HEADER AD

HEADER AD

NMB YAKABIDHI MADAWATI 200 SHULE NNE ZA MSINGI KIBAHA

Na Gustafu Haule, Pwani

WANAFUNZI 600 wa Shule nne za Msingi zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha wameondokana na adha ya kukaa chini baada ya Benki ya NMB kutoa msaada wa madawati 200,viti 16 na meza 8 yenye thamani ya Sh.milioni 25.

Shule zilizonufaika na msaada huo ni Kambarage,Lumumba,Kongowe na Bungo ambapo kila Shule imepata madawati 50 huku katika Shule ya Msingi Viziwaziwa ikipata viti 16 na meza 8 kwa ajili kuboresha ofisi ya walimu.

     Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kambarage iliyopo katika Kata ya Tumbi Halmashauri ya Kibaha Mjini wakifurahia kwa pamoja baada ya kupokea msaada wa madawati kutoka benki ya NMB.

NMB imekabidhi msaada huo Oktoba 10 mwaka huu katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kambarage huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam Dismas Prosper, amesema kuwa NMB imeweka utaratibu wa kila mwaka kusaidia jamii.

        Meneja NMB Kanda ya Dar es Salaam Dismas Prosper akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi msaada wa madawati katika Halmashauri ya Mji Kibaha Oktoba 10 mwaka huu.

Prosper,amesema kuwa kila mwaka  NMB imekuwa ikitenga asilimia 1 ya  faida yake na kurudisha katika jamii kwa kusaidia katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya na mpango huo ni endelevu nchini nzima.

Amesema kuwa,wameweka utaratibu huo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusimamia sekta ya elimu nchini hasa katika Shule za Mijini na Vijijini ili kuona wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.

        Meneja wa NMB Kanda ya Dar  es Salaam Dismas Prosper wa  pili kulia akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John msaada wa madawati 200,viti 16 na meza 8 yenye thamani ya Sh.milioni 25 kwa ajili ya Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji Kibaha.

"NMB imeweka utaratibu wake maalum wa kuhakikisha kila mwaka inatenga asilimia 1 ya faida yake na kurudisha kwa jamii katika kusaidia sekta ya elimu na afya,lakini leo tupo hapa kwa ajili kukabidhi madawati 200 ,viti 16 na meza 8 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa Shule nne na walimu wa Shule ya Viziwaziwa,"amesema Prosper.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John, ameishukuru NMB kwa kutoa msaada huo kwani umesaidia kuokoa wanafunzi wengi ambao walikuwa wakipata shida katika masomo yao.

     Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kambarage iliyopo katika Kata ya Tumbi Halmashauri ya Kibaha Mjini wakifurahia kwa pamoja baada ya kupokea msaada wa madawati kutoka benki ya NMB.

John ,amesema walichokifanya NMB ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na benki hiyo ili kuhakikisha wanatatua kwa pamoja changamoto za elimu zilizopo katika Shule mbalimbali.

Nae afisa elimu Awali na Msingi kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha Berdina Kahabuka,amesema msaada huo umesaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji ambapo ameomba benki hiyo kuendelea kusaidia na Shule zingine zilizopo katika Halmashauri hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Kambarage Happiness Msaki,amesema msaada wa madawati hayo umepunguza adha ya wanafunzi wake kukaa chini kwani awali kulikuwa na upungufu wa madawati 113 hali ambayo ilikuwa ikisababisha utoro na wengine kushindwa kufuatilia vizuri masomo yao.

       Meneja wa NMB Kanda ya Dar  es Salaam Dismas Prosper wa  pili kulia akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John msaada wa madawati 200,viti 16 na meza 8 yenye thamani ya Sh.milioni 25 kwa ajili ya Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji Kibaha.

Msaki , amesema kuwa Shule yake inajumla ya wanafunzi 878 na kwa wastani darasa moja linachukua wanafunzi 150 ambapo wengi wao walikuwa wanakaa chini lakini  baada ya NMB kutoa madawati hayo kwasasa wanaupungufu wa madawati 50.

Hata hivyo,baadhi ya wanafunzi wa Shule hiyo akiwemo Michael Daudi wa darasa la tano na Hasnat Said ,wameishukuru benki ya NMB kwa msaada huo kwakuwa utawasaidia kusoma katika mazingira mazuri.

No comments