatahivyo ,mmoja wa waandishi wa habari waliokuwepo katika ziara hiyo Julieth Mkireri kutoka gazeti la Nipashe aliishukuru Taifa Gas kwa kuona umuhimu kwa kuwashirikisha Wanahabari katika juhudi za kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala.
Mkireri , amesema kupitia mafunzo hayo watakwenda kuwa mabalozi wazuri katika kuandika habari ambazo zitasaidia kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukataji miti hovyo kwasababu ya kuchomea mkaa na kuni pamoja na kueleza faida za matumizi ya nishati mbadala ikiwemo LPG.
Post a Comment