HEADER AD

HEADER AD

ZAHANATI SITA KUFUNGULIWA WILAYANI MASWA

Na Samwel Mwanga, Maswa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa katika mkoa wa Simiyu inatarajia kufungua zahanati sita zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo katika mwaka huu wa fedha 2023/2024.

Hatua hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuleta maboresho kwenye sekta ya afya.

        Mwonekano wa zahanati ya Isulilo katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ambayo imeanza kutoa huduma ya matibabu

Zahanati zinazotarajiwa kufunguliwa ni pamoja na Mwantumbe, Mwabayanda,Isulilo, Kizungu,Njiapanda na Mwanganda.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Maisha Mtipa wakati akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake mara baada ya kutembelea zahanati ya Isulilo iliyokamilika ujenzi wake na ambayo imeanza kutoa huduma Oktoba 2 mwaka huu.

       Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Maisha Mtipa akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani)juu ya ufunguzi wa zahanati sita katika wilaya hiyo

Amesema kuwa halmashauri hiyo imejipanga kutoa huduma ya Afya kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwafikishia kwa karibu huduma hizo kwa kufungua zahanati ambazo zitaleta chachu kwenye upatikanaji wa huduma za Afya wilayani Maswa.

"Katika sekta ya Afya pamoja na mambo mengine tumejipanga kwa mwaka huu wa fedha kufungua zahanati sita ambazo tayari zina usajili wa awali  na mojawapo ya zahanati ni hiyo ya Kijiji cha Isulilo ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi na malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunawasogezea wananchi huduma za afya huko huko walipo maeneo ya vijijini"

"Pia tumeamua kuzipandisha hadhi baadhi ya zahanati kuwa vituo vya Afya ambazo ni Zebeya ,Ipililo, Shishiyu, Mwabayanda (S)na tumepokea fedha nyingi kutoka serikalini zaidi ya  Bilioni Moja kwa ajili ya kujenga miundo hiyo pamoja na kununua Vifaa tiba,"amesema.

Kitanda cha kuzalishia katika Zahanati ya Isulilo iliyopo wilaya ya Maswa.

Aidha ametoa shukrani kwa serikali ya Awamu ya sita kwa kuendelea kuipatia fedha halmashauri hiyo kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma ya Afya.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Hadija Zegega amesema kuwa zahanati ya Isulilo ilipata usajili Mwezi Septemba mwaka huu na haikuweza kufunguliwa mapema kutokana na changamoto ya watumishi na Vifaa tiba lakini kutokana na uhitaji wa huduma ya Afya kwa wananchi wa Kijiji cha Isulilo ilibidi kuchukua baadhi ya Vifaa tiba kwenye zahanati ya Isanga na Hospitali ya wilaya ya Maswa ili ianze kutoa huduma ya matibabu.

       Mganga wa zahanati ya Isulilo,Anatory Edward akieleza jinsi walivyoanza kutoa matibabu mara baada ya zahanati hiyo kufunguliwa.

"Mara baada ya zahanati ya Isulilo kupata usajili kukawa na changamoto ya watumishi na Vifaa tiba tulichokifanya tulichukua baadhi ya Vifaa tiba katika Zahanati jirani ya Isanga na Hospitali ya wilaya yetu ya Maswa ili zahanati ianze kazi mara moja ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi,"

"Vifaa tiba ambavyo tuliviweka hapa ni pamoja na Vitanda ,magondoro na mashuka na Vitanda hivyo ni kwa ajili ya wagonjwa ambavyo vitatumika kwa kuwachunguzia wagonjwa na kuzalishia"amesema.

Dk Zegega ameendelea kueleza kuwa zahanati hiyo itapatiwa Vifaa tiba kutoka MSD muda wowote kuanzia sasa kwani wapo katika wilaya hiyo wakiendelea na usambazaji wa vifaa tiba pamoja na dawa katika Zahanati,vituo vya Afya na Hospitali ya wilaya.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Hadija Zegega(mwenye miwani)akiwa na Mganga wa zahanati ya Isulilo,Anatory Edward wakiangalia baadhi ya dawa na Vifaa tiba katika Zahanati hiyo.

Pia amesema kuwa tayari zahanati hiyo ina Mganga mmoja ambaye amehamishiwa hapo ambaye atasaidiana na wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kupata watumishi wengine katika Zahanati hiyo.

Diwani wa Kata ya Busangi, Paul Njige amesema kuwa zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu za Wananchi kwa kusaidiana na serikali pamoja na mfuko wa maendeleo wa Jimbo la Maswa Magharibi na kwa kuanza kutoa huduma kutapunguzia Wananchi wa Kijiji hicho kufuata huduma za Afya umbali mrefu wa kilomita 10 katika hospitali ya Wilaya ya Maswa.

Sehemu ya kuhifadhi Dawa katika Zahanati ya Isulilo wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu


Moja ya kitanda cha Wagonjwa katika Zahanati ya Isulilo iliyopo wilaya ya Maswa

No comments