BILIONI 23.49 KUJENGA BARABARA YA LAMI BUSWERU- NYAMADOKE - NYAMHONGOLO
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KIASI cha 23,490,253.00 (Bilioni 23.49) kinatarajiwa kutumika kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Buswelu-Nyamadoke-Nyamhongolo yenye urefu wa kilomita 9.5 na barabara ya Buswelu-Busenga-Coca Cola yenye urefu wa kilomita 3.3 ndani ya jimbo la Ilemela.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula katika viwanja vya shule ya msingi Nyamhongolo wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.
Dkt. Angeline amesema kuwa jimbo la Ilemela lina barabara zenye jumla ya urefu wa Km 878 huku Km 38.47 pekee zikiwa zimewekwa Lami sawa na 4%.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula (wa tatu kulia) akiwa amesimama na Baadhi ya viongozi na wananchi.
Amesema kutekelezwa kwa mradi huo wa ujenzi wa barabara kutasaidia kumaliza kero na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa barabara za uhakika kwa wananchi wa kata ya Nyamhongolo na Ilemela kwa ujumla wake.
"Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hasan, Kiukweli tumpe maua yake, ametoa zaidi ya Bilioni 33 kwaajili ya miradi ya maendeleo Ilemela ikiwemo na huu wa barabara na amesema mradi usianze kabla ya kulipa wananchi fidia zao’" Amesema.
Aidha Dkt Mabula ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kumuamini na kumteua kutumikia nafasi ya waziri wa ardhi kwa kipindi chote alichokuwa akiitumikia wizara hiyo pamoja na kumshukuru kwa fedha za maendeleo alizozitoa kwaajili ya miradi mbalimbali ndani ya jimbo lake.
Kwa upande wake mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga amesisitiza wananchi kuhakikisha wanalipa kodi za Serikali kwa kuwa kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo barabara za Lami.
Yusuph Ernest Bujiku ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela, amesema kuwa anaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo unaofanyika ndani ya wilaya yake, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuiunga mkono Serikali na viongozi wake.
Wakati huohuo, Dkt Angeline Mabula amepata wasaa wa kukabidhi mifuko ya Saruji 100 kwaajili ya ujenzi wa Zahanati za Bwiru kata ya Pasiansi na Lubala kata ya Kitangiri kila moja ikipata mifuko 50 iliyotolewa na Benki ya (TCB) Tanzania Commercial Bank.
Pia amekabidhi hati miliki kwa wananchi wanaopata huduma za Kliniki ya ardhi katika viwanja vya Furahisha, kukagua mradi wa maji Nyamhongolo na kuzungumza na mawakala wa mabasi katika stendi ya Mabasi na Malori Nyamhongolo.
Post a Comment